RAIS wa Marekani Donald Trump amefurahia ushindi baada ya kuondolewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, ndani ya Ikulu ya Marekani amewaponda wapinzani wake wa kisiasa.
''Nimefanya makosa kwenye maisha yangu, nitakiri......lakini haya ndio matokeo, '' alisema huku akinyanyua gazeti lililokuwa na kichwa cha habari ''Trump hana hatia''.
''Tumepita kubaya, hatukutendewa haki.Hatukufanya kosa lolote,'' alisema Ikulu. ''Ulikuwa uovu, ilikuwa rushwa.''
'' Sasa tuna neno zuri. Sikufikiria kama litakuwa zuri namna hii, ''Linaitwa kusafishwa kabisa.''
Trump alishtakiwa na bunge la wawakilishi mwezi Desemba kwa matumizi mabaya ya madaraka na kulizuia Bunge kutekeleza majukumu yake, lakini hakukutwa na hatia siku ya Jumatano baada ya mchakato wa majuma mawili wa kesi dhidi yake kwenye bunge la seneti linalodhibitiwa na chama cha republican.
Trump pia alieleza kuhusu uchunguzi uliokuwa ukifanyika kuhusu kampeni za uchaguzi wa mwaka 2016 na uhusiano na Kremlin.
''Ulikuwa upumbavu mtupu,'' alisema '' Hili suala halipaswi kutokea tena kwa rais atakayefuata.''
Trump alisema kuwa bado ana imani na chama cha Republican wakati huu wakielekea kwenye uchaguzi ujao wa mwezi Novemba.
Sherehe baada ya kusafishwa kwake kulitofautiana na rais Bill Clinton ambaye alihutubia mwaka 1999, alipoomba radhi kwa raia wa Marekani, baada ya kushtakiwa.
''Ninataka kusema tena kwa raia wa Marekani ninaomba radhi kwa kile nilichokisema na kwa mzigo mkubwa walioubeba wabunge na raia wa Marekani kwa ujumla,'' Bwana Clinton alieleza.
Alipokuwa akimaliza kuzungumza, Trump aliomba radhi kwa familia yake, kwa ''kupita kwenye misukosuko hiyo''.
Kwanini Trump hakupatikana na hatia?
Baada ya kesi iliyochukua takribani wiki mbili rais wa Marekani Donald Trump ameondolewa mashtaka na sasa anaweza kuendelea kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.
Ni matokeo yaliotarajiwa, lakini njia iliotumiwa kufikia uamuzi huo ndio iliyovutia.
Hizi hapa ni nambari nne zinazoelezea kesi hiyo. Na kile kitakachofanyika sasa.
Kuondolewa kesi kwa bwana Trump katika bunge la seneti kunaonesha umaarufu wake miongoni mwa wanachama wa chama cha Republican.
Iwapo haikuwa wazi kabla ya kesi hiyo kwamba alikuwa na uungwaji mkono katika wadhfa wake na chama chake basi ni wazi hivi sasa.
Hajawahi kupoteza umaarufu miongoni mwa wanachama wa Republican ama hata kuongeza umaarufu miongoni mwa wanachama wa Democrats.
Kulingana na kura ya maoni iliofanywa na Gallup wiki hii asilimia 94 ya Republicans wanaunga mkono utendakazi wa bwana Trump tangu achukue mamlaka.
Takwimu hizi zimeendelea kuimarika licha ya kesi iliokuwa ikimkabili.
Gallup pia iliripoti kwamba asilimia 89 ya wanachama wa Republican walimuunga mkono rais Trump katika mwaka wake wa tatu uongozini - hii ilimfanya kuwa rais wa pili mwenye umaarufu mkubwa kwa wakati wake kama rais miongoni mwa wanachama wa chama chake.
Haikuwa hivi. Miaka minne iliyopita wakati ambapo maafisa wakuu wa chama cha Republican walikuwa wanajiandaa kumshutumu rais Trump, mtu ambaye hatimaye alikuwa chaguo la chama chake kuwania kitu cha urais.
Mwaka 2016, seneta wa jimbo la Alaska, Lisa Murkowksi aliapa kutompigia kura . ''Iwapo tutamchagua Trump tutaharibikiwa'', alisema seneta wa jimbo la Carolina kusini Lindsey Graham.
Bwana Trump aliteuliwa kuwakilisha chama cha Republican na maseneta wote wawili bi Murkowski na Graham walikuwa katika sakafu ya bunge la seneti wakati wa kesi yake ili kumuunga mkono.
Kama ilivyodhihirishwa wakati wa uchaguzi wa kati kati wa 2018, wakati ambapo wanachama kadhaa wa chama cha Republican ambao hawakumuunga mkono bwana Trump walipoteza viti vyao , ambapo wafuasi wa chama cha Republican walikataa kumsamehe yeyote ambaye hakumuunga mkono rais Trump.
Umaarufu wake hata hivyo haumaanishi kwamba wafuasi wake wanaamini kwamba hakuwa na makosa katika kesi hiyo.
Katika kura ya maoni iliofanywa na AP na sio kituo cha utafiti wa umma NORC, wiki iliyopita asilimia 54 pekee ya wanachama wa Republicans wanaamini hakufanya makosa.
-BBC
No comments:
Post a Comment