Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula (kushoto) akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw Emmanuel Tutuba (wa pili kushoto) na Naibu Katibu Mkuu (Mawasiliano) Dkt Jim Yonaz (wa tatu kushoto) akisalimiana na Dkt. Godwill Wanda, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara Taifa, Baada ya Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA kufungwa rasmi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula (kushoto) akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA, jijini Dar es Salaam.
Na Faraja Mpina - WUUM, Dar es Salaam
MKUU wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainab Chaula ameiasa jamii ya kitanzania kutumia simu janja kutafutia fursa mbalimbali za kujitafutia kipato ili kuinua uchumi binafsi na nchi kwa ujumla. Dkt. Chaula alizungumza hayo alipokuwa akifunga Kongamano la Nne la Mwaka la TEHAMA lililofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 7 hadi Oktoba 9, 2020.
“Tuzitumie simu janja vizuri kwa kutafuta fursa za kutuinua kiuchumi, tusitumie simu hizo kuperuzi kwa ajili ya burudani pekee bali tufunguke, tutafute fursa za kiuchumi kwa kutumia simu janja zilizounganishwa na mtandao ili maendeleo yapatikane kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alizungumza Dkt. Chaula.
Dkt Chaula ametoa rai kwa wadau kutoka taasisi za umma na binafsi walioshiriki katika Kongamano hilo kutekeleza yale yaliyo ndani ya uwezo wao, wasiiachie Serikali ifanye kila kitu kwasababu fursa nyingi zinapatikana kwa wadau hao ,na kuwaasa wasitoe fursa kwa kufahamiana bali kwa kila mtanzania anayekidhi vigezo kulingana na Katiba, sheria na taratibu za nchi.
Aidha, Dkt. Chaula aliliambia Kongamano hilo kuwa, Wizara imepokea maoni yote yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa haraka, uaminifu na uadilifu mkubwa, ili fursa zilizobainishwa na masuala mengine yaliyojadiliwa ambayo yanahitaji mkakati wa kidijitali, kwa kushirikiana na wadau mkakati huo utaandaliwa na kutekelezwa kwa wakati.
Naye Mhadhiri kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dkt. Moses Mwasaga amesema kuwa matumizi stahiki ya simu janja yatawezesha watu wengi zaidi kuingia na kushiriki kwenye uchumi wa kidijitali kwa kupata huduma mbalimbali na kutengeneza ajira kama ilivyo kupitia mfumo wa miamala ya fedha kupitia simu ya mkononi, ambapo watu wengi wameweza kujiajiri kama mawakala wa kutoa huduma hiyo muhimu, ambayo hapo awali ilikuwa ikitolewa na benki pekee.
No comments:
Post a Comment