Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akiongea na wananchi wa kitongoji cha Mtwivila kilichopo katika kijiji cha Ukami wakati akiwaeleza lengo la kujenga kituo cha afya cha kata ya Mapanda.
Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa akiongea na wananchi wa kijiji cha Mapanda wakati akiwaeleza lengo la kujenga kituo cha afya cha kata ya Mapanda.
ZIARA ya mbunge wa jimbo la Mufindi
Kaskazini imeanza kuzaa matunda baada ya kuamua kuanza kujenga kituo cha afya
cha kata ya Mapanda ambacho kitakuwa msaada mkubwa katika kuboresha sekta ya
afya.
Akizungumza kwenye mikutano ya
hadhara ya vijiji vya Mapanda,Chogo,Ukami,Uhafiwa,
Ihimbo pamoja na vitongoji vya Mtwivila na Kisusa mbunge wa jimbo la Mufindi
Kaskazini Mahmoud Mgimwa alisema kuwa imefika wakati wa kuhakikisha wanapata
kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya katika kata hiyo.
“Mtake mistake kituo cha afya
kitajengwa hapa kwa mchango wangu kama mbunge,mchango wa serikali pamoja na
nguvu zenu wananchi kwa pamoja tutaweza kufanikisha swala hili na mimi kama
mbunge sipo tayari kuona kituo hiki hakijengwi,” alisema Mgimwa.
Mgimwa alisema kuwa wakianza
ujenzi wa kituo hiki cha afya cha kata atachangia mifuko mia mbili ya saruji
kwa awamu hiyo ya kwanza kama kuwaunga mkono ila ataendelea kuchangia katika
ujenzi wa kituo hicho cha afya.
“Mimi nimeanza kwa kuchangia
mifuko hiyo ya saruji ila nitawatafuta wadau wengine kuhakikisha wanatuchangia
ili kupunguza mzigo wa michango kwenu wananchi ambao ndio mmeniweka madarakani
hadi hii leo” alisema Mgimwa
Mgimwa alisema kuwa
atahakikisha wawekezaji wote ambao wanaizunguka kata ya Mapanda wanachangia
shughuli za maendeleo kwa kuwa wamekuwa wakitajilika kutumia ardhi iliyopo
katika kata hiyo.
Aidha Mgimwa alisema kuwa
wakianza ujenzi wa kituo hicho cha afya atahakikisha waziri wa TAMISEMI
Salemani Jafo anafika katika eneo la ujenzi na kutoa mchango wa serikali kwa
kuwa serikali huwa inachangia pale ambapo wananchi wameanza kufanya maendeleo.
“Waziri Jafo lazima atakuja tu
kufanya mkutano wa hadhara hapa katika eneo hili ambalo kituo cha afya
kitajengwa hicho wananchi lazima muanze ujenzi wa kituo hiki,” alisema Mgimwa.
Nao baadhi ya wananchi
waliohudhuria mikutano hiyo walisema kuwa wapo tayari kuchangia ujenzi wa kituo
hicho cha afya ili kuboresha sekta afya ambapo wamekuwa wakiteseka kwa kusafiri
umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment