NCHIZA SADC ZATAKIWA KUPAMBANA NA UGAIDI NA UTASISHAJI FEDHA HARAMU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 13 July 2020

NCHIZA SADC ZATAKIWA KUPAMBANA NA UGAIDI NA UTASISHAJI FEDHA HARAMU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ambaye pia ni Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa Hazina wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Hazina na Magavana wa Benki Kuu za Jumuiya hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam
Na Farida Ramadhani, Dar es Salaam
NCHI za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimeshauriwa kuunganisha nguvu zao kupambana na changamoto ya utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa makundi ya kigaidi zinazotishia usalama na kuharibu uchumi wa nchi hizo  .
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mwenyekiti wa Maafisa Wandamizi wa HAZINA wa SADC, Bw. Doto James wakati akifungua Kikao cha Maafisa Waandamizi (Makatibu Wakuu) wa HAZINA na Benki Kuu wa nchi wanachama wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. James ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho kitakachofanyika kwa siku mbili, alisema kuwa changamoto hiyo imesababisha baadhi ya nchi wanachama kuingia katika orodha ya nchi zilizo kwenye athari ya kuingia kwenye vikwazo vya kimataifa kwa kushindwa kutimiza vigezo na masharti ya Kikosi cha Masuala ya Fedha (Financial Action Task Force), hali iyonaweza kuathiri malengo ya jumuiya ya kuvutia uwekezaji.
Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hiyo na nyingine kadhaa za kijamii, kimazingira na kiuchumi Jumuiya hiyo imeendelea kutekeleza azma yake ya kufikia malengo ya maendeleo iliyojipangia kupitia Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa SADC hali inayoashiria kuwa Jumuiya hiyo ni imara kutokana na kuwepo kwa sera nzuri na mifumo mizuri wa kitaasisi ndani ya Jumuiya hiyo.
“Pamoja na mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana kwa miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi wanachama zimeendelea kukabiliana na changamoto nyingine katika sekta za uchumi ikiwemo ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti na hii changamoto mpya ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona”, alisema.
Bw. James alisema katika kikao hicho Makatibu Wakuu hao watajadili na kutoa mapendekezo ya ajenda mbalimbali za masuala ya fedha na uwekezaji kwenye nchi za SADC ikiwemo athari za Kiuchumi na Kijamii zinazotokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 yatakayowasilishwa kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu wa SADC utakaofanyika tarehe 15 Julai, 2020
Alisema kuwa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji, pamoja na mambo mengine, wanajukumu la kusimamia itifaki ya Fedha na Uwekezaji katika Jumuiya ya SADC kwa lengo la kuhakikisha Sera na Maamuzi ya Baraza la Mawaziri wa SADC kwenye masuala yanaohusu Fedha na Uwekezaji vinatekelezwa.
“Ili kukabiliana na athari hizo, ni vema nchi wanachama kutumia mifumo ya kitaasisi katika kutafuta njia mbadala zenye ubunifu ili kuharakisha hatua za kuimarisha uchumi ndani ya jumuiya yetu, ni matumaini yangu kuwa kikao hiki ni njia muafaka katika kujadili changamoto za kiuchumi na kutoa mapendekezo ya kitaalam yatakayowasilishwa katika Mikutano ya Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kama ilivyoanishwa katika agenda za mikutano hiyo”, alisema Bw. James.
Alizitaja ajenda nyingine watakazo jadili na kutoa mapendekezo kuwa ni kupitia  taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano uliopita  wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji uliofanyika Windhoek, Namibia mwezi Julai 2019, kupokea na kujadili taarifa ya hatua iliyofikiwa ya namna uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC (SADC Regional Development Fund) na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maandalizi ya Miradi ya Maendeleo wa SADC (Project Preparation Development Facility).

Viongozi hao pia watajadili  na kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa Mfuko Maalum wa Kugharamia Miradi ya Muundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme (Regional Transmission Infrastructure Financing Facility - RTIFF) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, kupitia taarifa ya maendeleo ya Sekta ya Fedha ya Magavana wa Benki Kuu nakupitia taarifa ya utekelezaji wa masuala ya udhibiti wa fedha haramu.
Mkutano  wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu wa SADC unaondaliwa katika kikao hicho ulipangwa ufanyike kuanzia tarehe 13 hadi 17 Julai, 2020 lakini kutokana na mlipuko wa COVID-19, mkutano huu utafanyika kwa njia ya mtandao kama ilivyoelekezwa katika  Mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2020, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment