Jiwe la Pomonda moja ya vivutio vya utalii ndani ya ziwa Nyasa. |
Kaburi la pamoja la mashujaa 66 wa Vita vya Majimaji waliozikwa kaburi moja ndani ya Makumbusho ya Majimaji. |
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) Makao makuu jijini Dar es salaam Lunogelo Buhela akizungumza na wadau wa utalii mkoani Ruvuma, amesema sekta hiyo kwa miaka mingi imekuwa inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Kwa mujibu wa Buhela Taasisi yake inashirikiana na wataalam katika Mkoa wa Ruvuma ili kutengeneza mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
“Sekta ya utalii nchini Tanzania ni ya muhimu sana kiuchumi,utalii unaposhamiri una faida kubwa kwa serikali na watu binafsi,utafiti unaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma kwa miaka mingi umekuwa nyuma kuvuna fursa za utalii’’, alisema Buhela.
Kwa mujibu wa Mtafiti huyo Mwandamizi,katika watalii 300 wanaoingia Tanzania,Mkoa wa Ruvuma unapata mtalii mmoja tu jambo ambalo amesema limekuwa changamoto katika kukuza sekta ya utalii katika Mkoa huo.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini yenye vivutio vya utalii vya aina mbalimbali na ambavyo havipatikani sehemu nyingine yeyote duniani .
Amevitaja miongoni mwa vivutio adimu katika Mkoa huo kuwa ni ziwa Nyasa ambalo ni kitovu cha utalii kutokana na kusheheni aina zote za vivutio vya utalii,vivutio vingine ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Mto Ruvuma,makanisa makongwe,ngoma za asili,utalii wa kilimo cha Ngoro,mapango na mawe ya kihistoria.
Ameutaja mpango mkakati wa kukuza sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma kuwa unaweza kusaidia kuinua pato linalotokana na utalii ili kuchangia katika pato la Taifa na wananchi na kwamba watalii wanapoingia kwa wingi wanasisimua shughuli za kiuchumi kutokana na kulala,kunywa na kusafiri.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Jeremiah Sendoro amesema mpango mkakati huo utafanikiwa kwa sababu serikali imejitahidi kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Amesema serikali tayari imejenga miundombinu bora ya usafiri katika Mkoa wa Ruvuma zikiwemo barabara za lami,meli katika ziwa Nyasa,kuboresha uwanja wa ndege wa Songea, kuanzisha safari za ndege za abiria na wawekezaji kujenga hoteli za kisasa katika Mkoa wa Ruvuma.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe amesema ili mpango mkakati wa kukuza utalii upate matokeo chanya ni vema itolewe sera mpya ya utalii inayonufaisha mikoa ya kusini, elimu ya utalii iwe endelevu na matangazo ya kuvitangaza vivutio vya utalii mkoani Ruvuma yawe endelevu.
Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Jamii na Uchumi (ESRF) Lunogelo Buhela katika mahojiano nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. |
Hoteli yenye hadhi ya kitalii inayomiliwa na watawa wa kanisa katoliki Jimbo kuu la Songea,ina vyumba 35 imejengwa mwambao mwa ziwa Nyasa. |
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
No comments:
Post a Comment