RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein leo amongoza waombolezaji katika mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Brigedia Jenerali Mstaafu, Ramadhani Haji Faki yaliyofanyika Mkwajuni Zanzibar.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amemwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika mazishi hayo, alipata fursa ya kutoa salamu za pole za Rais kwa wanafamilia na ndugu wa marehemu baada ya mazishi .
Akitoa salamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Abood amemuelezea marehemu kuwa ni kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kutetea haki na kusimamia maendeleo katika nchi yetu.
“Aliweka mbele maslahi ya taifa na kuweka mbali maslahi yake binafisi ndiyo maana alishiriki katika vita kati ya Tanzania na Uganda vilivyomundoa madarakani Nduli Iddi Amini.”
Marehemu alizaliwa mwaka 1930 katika kijiji cha Mkwajuni, Kaskazini Unguja na mwaka 1983 hadi 1984 alikuwa ni Waziri Kiongozi wa Zanzibar.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu leo ametoa pole kwa familia ya Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine ambayo imeondokewa na Lazaro Edward Sokoine, aliyefariki Machi 28,2020 katika hospitali ya taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia Balozi Joseph Sokoine ambaye Pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, kesho kutakuwa na misa ya kumuombea marehemu kwenye kanisa katoliki Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es salaam.
Amesema mazishi yanatarajiwa kufanyika katika kijiji cha Embwiki Monduli Juu keshokutwa..
No comments:
Post a Comment