SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR ZAAHIDI KUNDELEZA USHIRIKIANO KWENYE SEKTA YA UJENZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 13 February 2020

SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR ZAAHIDI KUNDELEZA USHIRIKIANO KWENYE SEKTA YA UJENZI

 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua jambo katika kikao kazi cha mashirikiano kwenye Sekta ya Ujenzi baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kilichofanyika kisiwani Pemba.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mustafa Aboud Jumbe, akizungumza jambo wakati akifunga kikao kazi cha mashirikiano kwenye Sekta ya Ujenzi baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kilichofanyika kisiwani Pemba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nyumba na Nishati kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Ali Khalil Mirza, akishauri jambo wakati wa kikao kazi cha mashirikiano kwenye Sekta ya Ujenzi baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kilichofanyika kisiwani Pemba.

Wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiwa katika kikao kazi cha mashirikiano kwenye Sekta ya Ujenzi baina ya Serikali hizo, kilichofanyika kisiwani Pemba.

Mjumbe Allex Mollel, kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), akichangia jambo katika kikao kazi cha mashirikiano kwenye Sekta ya Ujenzi baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kilichofanyika kisiwani Pemba.



SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimesema zitaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kuboresha miundombinu na usafirishaji ili kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch, Elius Mwakalinga, wakati akifungua kikao kazi cha mashirikiano kwenye sekta ya Ujenzi, baina ya Serikali hizo kilichofanyika kisiwani Pemba.

Mwakalinga, amesema kuwa kupitia Taarifa za utekelezaji ambazo  wakurugenzi wa Taasisi wameagizwa kuziwasilisha kwao, zitawsaidia wao kama Watendaji wakuu kujua namna gani ya kutatua chagamoto hizo kwa pamoja ili kufikia malengo waliojiwekea.

“Hatukuongea kisiasa, tumeongea kitaalaam namna ya kuboresha miundombinu na usafirishaji na tumepata maoni kutoka kwa wajumbe namna ya kuondosha changamoto katika masuala haya kati ya serikali hizi”, amesema Katibu Mwakalinga.

Aidha, Mwakalinga, amefafanua kuwa mkutano huo ni endelevu kwani nia na madhumuni yake ni kuhakikisha wanajadili changamoto na kupata maoni ya wataalam kwa pamoja ambayo yatasaidia katika kuboresha na kufanikisha maendeleo katika Sekta ya Ujenzi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu, hivyo pamoja na mambo mengine kikao hicho kimeazimia kwa kuwaagiza wakuu wa Taasisi ambao ni wajumbe katika kikao hicho kuandaa taarifa zao za utekelezaji na kuonesha changamoto zao ili kwa pamoja ziweze kutafutiwa ufumbuzi.

Ameongeza kuwa mikutano hiyo inatoa fursa kwa wajumbe kubadilishana uzoefu na hivyo kupata uelewa mpya ili kufanikisha maendeleo ya miundombinu baina ya Serikali hizo.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Ali Khalil Mirza, amesema kuwa kupitia vikao hivyo wataalamu kutoka pande hizo mbili watashauriana na kubadilishana uzoefu ambao utasaidia kuboresha utendaji kazi katika maeneo ya kazi.

Mjumbe kutoka Tanzania Bara ambaye ni Mkurugenzi kutoka Kitengo cha Usalama na Mazingira, Eng. Julius Chambo, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar (SMZ),  inashauriwa kuanzisha mizani katika barabara zao ili kuzilinda na ziweze kudumu kwa muda mrefu pamoja na kuweka mifumo ya kisasa ambayo itasaidia kupunguza mianya ya rushwa.

“Nashauri na nyinyi muanze utaratibu wa kujenga mizani kama sisi na kuweka mifumo ya kisasa kwenye mizani hizi, mathalani kwa upande wetu tangu tuweke mfumo wa kisasa katika mizani zetu, tayari  tumeshakamata watu 13 ambao wamekutwa na vitendo vya utendaji mbovu wa kazi”, amefafanua Chambo.

Mkutano huu wa mashirikiano umekutanisha wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT), kwa kuzihusisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati ambapo wajumbe hao walikutana na kujadili masuala mbalimbali yahusuyo Sekta ya Ujenzi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment