NA LUSUNGU HELELA
NAIBU Waziri wa
Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema kutokana na kukua kwa
teknolojia ya Kisasa, Maafisa wanyamapori watakuwa na uwezo wa kuwaona faru
popote walipo wakati wakiwa wamekaa ofisini hali itakayosaidia kuwalinda
wanyamapori hao ambao wapo hatarini kutoweka .
Pia amesema Maofisa
hao watakuwa na uwezo wa kufuatilia mienendo ya wanyama hao pale walipo na
popote wanapoenda ili kujua kama wanaumwa au wanatatizo lolote hali
itakayosaidia kwenda kutoa huduma ili wanyama hao waendelee kuishi.
Mhe. Hasunga amezungumza
hayo alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mara baada ya kushuhudia zoezi la uwekaji wa vifaa vya utambuzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa
faru waliopo katika Hifadhi hiyo.
Ameongeza kuwa hatua
hiyo ni muhimu sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori hali itakayopelekea
majangili kukamatwa hata kabla hawajamuua faru.
Kwa upande wake,
Mratibu wa Mradi wa faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Phillibert Ngoti
amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa zoezi hilo la uwekaji alama za vifaa vya
kisasa unafanywa katika Hifadhi hiyo kwa kushirikina na Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Frunkfurt
Zoological Society( FZS) pamoja Friedkin Conservation Fund (FCF)
Bwana Ngoti
amefafanua kuwa zoezi la uwekaji wa vitambuzi hivyo kwenye faru
unafanyika kwa namna mbili, kuna vitambuzi vinavyowekwa ndani ya pembe za faru
na pia kuna vitambuzi vinavyowekwa kwenye mguu mmoja wa mbele wa faru ili
kusaidia kujua popote pale walipo.
Kwa upande wake,
Kiongozi wa Mradi wa Uhifadhi kutoka FZS, Rian Habuschagne amesema mradi huo
umefadhiliwa na Frunkfurt Zoological Society kwa kushirikiana na Friedkin
Conservation Society.
Bwana Habuschagne
ameeleza kuwa, wameweza kusaidia helkopta, mahema, kumlipa rubani, chakula kwa
askari wanyamapori pamoja na magari na hadi kukamilika kwa mradi huo
unaweza kugharimu zaidi ya bilioni moja.
Ameongeza kuwa
utaratibu wa uwekaji vitambuzi kwa faru umekuwa pia ukifanyika
nchini Afrika Kusini hali iliyosaidia sana katika kuwalinda faru.
Aidha, Daktari wa
Wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Alex Muse anayeshiriki katika
zoezi hilo amesema kuwa zoezi la uwekaji vitambuzi kwa faru lina changamoto
zake lakini kwa vile kuna timu nzuri kwa ajili ya kazi hiyo hivyo imekuwa
kazi nyepesi kwao.
No comments:
Post a Comment