WAZIRI MKUU AKAGUA UJEZI WA OFISI ZA HALMASHAURI NA HOSPITALI YA WILAYA RUANGWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 30 July 2019

WAZIRI MKUU AKAGUA UJEZI WA OFISI ZA HALMASHAURI NA HOSPITALI YA WILAYA RUANGWA



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo. Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa na yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi, alikagua ujenzi huo Julai 29, 2019. Jengo hilo linalojengwa na SUMA JKT, linahitaji sh. bilioni 3.77 hadi kukamilika kwake.

Akiwa kwenye eneo la ofisi hizo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Halmashauri hiyo. Ujenzi wa ofisi hiyo ambayo ikikamilika itakuwa na ghorofa moja, ulianza Juni mosi, 2019 na unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani. Jengo litakuwa na ofisi 33 za chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.

Kazi ambazo zimeshafanyika hadi sasa ni usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi; upimaji wa sampuli ya udongo (Geotech Survey); uingizaji wa maji eneo la ujenzi; uchimbaji wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji  na uvutaji wa umeme eneo la ujenzi. Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000 yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya matofali yote. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi unaendelea.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu jana alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa. Akiwa hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Mahela Njile kwamba hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa kugharimu jumla ya sh. bilioni 7.5 kulingana na maksio ya OR-TAMISEMI.

Dkt. Njile alisema katika awamu ya kwanza Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.

“Serikali imeelekeza ujenzi huu ufanyike kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri na kamati mbalimbali,” alisema.

Akizungumza na wakazi waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua kutumia force account ambayo alisema inapunguza sana gharama za manunuzi. Aliitaka Halmashauri hiyo isisubiri hadi kazi ya ujenzi ikamilike, na badala yake wahusika wajipange na kuanza kufanya usafi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo. “Halmashauri tusikae tu kusubiri ujenzi uishe. Tufanye usafi kuzunguka eneo lote, tupande miti na maua ili mandhari ianze kupendeza,” alisema.

Kuhusu muda wa kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu aliwashauri mafundi wazidishiwe muda wa kufanya kazi. “Badala ya kufanya kazi mchana peke yake, bora waongezewe muda wafanye hadi usiku ili kufidia muda uliopotea, na uliobakia ni mfupi mno,” alisema.

Alisema anaamini kazi hiyo itakamilika ndani ya muda mfupi ili huduma zianze kutolewa hapohapo Ruangwa na kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda hadi hospitali ya Ndanda.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema amekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuona shule ya sekondari Liuguru inabadilishwa na kuwa shule ya bweni kwa ajili ya wasichana pekee.

“Ndoto yangu ni kuona shule hii inakuwa ya wasichana peke yao. Na tukifanikiwa, tutatengeneza akinamama wasomi, wanaojitambua, wenye maadili mema na wachapakazi,” alisema.

Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Liuguru, kata ya Narungombe, wilayani Ruangwa Julai 29, 2019 mara baada ya kukagua shule hiyo. Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, alisema amechagua shule za Mnacho na Liuguru ziwe ni za bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike tu kama njia ya kuwaongezea fursa za masomo katika wilaya hiyo.

“Leo nimekuja kuwaeleza ndoto yangu. Tunahitaji kuona kila mtoto anayeenda shule, anakuwa na uhakika wa kumaliza masomo yake ya elimu ya juu. Wilaya hii tuna shida ya idadi kubwa ya mimba kwa watoto wa kike, na mimi hili jambo linanikera sana,” alisema.

“Tulikubaliana tuwe na kaulimbiu yetu kwamba ‘Ruangwa kwa maendeleo inawezekana’, lakini kwenye elimu tumekwama kuleta maendeleo kwa sababu dada zetu hawamalizi shule na sisi ndiyo wasababishaji. Tumeweka sheria ya kuwafunga watu wanaowapa mimba wanafunzi, lakini bado haisaidii.”

“Njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kufanya shule hizi ziwe za bweni ili wakae hapa shuleni, wafundishwe bila kupoteza muda wa kwenda nyumbani au kukutana na vikwazo wawapo njiani kuja shule au kurejea nyumbani,” alisema.

“Kwa wenzetu kwenye mikoa mingine, mtoto wa kike akianza shule ya awali, atamaliza ya msingi, ataenda sekondari hadi chuo kikuu. Akimaliza kusoma, anarudi nyumbani kuja kufanya kazi kwao na kuwasaidia wengine waliokosa fursa.” 

“Tunahitaji mabweni kwa ajili ya watoto wetu wa kike kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, tunahitaji nyumba za walimu ili wake hapa na kuwalea wanafunzi wetu. Yakikamilika, tutawahamisha wavulana wanaosoma hapa na kuwapeleka shule za jirani au za bweni, ili hapa tuwaachie wasichana peke yao,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema kwa kuanzia zitatumwa sh. milioni 100 ili zitumike kujenga nyumba nne za walimu, kisha atatafuta fedha nyingine ajili ya ujenzi wa mabweni, bwalo la chakula, jiko na mahitaji mengine kadri fedha zitakavyopatikana. 

Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wahakikishe wanakazania masomo kwani hakuna muujiza wa kufaulu mitihani kama hawatasoma kwa bidii. “Wanangu wa Form 2 na Form 4 hakuna muujiza wa kufaulu mitihani iliyo mbele yenu. Ni lazima msome kwa bidii. Na msikubali kuishia Form 4, lazima mwende Form 6 na mkimaliza hakikisheni mnafika chuo kikuu,” alisisitiza.

Mapema, akiwasilisha taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Samuel Diwani alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007, hivi sasa ina walimu 11 ambapo watatu kati yao wanafundisha masomo ya sayansi na wanane waliobakia wanafundisha masomo ya lugha na sanaa.

Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 109 ambapo 51 kati yao ni wavulana na 59 ni wasichana, inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa nyumba tisa za walimu, ukosefu wa maabara mbili na iliyopo moja haijakamilika kwa asilimia 100. Nyingine ni ukosefu wa mabweni, maabara ya kompyuta, mfumo wa umemejua, maktaba, jengo la utawala na stoo.

No comments:

Post a Comment