Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga. |
SERIKALI imesema haitopanga bei ya zao la pamba ya wakulima katika msimu wa mwaka 2020 unaotarajia kuanza mwezi huu ili kuwezesha soko kuamua na mkulima kupata soko la uhakika.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati akifungua kikao cha wadau wa zao la pamba kilichofanyika jijini Mwanza leo (07.06.2020) na kuwashirikisha wakuu wa mikoa 17 inayolima pamba nchini. Waziri Hasunga amesema kuwa serikali itakuwa msimamizi mkuu kuhakikisha maslahi ya wakulima wa pamba yanalindwa muda wote.
“Kazi ya serikali ni kuweka mazingira wezeshi ya biashara ya zao la pamba kufanyika kama ilivyo kwa mazao mengine.Hivyo leo hapa hatutapanga bei badala yake tunaachia soko liamue” alisema Waziri Hasunga.
Hasunga aliongeza kusema dhamira ya serikali ya awamu Tano ni kufanya Kilimo kuwa cha kibiashara na si cha kujikimu kwa wakulima kuondolewa vikwazo zaidi.
Aidha,amesema ni lengo la serikali kuhakikisha pamba yote ya wakulima inaongezwa thamani hapa nchini kwa kutumia viwanda vya ndani na kuwataka wafanyabiashara wengi kujitokeza kununua pamba yote ya wakulima.
Akihitimisha hotuba yake Waziri Hasunga alisisitiza kuwa serikali itahakikisha pamba ya wakulima inapata soko la uhakika kwa kuzingatia ushindani ili wakulima wapate faida.
" Nitashangaa kuona mzalendo wa Tanzania akinunua pamba kwa bei ndogo na kuwanyonya wakulima" alisema Hasunga.
Kuhusu kiwango cha uzalishaji kushuka Hasunga alisema kumetokana na uwepo wa mvua nyingi msimu huu na pia upungufu wa madawa na viuatilifu kwa baadhi ya wakulima.
" Tathmini ya awali imeonesha msimu huu uzalishaji pamba utashuka hadi tani 150,000 toka tani 348,000 msimu wa 2019 kutokana na mvua kuwa nyingi na kuathiri uzalishaji nchini" alisema Hasunga.
Hasunga aliwafahamisha wadau kuwa katika msimu uliopita wakulima nchini walipata zaidi ya shilingi bilioni 419 zilizotokana na mauzo ya pamba takribani tani 348,000 iliyozalishwa nchini mwaka 2019.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Kilimo alitangaza rasmi kuanza kwa msimu wa ununuzi wa pamba kuwa tarehe 15 Juni 2020 na kusema Bodi ya pamba ikamilishe taratibu zote za kuanza msimu ili wakulima wauze na kupata fedha zao kwa wakati.
Kwa upande wake Naibu Waziri Kilimo Hussein Bashe alisema ili kuhakikisha wakulima wanapata fedha zao kwa uhakika tayari akaunti 128,000 za benki zimefunguliwa na wakulima kwa ajili ya kutumika kulipa fedha zao.
Bashe amezipongeza taasisi za fedha kwa kufungua akaunti hizo za wakulima bure na kuwataka waendelee kufungua nyingi zaidi ili asiwepo hata mkulima mmoja asiye na akaunti.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano uliowezesha pamba ya wakulima msimu wa 2019 kupata mafanikio na wakulima kuweza kuuza pamba yote.
Naye mwakilishi wa wanunuzi wa zao la pamba Christopher Gachuma alisema wamejipanga tayari kuanza ununuzi wa pamba yote ya wakulima kwa kuzingatia bei ya soko.
Gachuma ameshukuru serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwahakikishia wanunuzi kuwa fedha zipo kwa ajili ya taasisi za fedha kukopa ili kununua pamba ya wakulima nchini.
No comments:
Post a Comment