KIWANJA CHA NDEGE MSALATO KUANZA KUJENGWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 9 July 2020

KIWANJA CHA NDEGE MSALATO KUANZA KUJENGWA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (aliyevaa kofia), akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Bi. Bertha Bankwa, akieleza kuhusu maendeleo ya upanuzi wa kiwanja cha ndege mkoani hapo wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na sehemu ya maegesho ya ndege. Kushoto ni Meneja wa Wakala Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (aliyevaa kofia), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, alipokagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege na sehemu ya maegesho ya ndege. 

SERIKALI imewatoa wasiwasi wafanyabiashara na watumiaji wa usafiri wa anga kwa kuahidi kuanza ujenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Msalato jijini Dodoma mara baada ya taratibu zilizobaki kukamilika.

Akizungumza mjini humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya kutua na kuruka ndege na sehemu ya maegesho ya ndege Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kurahisisha usafirishaji kwa kuruhusu mashirika mengi zaidi kutumia kiwanja hicho.

“Niwahakikishie watanzania kuwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kitajengwa na kwa wakazi wa Dodoma ambao wanadai fidia, Serikali itahakikisha wanalipwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza idadi ya ndege ikiwemo ndege zenye uwezo wa kubeba abiria  zaidi ya 200 kwa wakati mmoja.
  
Naibu Waziri Kwandikwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha usafiri wa anga nchini kwa kuendelea na miradi mikubwa ya uboreshaji wa viwanja vya ndege zaidi ya kumi na moja nchi nzima vikiwemo vya Lindi, Songea, Shinyanga, Musoma, Songwe na  Mtwara.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amesema mradi umefikia zaidi ya asilimia 70 na kuahidi kuendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha viwango vinazingatiwa.

Mhandisi Chimwangu, ameongeza kuwa kwa sasa kazi zinazoendelea na ni kuweka tabaka la pili la barabara ya kuruka na kutua ndege mara baada ya tabaka la kwanza la kushindilia mawe kukamilika.

Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Bi Bertha Bankwa, amesema kuwa kukamilika kwa upanuzi wa sehemu ya maegesho ya ndege utaruhusu ndege zaidi ya nne kupaki kwa wakati ikiwemo ndege kubwa ya AIRBUS.

Mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, unafanywa na Kampuni ya CHICCO, na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5.

No comments:

Post a Comment