Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki akielezea jambo kuhusu masula ya ajira wakati wa Mkutano huo. Kushoto ni Kamishna wa Kazi - Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Francis Mbindi. |
Sehemu ya Wajumbe wa
Mkutano huo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika Mkutano huo wa
Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa SADC sekta ya Kazi na
Ajira.
|
Na; Mwandishi Wetu
NCHI Wanachama wa Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimejizatiti kuimarisha Sera na kujenga
mipango ya pamoja itakayowezesha kukuza ajira kwa vijana katika Ukanda huo.
Akifungua Mkutano wa
Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na Wadau wa Utatu wa Jumuiya hiyo wanaosimamia
Sekta ya Kazi na Ajira hii leo Machi 2, 2020 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe alisema
kuwa Mkutano huo umewakutanisha Wataalamu wa sekta ya Kazi na Ajira kwa lengo
la kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazo jadiliwa katika Mkutano wa Mawaziri
ambao utafunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Alieleza kuwa ajenda
zitakazo jadiliwa ni pamoja na masuala ya kisera kuhusu ukuzaji wa ajira kwa vijana, pia masuala yanayohusisha uhamaji wa nguvu
kazi ndani ya jumuiya ya SADC ambapo itasaidia pia kutoa fursa ya kukuza ajira
kwa nguvukazi ya nchi wanachama.
“Itambulike kuwa uimarishwaji
wa sera katika sekta ya kazi na ajira utasaidia kwa kasi kikubwa kuwa chachu ya
maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa afrika endapo
itasimamiwa vizuri,” Alisema Massawe
Aliongeza kuwa kauli mbiu
ya Mkutano huo isemayo “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi
kwa Maendeleo Endelevu” inaelezea umuhimu wa sekta ya kazi na ajira katika
kuongeza tija ya ukuaji wa soko la ajira kwa nchi wanachama.
Naye Naibu Katibu Mtendaji
mwenye dhamana ya Utangamano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo alieleza kuwa
mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano uliofanyika mwezi Novemba 20, 2019
ulioshirikisha wataalamu na wadau wa utatu umechangia katika kujenga miongozo
sahihi na sera zitakazo wawezesha nchi wanachama wa SADC kukuza sekta ya kazi
na ajira.
Kwa Upande wake Mkurugenzi
wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw. Ally Msaki alisema kuwa Mkutano wa Mawaziri
utakao funguliwa rasmi tarehe 5 Machi, 2020 utawawezesha Mawaziri wa Nchi
wanachama wa SADC kujadili kwa pamoja ajenda mbalimbali zitakazokuwa zimepitiwa
kwenye kikao cha wataalam kwa lengo la kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini
na jumuiya hiyo kwa ujumla.
Hadi sasa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zilizoshiriki katika Mkutano huo
ni Angola, Afrika Kusini, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji,
Zambia, Zimbabwe, Malawi, Namibia, Eswatini, Lesotho, Jamhuri ya Shelisheli na
Tanzania.
No comments:
Post a Comment