Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy
Matamwe akimsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa, Asajile
Mwambambale, wakati alipofika ofisini
kwake kwa ajili ya kufuatialia hatua za
menejimenti ya maafa wilayani humo.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy
Matamwe akikagua sehemu ya tuta la mto Mkondoa Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro,
Tuta hilo lenye urefu wa Kilometa 4, tayari kilometa 1 ya tuta hilo imeshaathiriwa
na maji ya mto huo. Wakati alipofika wilayani humo kukagua shughuli za
menejimenti ya maafa.
Akiongea wilayani Kilosa wakati wa kufuatilia hatua za urejeshaji hali kutokana na athari za maafa ya mafuriko yaliyotokana na mvua zilizonyesha, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe ameeleza kuwa wamelipokea ombi hilo ambalo ni muhimu kutekelezwa kwa ajili ya kupunguza athari za maafa wilayani humo.
“Mvua zinaponyesha na tukawa na utaratibu mzuri wa kuyavuna maji hayo,
matokeo ya mvua hizo huwa zinachochea shughuli za maendeleo hasa kilimo, lakini
bila kuyavuna maji yanaweza kusababisha maafa kama mafuriko. Kwa kulitambua hili, tutaratibu
wizara husika kuhakikisha mabwawa yanafufuliwa ili kuhifadhi maji na kupunguza
maji mengi yanayoingia mto Mkondoa” Alisisitiza Kanali, Matamwe.
Kanali Matamwe amewataka wananchi wa kilosa kutoendeleza shughuli za
kibinadamu kando ya mto huo kutokana na kuwa serikali imetumia gharama kubwa za
kujenga tuta la mto Mkondoa kwa lengo la kupunguza athari za maafa yaliyokuwa
yanatokea baada ya mto huo kujaa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ambaye
pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Wilaya ya Maafa Bw. Asajile Mwambambale,
amefafanua kuwa ipo haja ya kuharakisha ujenzi wa bwawa la Kidete ili kuweza kupunguza kasi ya maji
ma wingi wa maji yanayo ingia mto Mkondoa, ambapo athari zake za mafuriko huathiri watu, mali na miundombinu ya Kilosa.
“Pamoja na kuwa tungependa utafiti wa kina ufanyike kuanzia kwenye
chanzo cha mto Mkondoa ili kuweza
kuelewa tabia ya mto huu, niliombe
Baraza la Taifa la Usimamizi wa maafa, litusaidie kuzielekeza hizi wizara za
kisekta, ikiwemo wizara ya maji, zikamilishe mipango ya kufufua na kujenga mabwawa ambayo yatasaidia
kuhifadhi maji na kupunguza wingi wa maji yanaoyoingia katika mto Mkondoa”
alisema Mwambambale.
Mwambambale amefafanua kuwa wilaya ya kilosa imeendelea kutekeleza
mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na mafuriko kwa kutoa mchanga kwenye mto Mkondoana
Mkundi, ili kuongeza kina cha mito hiyo. Pia zoezi la Upandaji wa miti na
matete kando ya mto Mkondoa limefanyika.
Aidha Kamati za maafa za kata na vijiji pamoja na timu za uokoaji na kutoa
misaada kwa waathirika wakati wa maafa zimejengewa uwezo.
Wilaya
ya Kilosa ni miongoni mwa wilaya 7 za mkoa wa Morogoro ambayo imekuwa
ikiathiriwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na mvua zinazonyesha mikoa ya
jirani ya Dodoma na Manyara hususani Wilaya za Mpwapwa, Kongwa na Kiteto, maji
ya mvua hizo hupita wilayani Kilosa kupitia mto Mkondoa na Mkundi.
No comments:
Post a Comment