BENKI YA NMB YASAIDIA VIFAA KITUO CHA AFYA MIRERANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 2 March 2019

BENKI YA NMB YASAIDIA VIFAA KITUO CHA AFYA MIRERANI

Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenesta Mhagama (kulia) baadhi ya vifaa tiba vilivyotolewa na NMB kwenye Kituo cha Afya Mirerani. Vifaa vilivyotolewa ni vitanda vitatu maalum kwa kujifungulia, vitanda 6 vya kulalia wagonjwa na magodoro yake, mashuka 70 na vifaa vya kupima kasi ya moyo, vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni 10.

Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi  akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenesta Mhagama (kulia) baadhi ya vifaa tiba vyenye thamani ya Sh Milioni 10 vilivyotolewa katika Kituo cha Afya Mirerani.

Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenesta Mhagama (kulia) juu ya vifaa tiba vilivyotolewa katika Kituo cha Afya Mirerani. Vifaa vilivyotolewa ni vitanda vitatu maalum kwa kujifungulia, vitanda 6 vya kulalia wagonjwa na magodoro yake, mashuka 70 na vifaa vya kupima kasi ya moyo, vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni 10.

NA MWANDISHI WETU, SIMANJIRO

BENKI ya NMB imetoa msaada wa vitanda vya kujifungulia pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh Milioni 10 katika Kituo cha Afya Mirerani kilichopo mkoani Manyara. Vifaa hivyo vimekabidhiwa wakati wa ufunguzi wa Kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU), Mirerani, kituo kilichojengwa na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF).

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi alivitaja vifaa hivyo kuwa ni vitanda vitatu maalum kwa kujifungulia, vitanda 6 vya kulalia wagonjwa na magodoro yake, mashuka 70 na vifaa vya kupima kasi ya moyo, huku vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni 10.

"Napongeza Serikali kwa juhudi za kuboresha huduma za afya, NMB tunajua ni muhimu wadau binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali na ndiyo maana huwa tunatenga asilimia moja baada ya kodi kusaidia sekta ya elimu na afya," alisema Mponzi.

Awali akizindua Kituo hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenesta Mhagama, amewataka viongozi, wananchi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika eneo la Mji Mdogo wa Mirerani, Mkoani Manyara, ambalo lina asilimia 16 ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Amesema jitihada za wadau zinahitajika ili kupunguza maambukizi mapya katika eneo hilo kwani Mamlaka ya mji mdogo ina maambukizi makubwa ikilinganishwa na maambukizi ya Mkoa mzima wa Manyara ambayo ni asilimia 2.3, huku akikemea vitendo vya unyanyapaa kwa walio na maambukizi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, amesema bado kuna tatizo kubwa nchini la watu wengi kutokujitokeza kupima Ukimwi na ndiyo maana wamelazimika kusogeza huduma ya Kituo hicho katika eneo la Mirerani hususani kwa ajili ya wachimbaji.

Amesema kuwa licha ya Kituo hicho kulenga wananchi wote,kitasaidia wachimbaji wengi kuhamasika kupima ili wajue afya zao na kuiomba Serikali na wadau kwa ujumla kufanya survey katika migodi yote nchini ili kujua hali ya maambukizi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenesta Mhagama (kulia) akiangalia sehemu ya vifaa vya afya vilivyotolewa na Benki ya NMB.

No comments:

Post a Comment