SERIKALI ya Marekani Yatoa Misaada Yenye Thamani ya Dola
750,000 Ili Kutengeneza Ajira Kwa Vijana wa Vijijini Mbeya, Tanzania - Mei 29,
2019, Serikali ya Marekani ilitoa misaada yenye thamani ya dola 750,000 kwa
taasisi tisa ambazo zinasaidia utengenezaji wa ajira, ujasiriamali, uongozi, na
maisha bora kwa vijana.
Misaada hiyo
inatolewa na mradi wa Inua Vijana wa Feed the Future Tanzania , inayofadhiliwa
na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa
(USAID), na wanatarajia kutengeneza ajira 950 kwa vijana katika makampuni 700
mapya au ambayo yanaongozwa na vijana katika mikoa ya Iringa, Mbeya, na
Zanzibar.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andrew Karas, na Mheshimiwa
Suleiman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), walikabidhi misaada hiyo kwa taasisi husika.
Wakati wa hotuba yake, Bwana Karas alibainisha kuwa
“Kuwekeza katika uongozi wa vijana nchini Tanzania ni kipaumbele cha USAID na Serikali
ya Tanzania. Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana, na idadi ya wananchi wake
inatarajiwa kuongezeka mara mbili ndani ya miaka 25 hadi 30 ijayo.
Jitihada za makusudi zinahitajika kwa serikali, sekta
binafsi na jamii ili kuhakikisha kuwa nguvu, vipaji, na matumaini ya vijana wa
leo, pamoja na kizazi kijacho, zinafanya Tanzania kuwa mahali pa mafanikio kwa
wote.”
Mradi wa Inua Vijana unahamasisha vijana wa vijijini
kushiriki katika sekta ya kilimo nchini Tanzania na kuwapatia fursa za kiuchumi
vijana wenye umri wa miaka 15-35 pamoja na kuhamasisha uongozi na mienendo ya
kiafya. Kupitia misaada hii, Inua Vijana ya Feed the Future Tanzania itabadili
changamoto kuwa fursa kwa vijana wa vijijini kuongoza na kushiriki katika
ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

No comments:
Post a Comment