WAZIRI WA KILIMO Mhe Japhet Hasunga na Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Bashungwa wamekutana na waandishi wa habari ili kuzungumza na umma wa Watanzania wote kuhusiana na Hali ya sukari nchini na mwenendo wa bei yake katika msimu huu wa uzalishaji wa sukari wa 2019/2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameanza kwa kueleza mahitaji na matumizi ya sukari nnchi ‘‘Mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida Nchini yanakadiriwa kufikia tani 470,000 kwa Mwaka. Kiasi hiki ni kwa wastani wa mahitaji ya kiasi cha tani 38,000 kwa kila Mwezi pamoja na kiasi cha tani 14,000 kwa ajili ya dharura.
Uwezo wa viwanda vyetu vya ndani kwa msimu wa 2019/20 kwa mujibu wa makadirio ya mwanzoni mwa msimu yaani Julai, 2019 ni kuzalisha takribani tani 378,000 za sukari. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 82.9 ya mahitaji halisi ya tani 456,000 ambayo hayajumuishi kiasi cha dharura cha tani 14,000.
Uwezo huu wa uzalishaji wa viwanda vya ndani unaacha pengo la kiasi cha tani 78,000 ili kuweza kutosheleza mahitaji halisi ya tani 456,000 bila kiasi cha dharura cha tani 14,000.
Hata hivyo, uwezo huu wa uzalishaji wa viwanda vya ndani ulitarajiwa kufikiwa pale tu panapokuwa na hali nzuri ya hewa na ufanisi mzuri wa viwanda’’
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameendelea kwa changamoto ambazo zimekumba msimu wa uzalishaji sukari wa Mwaka 2019/2020
‘‘Kutokana na ukweli kwamba msimu wa uzalishaji sukari wa Mwaka 2019/20 umekumbwa na changamoto kadha wa kadha zikiwemo
- Mvua nyingi kupita kiasi ambayo imepelekea uvunaji wa miwa kuwa mgumu,
- Mlipuko wa magonjwa ya miwa kama vile viding’ata wa njano n.k,
- Uharibifu wa mitambo ya baadhi ya viwanda na kuchelewa kupatiwa vipuri.
Sababu hizo zote kwa pamoja zimechangia kwa kiasi kikubwa Viwanda vyetu vya ndani kushindwa kufikia malengo ya kuzalisha tani 378,000 za sukari kwa msimu wa 2019/20.’’
Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Bashungwa ametoa hali ya uzalishaji wa viwanda vya sukari nchini:
‘‘Kutokana na hali halisi ya uzalishaji wa ndani wa sukari kuwa pungufu ya malengo ya uzalishaji, Serikali ilifanya makadirio ya kiasi cha sukari ya kuziba pengo la uzalishaji (gap sugar) na kutoa vibali kwa wazalishaji ili kuweza kuagiza na kuingiza sukari hiyo Nchini kwa wakati kwa ajili ya kukidhi mahitaji. Hadi hivi sasa tunazungumza na nyinyi, sukari iliyoagizwa kuja kuziba pengo la uzalishaji takribani tani 10,710 imeshaingia nchini na inaendelea kusambazwa katika Mikoa yote.
Mnamo tarehe 24, 28 na 30 Aprili, 2020 tunategemea kupokea jumla ya tani 13,500 za sukari ya kuziba pengo na tutaendelea kupokea kiasi kingine cha sukari Mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2020. Kiasi chote cha sukari kilichopo Nchini na tunachoendelea kupokea kinatosheleza kabisa mahitaji ya sukari nchini. Kwa taarifa hii, tuwaombe Wananchi wote kuwa watulivu kwa sababu Nchi yetu inayo sukari ya kutosha.’’
Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Bashungwa amesema serikali haitakubali kuona wafanyabiashara kupandisha bei kiholela
‘‘Tunapenda kuwatangazia Wafanyabiashara wote Nchini wenye tabia hizi za kupandisha bei kiholela waache mara moja kwani Serikali haipo tayari kuona Wananchi wake wanaumia kwa manufaa ya watu wachache.
Serikali itachukua hatua kali kwa Mfanyabiashara yeyote ambaye atabainika kujinufaisha kwa kuuza sukari bei ya juu kulikoni bei ya kawaida ya soko.’’
Aitha, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga kabla ya kutangaza bei ya sukari ya reja reja Katika Mikoa yote nchini amesema;
Kwa mujibu wa Sheria ya Sukari Na. 26 ya Mwaka 2001(Cap. 251) chini ya kifungu cha 11A inampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Kilimo kutangaza bei ya ukomo wa juu ya sukari.
Kutokana na changamoto ya wafanyabiashara kupandisha kiholela bei ya sukari nchini, Serikali tumeamua kuutangazia Umma wa Watanzania bei Kikomo ya sukari katika Mikoa yote Nchini Tanzania. Bei hizi kikomo zinalenga kukabaliana na changamoto ya kupanda kiholela kwa Bei ya Sukari Nchini ambayo kwa sasa imefikia wastani wa Shilingi 4,000/= hadi 4,500/= kwa kilo. Bei hii kikomo ya sukari imepangwa kwa kuzingatia gharama zote za uagizaji wa sukari ya kuziba pengo zinazotumiwa na wazalishaji kuagiza sukari kutoka nje ya Nchi.
Hivyo, kwa niaba ya Serikali tunapenda kuutangazia umma wa Watanzania kuwa bei ya sukari ya reja reja Katika Mikoa yote nchini itakuwa kama ifuatavyo;
KIWANGO CHA JUU CHA BEI YA SUKARI KWA REJA REJA KWA KILA MKOA
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amemaliza kwa kusisitiza kuwa;
‘‘Bei hizi za ukomo za sukari zimezingatia umbali wa kila eneo katika Mikoa yote nchini. Niwaombe Wafanyabiashara wote nchini kuzingatia maelekezo haya ya Serikali. Yeyote atakayekiuka maelekezo haya atakuwa ametenda kosa na hivyo atafikishwa katika vyombo vya sheria ili apate adhabu ambayo itahusisha ama kunyang’anywa leseni ya biashara, kulipa faini au adhabu zote kwa pamoja. Tutachukua hatua kali za kisheria kwa mfanyabiashara yeyote ambaye atakiuka masharti haya.’’
No comments:
Post a Comment