NEC YATOA MAFUNZO YA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA HALMASHAURI YA KINONDONI. - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 12 February 2020

NEC YATOA MAFUNZO YA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA HALMASHAURI YA KINONDONI.



Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk. Wilson Mahera Charles, akishuhudia watendaji waliokuwa wakifanya mazoezi ya kujifunza namna ya kutumia ( BVR KIT-Biometric Voters Registration Kit) wakati alipotembelea kukagua mafunzo hayo.

Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Vikroria Wihenga, Afisa Utumishi Bi. Faudhia Nombo, wakismikiliza Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk. Wilson Mahera Charles wakati alipotembelea kukagua mafunzo kwa watendaji yaliyokuwa yakitolewa na tume hiyo.

Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Bi. Vikroria Wihenga,akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dk. Wilson Mahera Charles wakatikati mwenye suti wakati alipotembelea kukagua mafunzo kwa watendaji yaliyokuwa yakitolewa na tume hiyo. Kulia ni Afisa Utumishi Bi. Faudhia Nombo.

Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Bi. Faudhia Nombo akizungumza na watendaji waliokuwa wakipewa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.



KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Bi Faudhia Nombo amefungua na kufunga  mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa watendaji wa kata ambao wanafahamika kama maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata.

Mafunzo hayo yaliyosimamia na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, yalianza kutolewa Februali 10 na kumalizika Februari  11 katika ukumbi wa Polisi Ofis Mes ambapo jumla ya Kata 20 zilizopo katika Halmashauri hiyo zilishiriki.

Akizungumza wakati wa kufungua na kufunga mafunzo hayo, Bi Faudhia alisema kuwa mafunzo hayo ni chachu kwa maafisa hao na kwamba wanapaswa kutumia nafasi hiyo vizuri ili kuisaidia Serikali kupata idadi kamili na sahihi ya wananchi watakaopiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Alifafanua kuwa  waandikishaji hao wasaidizi kwa ngazi ya kata wanapaswa kuhakikisha kuwa wanafuatilia na kusikiliza mafunzo hayo kwa umakini mkubwa kwani kazi hiyo ya uboreshaji wa dafatri ni nyeti na ni kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata ambapo yanahusisha mfumo mzima wa namna ya mchakato wa uandikishaji ambapo mfumo huo umegawanyika katika maeneo matatu.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni uandikishaji wa mwananchi mpya kabisa,  uboreshaji wa taarifa za mpiga kura kwenye daftari (hii ni iwapo mwananchi alihama eneo la makazi au iwapo taarifa zilikosewa) pamoja na kumuondoa mpiga kura kwenye daftari kutokana na sababu mbalimbali kama vile kifo.

Alisema mafunzo hayo pia yalitolewa kwa watendaji ambao watahusika na uingizaji wa taarifa za wapiga kura katika mfumo wa kuandikisha wapiga kura (BVR Kit operator) pamoja na waandikishaji wasaidizi.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo pia yalihusisha kuapishwa kwa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata, namna ya ujazaji wa fomu mbalimbali pamoja na namna ya kutumia sanduku litakalotumika kubeba vifaa mbalimbali vilivyounganishwa na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kuingiza taarifa binafsi za mpiga kura ( BVR KIT-Biometric Voters Registration Kit).

“ Naomba niwaeleze jambo moja, kazi hii mliyopewa ni muhimu kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba mwaka huu, tunaboresha daftari la wapigakura kwasababu, kuna wengine wametimiza miaka 18 hivi karibuni, wengine wamehama makazi yao, kwa hiyo huu mchakato ni muhimu sana ni waombe mkafanye kwa uangalifu mkubwa” kama mlivyo elekezwa na watoa mada” alisema Bi Faudhia.

Aliongeza kuwa” mnatakiwa kutumia lugha nzuri unapomuhoji mwananchi aliyefika kujiandikisha au kuboresha taarifa zake,tumeambiwa hapa na Maafisa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, uandikishaji huu hauhusiani na kitambulisho cha Taifa, kwa hiyo hata kama mtu atakuja kujiandikisha bila kitambolisho cha NIDA muandikisheni.

Zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni  litaanza rasmi Tarehe Februari 14 mwaka huu ambapo  litadumu kwa muda wa siku saba (7 ) na hivyo kumalizika Februari 21 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment