NAIBU WAZIRI wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameridhishwa na kasi ya upanuzi wa Bandari ya Tanga baada ya kushuhudia kazi inayoendelea kufanyika kwenye bandari hiyo wakati wa ziara yake mkoani humo.
Nditiye amesema kuwa tayari Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 172 kwa ajili ya kupanua bandari hiyo kwa kuongeza kina cha sehemu ya kupakia na kupakua mizigo; ujenzi wa ghati na ukarabati wa ghala ili kuongeza uwezo wa bandari hiyo wa kusafirisha mizigo na bidhaa mbali mbali ndani na nje ya nchi.
“Tunategemea bandari hii itakapokuwa imekamilika ndani ya mwaka mmoja itaweza kuhudumia mizigo mingi sana kwa kushirikiana na bandari ya Dar es Salaam kwa sababu tunategemea iweze kuhudumia meli mbili zenye uzito wa tani 35,000 kwa mara moja, itakuwa ni bandari ya kisasa, kazi ya kwanza ya kuchimba kina imekamilika, sasa tunaenda kununua vifaa na itaenda sambamba na ujenzi wa ghati kubwa lenye urefu wa mita 500, tumejipanga kutekeleza IIani ya CCM kwa kuhakikisha kwamba vitu vyote tulivyoahidi, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Joh Pombe Magufuli alivyoahidi, na CCM ilivyoahidi kwa wananchi vinatekelezwa kwa wakati”, amefafanua Nditiye.
Ameongeza kuwa mizigo mingi iliyokuwa inakuja maeneo ya Kaskazini ikitoka nje ya nchi haitakuja tena mpaka Dar es Salaam, itakuwa inaishia Tanga ili watu wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga wapate mizigo yao kutokea bandari ya Tanga kwa kuwa Serikali imeimarisha reli, hivyo, mzigo ukishuka Tanga unaingia kwenye treni na kwenda kwenye mikoa hiyo na nchi za jirani zisizopakana na bahari zitapata huduma ya kusafirisha bidhaa na mizigo yao.
Pia, ameipongeza Bodi, Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na wafanyakazi wa bandari ya Tanga kwa usimazi wao mzuri walioufanya kwa kuwa kazi ambayo Serikali imetegemea imeanza kuonekana ya upanuzi wa bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa watu wengi waishio Tanga kwa kazi ambazo sio za kitaalamu.
Kaimu Meneja wa Bandari hiyo, Juma Mohamedi Juma amesema kuwa Menejimenti ya Bandari ya Tanga iko tayari kuchapa kazi na wanasimamia mradi huo ili uende vizuri na utakapokamilika utaongeza uwezo wa bandari hiyo wa kuhudumia meli kwa urahisi, kwa haraka na kupunguza muda wa kupakia na kupakua mizigo na bidhaa ambapo itavutia wafanyabiashara wengi zaidi kutumia bandari hiyo na utaweza kuhudumia eneo lote la nchi za Rwanda, Burundi na Uganda ambapo mkataba wa kipindi cha mwaka mmoja ulioanza kutekelezwa mwezi Oktoba mwaka jana umesainiwa baina ya TPA na mkandarasi wa kichina wa kampuni ya China Harbour Engineering Company Ltd kwa ajili ya upanuzi wa bandari hiyo.
“Hadi sasa kazi ya kuchimba ili kupanua kina cha bandari kwa ajili ya sehemu ya kupakia na kushusha mizigo imefikia asilimia 96; kazi ya kuleta vifaa ambavyo vinatengenezwa nje ya nchi na tukivileta nchini imefikia asilimia 20; na tupo ndani ya mkataba, na kazi hii ikikamilika tutakuwa na kina cha mita 13 kwenda chini tofauti na hapo awali tulikuwa na kina cha mita tatu tu, na tutakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 35,000 tofauti na hapo awali tulikuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 1,200 na kuwa na sehemu ya kuweka kontena 4,000,” amesema Juma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kupanua bandari ya Tanga kwa kuwa sasa wanajenga viwanda vingi hivyo upanuzi wa bandari hiyo utapanua wigo wa kibiashara, itaongeza mapato ya mkoa na wananchi kujipatia shughuli za kufanya za kuwaingizia kipato zitokanazo na shughuli za bandari.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment