![]() |
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa safari ya miaka mitano ya Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania (SAUT) kuelekea Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa hicho mwaka 1998. Uzinduzi huo umefanyika kwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la ukumbi wa mikutano unaojengwa kwa matumizi ya kitaaluma na kijamii. Wa pili kushoto ni wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala na Makamu wa Mkuu wa Chuo Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu (wa tatu kutoka kulia).
Na Eleuteri Mangi-SAUT
CHUO Kikuu cha Mt.
Augustino Tanzania (SAUT) kimezindua safari ya miaka mitano kuelekea Jubilei ya
miaka 25 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998. Uzinduzi huo umefanywa na Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa uliofanyika
chuoni hapo kwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la ukumbi wa mikutano
unaojengwa kutumika kwa shughuli mbalimbali za kitaaluma na kijamii.
Akiongea na hadhira ya
viongozi mbalimbali, wahadhiri, wanafunzi pamoja na wananchi waliohudhuria katika tukio hilo liliotanguliwa na ibada ya
misa takatifu iliyongozwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo
Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala, Rais Mstaafu Mkapa amesema kuwa vyuo
vikuu vya binafsi vinamchango mkubwa nchini katika kutoa elimu kwa Watanzania
bila kujali dini zao wala makabila yao hatua ambayo itawaweze kutoa mchango
katika kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi ya uchumi wa kati
ifikapo mwaka 2025.
Kuhusu Sera ya
Maendeleo ya Taifa, Rais Mstaafu Mkapa amesema kuwa elimu ya juu ina mchango
kwa taifa kwa kuzalisha wataalam wengi wenye ubora, ujuzi na uwezo wa kutatua
matatizo ya jamii, kukabiliana na changamoto za maendeleo ili kufikia ushindani
katika ngazi za kikanda na za kimataifa.
“Serikali inatambua na
inathamini mchango wa sekta binfsi katika vyuo vikuu kwa kutoa elimu nchini,
vyuo vikuu binafsi vina nafasi ya kuzalisha wataalamu mbalimbali kwa manufaa
kwa mtu mmoja mmoja, jamii, taifa na hata nje ya mipaka ya Tanzania.” amesema
Rais Mstaafu.
Katika kukuza na
kupanua wigo wa kutoa elimu ya juu nchini, Rais Mstaafu Mkapa atakumbukwa kwa
mchango wake wa kuwezesha dini mbalimbali nchini kuwa na vyuo vikuu vyake
ikiwemo Chuo Kukuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) kinachomilikiwa na
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Chuo Kikuu cha Kiislamu cha
Morogoro (MUM) kinachomilikiwa na Kinachomilikiwa na Baraza la Waislam Tanzania,
Chuo Kikuu Cha Mt. John Dodoma kinachomilikiwa na Kanisa la Waangikana Tanzania,
Chuo Kikuu cha Tumaini kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania pamoja na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Sebastian Kolowa.
Kwa upande wake Makamu
wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza
la Chuo cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Askofu Flavian Kassala
ameishukuru Serikali ya Tanzania kuwa msaada kwa kwa sekta binafsi ambapo
baraza hilo linathamini na linaiunga mkono Serikali kwa kutoa elimu nchini ili
wanaoipa waweze kutoa msaada kwa watu wanaohitaji msaada huo kwa wakati.
“Kanisa linatoa
shukrani kwa Serikali, watu binafsi na taasisi zinazoendelea kutoa mchango kwa
SAUT, elimu tunayotoa katika ngazi zote imewasaidia watu kutatua matatizo
katika mazingira yao” amesema Askofu Kassala.
Aidha, Askofu Kassala
aliendelea kusema “Tunajenga watu ambao wanazingatia maadili na utu wa mtu kwa
kusaidia jamii inayohitaji msaada kutoka kwa watu ambao wamepata elimu, SAUT
inamchango mkubwa katika kuwajenga na kuwalea watu kiroho na kimwili kupitia
elimu” alisisitiza Askofu Kassala.
Naye Makamu wa Mkuu wa
Chuo hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu amesema chuo chao kinaendelea
kuzalisha wataalam kwa kwa ajili ya nchi hatua ambayo amemshukuru Rais Mstaafu Benjamin
Mkapa kuwa mlezi na msaada mkubwa kwa maendeleo ya SAUT.
Balozi Prof. Mahalu
amesema kuwa wataalamu wanaoandaliwa katika chuo hicho watokana na vitivo
vingine vinne (4) ambavyo ni Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano ya Umma,
Kitivo cha Biashara na Utawala, Kitivo cha Ualimu, Kitivo cha Sheria na Kitivo
cha Uhandisi.
Hatua hiyo imeungwa
mkono na Waziri wa Madini Dotto Biteko ambapo alitoa wito kwa Wanzania na
wanafunzi wanaosoma na wanaotarajia kujiunga na chuo hicho kuwa katika utoaji
wa elimu ya juu SAUT imejipambanua kuwa ni kinu cha kuandaa wanataaluma na
viongozi mbalimbali nchini.
“Tunabahati ya kuzaliwa
kwenye nchi yenye usawa na haki, SAUT inatoa haki ya elimu kwa vijana wetu
hatua inayowapelekea kuhama kwenye taifa la kulalamika na kuwa taifa la watu wa
matokeo, tunathamini kazi inayofanywa na chuo hiki ambacho kimekuwa kuwa chachu
ya malezi kwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.” Alisisitiza Waziri
Biteko.
Chuo Kikuu cha SAUT
kinamilikiwa na kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa
kwa mujibu wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu
Tanzania (TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka
2005 ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa
katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa chini ya
Askofu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu la Mwanza.
No comments:
Post a Comment