BENKI ya NMB, imetangazwa kuwa Mdhamini Mkuu wa Mbio za Bima Marathon 2020, zinazotarajiwa kufanyika Machi 28 jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Kampuni ya African Digital Banking Summit.
Kwa udhamini huo, mbio hizo zinazoenda kufanyika kwa mara ya pili mfululizo, zitatambulika kwa jina la NMB Bima Marathon 2020, ambazo zitahusisha mbio za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita tano. NMB imedhamini mbio hizo kwa kitita cha Sh. Milioni 35, ambako hafla ya NMB kutangaza udhamini wake huo katika mashindano hayo imefanyika jana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi ya udhamini, Meneja Mwandamizi wa Bima wa NMB, Martine Massawe, alisema wamevutiwa kudhamini Bima Marathon kutokana na mlengo wake.
"Mashindano haya yanatumika kama jukwaa la kutoa elimu ya Bima kwa Watanzania, lakini pia kuimarisha afya. Nasi tumeona ni fursa tunayoweza kuitumia kutangaza huduma mpya ya Bancassuarance. Lakini hii sio mara ya kwanza kwetu NMB kudhamini michezo, tumefanya hivyo katika soka ambako tumeidhamini Taifa Stars na timu za Azam FC na Singida United. Tumefanya hivyo pia katika mpira wa magongo, gofu na kriketi na kadhalika,” alisema Massawe.
Alitumia fursa hiyo kuwashauri Watanzania kujenga utamaduni chanya wa kutumia bima kadri ya mahitaji yao, kwa kutembelea matawi yote 224 kote nchini na kukata bima mbalimbali zikiwamo za maisha, magari, afya, nyumba, kilimo na dhamana kutoka kwa wabia wake.
Huduma za bima zitakazopatikana katika matawi ya NMB ni pamoja na zile za Kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Jubilee Insurance, Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) na Reliance Insurance.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya African Digital Banking Summit inayoratibu mbio hizo, Baraka Mtavangu, aliipongeza NMB kwa udhamini, anaoamini unaenda kubadili taswira ya mashindano hayo.
Alibainisha kuwa, mbio hizo zinatarajiwa kushirikisha wakimbiaji watu wazima wapatao 3,500 na watoto 500, na kwamba usajili unafanyika katika vituo mbalimbali, ikiwemo Mlimani city na baadhi ya matawi ya NMB kwa Sh. 20,000 kwa watu wazima na Sh. 15,000 kwa watoto.
“Kutakuwa na Washindi wa kwanza hadi wa tano katika mbio za kilomita 21 na kilomita 10, ambapo mshindi wa km 21 atajinyakulia sh. Mil. 1, huku mshindi wa km 10 atajishindia Sh. 700,000. Zawadi zingine zitatangazwa baadaye,” alisema Mtavangu.
Mratibu huyo alilishukuru Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kwa ushirikiano na kibali cha uendeshaji wa mbio hizo, ambazo alisema zitashirikisha Watanzania na wageni wanaoishi nchini, huku wakimbiaji wa nje wakitakiwa kujiandikisha kupitia chama cha riadha nchini.
#Umebima?
No comments:
Post a Comment