MBINGA YATENGENEZA HATIMILIKI ZA KIMILA ZAIDI YA 26,000 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 11 October 2020

MBINGA YATENGENEZA HATIMILIKI ZA KIMILA ZAIDI YA 26,000

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akikata utepe kuashiria uzinduzi wa hati za kimila Hlalmashauri ya Wilaya ya Mbinga.



Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akimkabidhi mmoja wa wananchi hatimiliki katika Kata ya Nyoni Mbinga.


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipozindua mpango wa ugawaji wa hatimiliki za kimila kata ya Nyoni Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezindua mpango wa kugawa hati miliki za kimila zaidi ya 1000  katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

Mndeme  amezindua hatimiliki hizo katika kijiji cha Nyoni kati ya hatimiliki zaidi ya 26,000 zilizotengenezwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya kugawawiwa vijiji 86.

Mndeme amesema  Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ametimiza ahadi aliyotoa kwa  watanzania ya kuhakikisha migogoro ya ardhi inamalizika kwa kupanga kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi kwa kila mwananchi.

Mndeme amevitaja vijiji vitano vya Kata ya Nyoni ni kati ya vijiji 86  ambavyo vimenufaika na mpango wa hati miliki za kimila  katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga .

 Katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewakabidhi hati  wakulima 20 wa Kata ya Nyoni   kwa niaba ya kata 24 zilizopo ndani ya Halmashauri  ya Wilaya ya Mbinga.

“Naomba Kuanzia sasa watu wa Benki  mzitambue   nyaraka hizi za hati miliki za kimila kuwa ni halali na wanaweza kuzitumia sehemu yeyote na vyombo vya kisheria kwa sababu mashamba haya yanakwenda kutambulika rasimi”. Amesema Mndeme.

Mndeme pia amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kufanikisha zoezi hilo  ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja katika  upimaji wa mashamba ambao umehusisha vijiji 86 vyenye ekari takiribani 59,000.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye amesema atahakikisha kila kipande ambacho kipo katika halmashauri ya  Wilaya ya Mbinga kinapimwa  ambapo ametoa rai kwa wananchi  ambao hawajapimiwa kuondoa hofu kuhusu zoezi hilo ambalo ni endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mbinga Juma Mnwele, amesema ekari 70,000 ya mashamba ya mazao ya kudumu ambayo ni  sawa na mashamba 26,247 yametambuliwa na kupimwa.

Hata hivyo Mnwele amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeweza kutengeneza hatimiliki za kimila 26,247 katika vijiji 86  zilizogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja  na vijiji hivyo ni  kati ya  vijiji 117 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Naye mkulima  wa kijiji cha  Nyoni  Ponziana Nzuyu amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli  kwa kuwaunga mkono wakulima ambapo ametoa rai kwa wataalam kuendelea kuwaelimisha wananchi faida za hatimiliki.

Imeandaliwa na Albano Midelo

Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma


No comments:

Post a Comment