Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiongea na wananchi wa
Dodoma kabla ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 20.6 kwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Dkt. Binilithi Mahenge (hayupo pichani) kwa ajili ya mradi wa kufyatua matofali wa kikundi cha vijana,
Dodoma.
NAIBU Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka kampuni za simu za
mkononi nchini kurudisha faida kwa jamii ambayo ni wateja wake na wanatumia
huduma za mawasiliano za kampuni zao.
Nditiye ameyasema hayo
wakati akikabidhi vifaa mbali mbali vya hospitali kwa ajili ya kuhudumia
wagonjwa ikiwemo vitanda, neti, mashuka na aproni vyenye thamani ya zaidi ya shilingi
milioni sita kwa niaba Serikali kwa Hospitali ya Makole iliyopo Dodoma
vilivyotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.
“Nitoe wito kwa
kampuni nyingine za simu za mkononi ziige mfano wa Halotel wa kurudisha
shukrani kwa wananchi,” amesema Nditiye.
Pia ameongeza kuwa
mawasiliano ni moja ya Sekta ambayo inashika nafasi ya tano kwa maswali Bungeni
ikiwemo Sekta nyingine za maji, afya, elimu, umeme, barabara ambapo Wabunge wamekuwa
wakiuliza maswali mara kwa mara kuhusu Sekta ya Mawasiliano ambapo
inadhihirisha kuwa wananchi wanatambua na kuthamini mchango wa mawasiliano
katika maisha yao ya kila siku kwa kuwa mawasiliano ni uchumi na ni maendeleo.
Vile vile amezitaka
kampuni za simu za mkononi nne zilizosaini mkataba na kupewa ruzuku na Serikali
kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mwezi Desemba mwaka jana ikiwemo
Vodacom, TIGO, Halotel na Shirika la Mawasiliano Tanzania kujenga minara ya na
kupeleka huduma za mawasiliano haraka kwa wananchi.
Naye Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Makole, Dodoma Dkt. George Matiko akipokea misaada hiyo
ameishukuru kampuni hiyo na kusema kuwa anaipongeza kwa kuunga mkono jitihada
za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za
kuboresha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya nchi nzima na kuongeza fedha
za kununua dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambapo hadi sasa hospitali hiyo
imepokea shilingi milioni 500 kutoka Serikalini ambapo zimewezesha ukarabati wa
hospitali hiyo na kuongeza utoaji huduma kwa wanawake 2,000 waliojifungua na
kufanya operesheni kwa wagonjwa 300.
“Tunashukuru kwa
jitihada zenu Halotel, mahitaji bado ni mengi, muendelee kutuunga mkono katika
kuwahudumia wananchi,” amesisitiza Dkt. Matiko.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Halotel, Tanzania Nguyen Van Son amesema kuwa wameamua kurudisha
faida na kutoa shukrani kwa wananchi kwa kuwaunga mkono kwa kutumia huduma za
kampuni yao ambayo imesambaa nchi nzima na inatoa huduma kwenye maeneo yote ya
mijini na hasa vijijini.
Nguyen ameishukuru
Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki yaliyowavutia kuweza nchini
kwenye Sekta ya Mawasiliano na wamedhamiria kuendelea kushirikiana na Serikali
na wananchi kwa ujumla ili kupanua huduma za mawasiliano na kuhakikisha kuwa
zinakuwa za viwango, ubora na gharama nafuu kwa mtumiaji.
Katika hatua nyingine,
Nditiye kwa niaba ya Serikali, ameshuhudia makabidhiano ya hundi ya shilingi
milioni 20.6 baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilithi Mahenge na Nguyeni
kwa ajili ya uanzishaji wa kiwanda cha kufyatua matofali cha kikundi cha vijana
wa Dodoma ambapo makabidhiano hayo yamefanyika kwenye viwaja vya Barafu mjini
humo.
“Vijana wa Dodoma
mtanufaika na Serikali kuhamia Dodoma, tumeona tuanzishe kikundi cha vijana ili
waweze kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali na mradi huo utakuwa na vijana
wa kutoka Jeshi la Kujenga Taifa ili wawasaidie ili baadae vijana waweze
kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao,” amesema Dkt. Mahenge.
Pia, ametoa rai kwa
vijana wajitokeze na kuchamkia fursa mbali mbali zilizopo mkoani humo na
wasikubali kukaa bure, wajihusishe na shughuli za uzalishaji, wasikubali kukaa
nyumbani na vijiweni.
|
No comments:
Post a Comment