*Ni baada
kuifunga Lipuli fainali za ASFC
TIMU ya Azam FC imefuzu
michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika msimu ujao baada ya kuifunga
Lipuli FC bao 1-0 kwenye fainali za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Mbali na kufuzu kushiriki
michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika, timu ya Azam imeondoka na kitita cha
sh. milioni 50, medani pamoja na kombe.
Fainali hizo zimefanyika Juni
1, 2019 katika uwanja wa Ilulu, Manispaa ya Lindi ambapo ushindi huo unaifanya
Azam FC kuungana na Simba kuliwakirisha Taifa kwenye michezo ya Kimataifa
itakayoanza Novemba mwaka huu.
Mshambuliaji wa Azam
Obrey Chirwa ndio aliyeiwezesha timu yake ya Azam kuibuka na ushindi katika
mchezo huo baada ya kufunga bao la ushindi katika kipindi cha pili.
Katika mchezo huo
ulioshuhudiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, timu ya Lipuli FC iliyong’ara kwa
kutawala mchezo kwenye kipindi cha kwanza, ilishindwa kutumia nafasi nyingi
ilizozipata kuifunga Azam.
Mbali na timu ya Lipuli
kuwa mshindi wa pili katika mashindano hayo, pia timu hiyo imetoa mchezaji bora
wa mechi ya fainali, Paul Ngalema pamoja na mfungaji bora wa mashindano hayo
Seif Rashid.

No comments:
Post a Comment