Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa akimkabidhi kadi ya pikipiki, Abdallah Juma wakati wa hafla ya makabidhiano ya zawadi kwa washindi iliyofanyika jijini Dar es Salaam. |
BENKI ya NMB imehitimisha kampeni yake ya Mastaboda, kwa kuwazawadia waendesha bodaboda watano kila mmoja pikipiki aina ya Boxer.
Madereva hao ni: Abdalla Said, Mohamed Salehe, Twaliha Mfinanga, Ramadhani Iddy na Adamu Gunza ambao wameibuka kidedea baada ya kufanya miamala ya juu zaidi kupitia Mastercard QR tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo.
NMB, kwa kushirikiana na Mastercard ilizindua huduma ya Mastercard QR mwanzoni mwa mwaka jana ikiwa na lengo la kumwezesha abiria wa bodaboda kulipa nauli kwa kutumia simu za mkononi na fedha hizo kwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya NMB ya dereva husika.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya zawadi iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa ameisisitiza jamii kufahamu umuhimu wa kutumia mfumo wa Mastercard QR hususani kipindi hiki ambacho dunia inapitia kwenye mlipuko wa ugonjwa wa ‘COVID-19’ unaosababishwa na virusi vya corona.
“Ukilipia nauli yako ya bodaboda kwa mfumo huu abiria na dereva wanapunguza uwezekano wa kupata au kusambaza ugonjwa wa COVID-19 kwa kuwa hakuna matumizi ya noti. Benki ya NMB ina mifumo rafiki ya kidigitali ya kuwawezesha wateja wetu kupata huduma zote za kukamilisha miamala kupitia simu zao za mkononi, ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma karibu zaidi kwa wateja,” amesema Baragomwa.
Washindi wakionyesha kadi za pikipiki baada ya kukabidhiwa. |
Naye Mkurugenzi wa Mastercard Afrika Mashariki, Frank Molla ameongeza kuwa ushirikiano wao na Benki ya NMB umelenga kuwasaidia wafanyabiashara kupokea malipo kwa mfumo wa kidijitali na kuwezesha miamala kufanyika kwa njia salama, rahisi na kutohitaji kuwa na pesa taslimu.
Hadi sasa kampeni hiyo imewafikia waendesha bodaboda 4,855, ikiwa ni safari ya kuwafikia bodaboda 75,000 nchi nzima ifikapo mwishoni mwa mwaka. Hadi sasa zaidi ya bodaboda 100 wamejishindia zawadi mbali mbali zikiwemo elfu hamsini zinazotolewa kila wiki, simu na watano ambao wamejishindia leo pikipiki.
No comments:
Post a Comment