SERIKALI YANUNUA RADAR NYINGINE YA TMA KUIJENGEA UWEZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 19 October 2018

SERIKALI YANUNUA RADAR NYINGINE YA TMA KUIJENGEA UWEZI

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi (kushoto) na Mwakilishi wa ECC kutoka Marekani wakisaini mkataba wa radar ya hali ya hewa itakayofungwa Mtwara, shughuli hiyo ikishuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA, Dk. Buruhani Nyenzi na wanasheria kutoka TMA na ECC.

KATIKA jitihada za kuzidi kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, Serikali ya awamu ya tano imekamilisha upatikanaji wa radar  ya hali ya hewa ya tatu  kwa kusaini mkataba utakaochukua miezi kumi na nne (14) mpaka kukamilika kwa radar hiyo. Radar hiyo itafungwa mkoani Mtwara, Mikindani katika kilima cha Mbae.

Akizungumza wakati wa kusainiana mkataba huo, mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mamlaka inazidi kujengewa uwezo wa kuendelea kuboresha huduma zake hususani katika kutoa utabiri sahihi wa hali ya hewa, hivyo upatikanaji wa radar hii ni neema kwa wananchi wa mikoa ya Kusini  mwa Tanzania. Aidha aliongezea TMA iko katika hatua za mwisho za zabuni ili kukamilisha ununuzi wa radar nyingine mbili zitakazofungwa Kigoma na Mbeya.

Kwa upande wa mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru serikali kwa jitihada zake za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuendelea kukamilisha ahadi ya kufungwa radar saba nchi nzima, hii ikiwa radar ya tatu baada ya kufungwa kwa radar  iliyopo Dar es Salaam na Mwanza.

Naye mwakilishi wa Entrerprise Electronics Corporation (ECC) kutoka Marekani bw. Edwin Kasanga alihakikishia bodi na menejiment ya TMA kuwa watamaliza kazi kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa radar ya kisasa zaidi.

IMETOLEWA NA OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

No comments:

Post a Comment