Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari wa mitandao ya Kijamii.
Wanahabari wa mitandao mbalimbali ya kijamii wakimsikiliza Mh. RC Makonda katika mkutano na wanahabari hao. |
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akifafanua jambo alipokuwa katika mkutano wake na waandishi wa habari wa mitandao ya Kijamii. |
Na Mwandishi Wetu
MAMILIONI ya shilingi yametengwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kama zawadi kwa ajili ya waandishi wa habari watakao shinda shindano la kuuliza maswali wananchi kuhusiana na Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam-Tanzania.
Akizungumza ofisini kwake leo Makonda alisema shindano hilo litawahusu waandishi wa habari wanao endesha mitandao yote ya kijamii, Online TV, Blog, Twitter, Website, Facebook na Instagram.
Alisema maswali yatakayoulizwa ni 12 ambayo yameandaliwa na ofisi yake, ambapo mwandishi mshindi kwa kuuliza atajinyakulia kitita cha shilingi milioni tatu huku mwananchi atakayejibu vizuri maswali hayo naye atapata sh.100,000.
Alisema kuwa maswali mengine 12 yatabuniwa na waandishi wenyewe lakini yanatakiwa yawe yenye mvuto na kusisimua yakilenga mada ya mkutano wa SADC na mshindi wa eneo hilo pia atajinyakulia milioni tatu na mwananchi atakaye yajibu kiufasaha ataondoka na sh.100,000.
"Maeneo litakapofanyika shindano hili ni sehemu za Bar, Saluni, kwenye vijiwe vya waendesha bodaboda, masokoni na kwa wamachinga ambapo waandishi watawauliza maswali mbalimbali ya jinsi wanavyoijua SADC na watakaojibu kwa usahihi watajinyakulia kiasi hicho cha fedha" alisema Makonda.
Alisema baada ya mahojiano hayo kila mwanahabari atayarusha hewani kwa kutumia mtandao wake.
Makonda alisema mshindi wa kwanza wa shindano hilo atapata sh.milioni tatu, mshindi wa pili milioni mbili na mshindi wa tatu milioni moja na kuwa sherehe ya kukabidhi fedha hizo kwa washindi itafanyika Agosti 5 mwaka huu katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Shindano ili linafanyika ikiwa ni moja ya hatua ya hamasa kuelekea mkutano mkuu wa SADC ambao unatarajiwa kufanyika hapa nchini hivi karibuni ambao utaongozwa na Rais Dkt.John Magufuli.
No comments:
Post a Comment