Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia)
akimsikiliza kwa makini Mbunge wa Mkuranga Abdallah Ulega kuhusu ukosefu wa
mawasiliano ya uhakika kwenye eneo hilo. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Mhandisi Peter Ulanga.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (mstari wa mbele katikati)
akikagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kata ya Mkamba Wilayani Mkuranga. Wa
kwanza kushoto mbele ni Mbunge wa Jimbo hilo Abdallah Ulega.
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye Wilaya ya Mkuranga iliyopo mkoa wa Pwani na kuahidi wananchi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaongeza mawasiliano kwenye Wilaya hiyo ambayo ina viwanda vingi vyenye uwekezaji wa aina mbali mbali.
Amesema kuwa katika
ziara yake amebaini kuwa yapo baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji kuongezewa
nguvu ili mawasiliano yaweze kufika eneo kubwa zaidi na kupeleka mawasiliano
kwenye baadhi ya maeneo ambayo yana ukosefu wa mawasiliano kwenye Wilaya hiyo
kwa kuwa mawasiliano ni maendeleo, uchumi na ulinzi na usalama.
Amefafanua kuwa,
“kimsingi mawasiliano yapo Mkuranga ila tunatakiwa kuongeza nguvu ili wananchi
wapate mawasiliano. Tunahitaji wananchi wa Tanzania wawasiliane,” amesema
Nditiye. Ameongeza kuwa minara iliyopo inaweza kuongezwa nguvu, kampuni
nyingine zitafunga mawasiliano kwenye minara ya kampuni nyingine zilizopo na
kujenga minara kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa.
Nditiye amemshukuru
Ulega na kuwapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuonyesha uhitaji wa mawasiliano
na wamegundua mawasiliano ni maendeleo yao, uchumi, ulinzi na usalama. Amesema
kuwa karibu asilimia 60 ya eneo la Mkuranga halina mawasiliano na ameyataka
makampuni ya simu yaliyojenga minara kwenye Wilaya ya Mkuranga kuongeza nguvu
ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G hadi teknolojia ya 4G.
Naye Mbunge wa Jimbo
la Mkuranga, Mhe. Abdallah Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
amesema kuwa Mkuranga haina mawasiliano ya uhakika, kuna shida kubwa sana ya
mawasiliano. “Tumefanya ziara ya kuja
kuona hali halisi ya upatikanaji wa mawasiliano kwenye Wilaya ya Mkuranga ya
upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika, baadhi ya vijiji havina mawasiliano ya
uhakika na wengine hawana mawasiliano kabisa na eneo hili lina wawekezaji wengi
wa viwanda na mawasiliano yanawawezesha wananchi kutoa taarifa za masuala ya
ulinzi na usalama”, amesema Ulega.
Ameyataja maeneo hayo kuwa vijiji vilivyopo
kwenye kata ya Mkuranga, Mpeko, Tengelea, Bupu, Kimanzichana, Kisegese, Mkamba,
Lukanga, Magawa, Msonga, Dondo, Vikindu na kata ya Mbezi.
Akijibu kiu ya
wananchi waliojitokeza wakati wa ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Peter Ulanga akiwa kwenye ziara hiyo
amesema kuwa UCSAF ilikuwa inaangalia Wilaya ya Mkuranga kwa muda na eneo lote
la Mkuranga wataliangalia ili liweze kupata mawasiliano. “Serikali inaangalia
mawasiliano kama dhana ya mkakati wa maendeleo ya wananchi kiuchumi, ndani ya
kipindi cha mwaka mmoja tutakuwa tumefikisha mawasiliano ya uhakika kwenye
vijiji vyote” amesema Ulanga.
Ameongeza kuwa Mkuranga ina kata 25 na tumeona
bado kuna matatizo ya mawasiliano ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa
2018/2019, UCSAF itapeleka mawasiliano kwenye kata 100 zilizopo kwenye maeneo
mbali mbali nchini ambapo watatoa kipaumbele kwenye kata za Mkuranga ambapo
kuna uwekezaji mkubwa.
Naye Meneja wa Kampuni
ya Simu ya Vodacom wa Wilaya ya Mkuranga, Godfrey Kamage amesema kuwa,
“tumepokea maoni ya wananchi na maelekezo ya Serikali, tutafikisha hili makao
makuu ya Vodacom ili kuongeza nguvu ya mawasiliano kutoka 2G hadi 3G na yaweze
kufika mbali zaidi,”.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment