HOTELI YA KIFAHARI YASHAMBULIWA NAIROBI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 16 January 2019

HOTELI YA KIFAHARI YASHAMBULIWA NAIROBI



Baadhi ya askari kanzu wakiwakagua baadhi ya watu wanaotoka katika eneo la tukio baada ya kuokolewa.
POLISI nchini Kenya wanaendelea na operesheni ya kukabiliana na watu wenye silaha walioshambulia majengo ya 14 Riverside katika mtaa wa Westland, Nairobi ilipo Hoteli kubwa ya kifahari ya DusitD2.

Taarifa zinasema ilisikika milipuko miwili mikubwa ya risasi na baadaye milio ya risasi mfululizo. Watu waliokuwa wamekwama ndani ya eneo hilo wanaendelea kuokolewa na polisi lakini bado wapo waliokwama.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Joseph Boinnet ameviambia vyombo vya habari kwa sasa bado ni mapema kubaini idadi ya majeruhi au waliofariki.

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab, ambalo awali lilidai kuhusika katika shambulio la Riverside, Nairobi limetoa idadi ya watua ambao linadai wameuawa. Ujumbe kwenye mtandao unaoaunga mkono kundi hilo wa Somali Memo unadai idadi ya waliofariki ni 47. Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuthibitisha hilo.

Waziri wa Usalama Dk. Fred Matiang'i ameeleza tu kwamba Wakenya wengi na watu wa mataifa ya nje wameokolewa kutoka kwenye jengo hilo, na kwamba majengo yote yamedhibitiwa.

Marekani kupitia ubalozi wake  nchini humo tayari imelaani shambulio la hoteli ya DusitD2. Balozi wa Marekani, Robert Godec ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kuwa wanashutumu vikali shambulio lililotekelezwa.

Amesema maafisa wote wa ubalozi huo wa Marekani wako salama na kwamba Marekani iko tayari kusaidia iwapo usaidizi wake utahitajika.

-BBC

No comments:

Post a Comment