Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas Elias
Mwangela akisalimiana na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila mapema leo
asubuhi alipowasili ofisini kwake.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas Elias
Mwangela akisaini kitabu ofisini kwake mapema leo mara baada ya kuwasili na
kupokelewa na watumishi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Songwe.
MKUU wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas Elias Mwangela amewasili katika ofisi yake mapema leo asubuhi kufuatia kuteuliwa kwake kuuongoza Mkoa wa Songwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli Julai 28, 2018.
Brigedia Jenerali Mwangela amepokelewa na kamati ya ulinzi na
usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya nne za Mkoa wa Songwe, wakurugenzi wa
halmashauri tano za Mkoa huu, wakuu wa idara pamoja na watumishi wote wa ofisi
yake.
Mara baada ya mapokezi hayo Brigedia Jenerali Mwangela amepokea
taarifa ya makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni
Mstaafu Chiku Gallawa katika kikao cha pamoja na wakuu wa wilaya, wakurugenzi,
wakuu wa idara na wajumbe wa kamati ya ulinzi na Usalama.
Gallawa amesema kuwa anayo furaha kumkaribisha Brigedia Jenerali
Mwangela na anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe
Magufuli kwa kumteua Brigedia Jenerali Mwangela, na kuwa wale waliokuwa
wakifurahia kuondoka kwake wakijua sasa wataanza kufanya kazi ndivyo sivyo
wajue wamepata kiongozi ambaye ni makini zaidi”.
Ameongeza kwa kuwataka watendaji na wanasiasa waendelee kuchapa
kazi kwa bidii wakiwa na lengo la kumkomboa mwananchi wa Songwe kutoka katika
umasikini na kuongeza pato la mkoa na taifa.
Naye Brigedia Jenerali Mwangela amemshukuru Gallawa kwa kuweka
misingi mizuri ambayo imelenga kuuinua Mkoa wa Songwe kiuchumi na kuahidi kuwa
atahakikisha mazuri yote atayaendeleza hasa pale alipoishia.
Ameongeza kwa kuwasihi watendaji kufanya kazi kwa kufuata
sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma na kwa kushirikiana kwa kuwa
anaamini katika ushirikiano kazi zinafanyika kwa ufanisi.
"Tufanye kazi tuwatumikie wananchi wa Songwe, milango ya
ofisi yangu itakuwa wazi kwenu kwakuwa napenda kufanya kazi kwa ushirikiano,
nami pia ninaomba ushirikiano wenu kama mliokuwa mnapa Gallawa ikiwezekana hata
Zaidi,” amesema Brigedia Jenerali Mwongela.
Amewataka watumishi kuzingatia muda katika kila jambo
wanalotekeleza wasiopoteze muda huku akiwasisitiza kufanya kazi kama timu moja.
“Nawapa mfano wa silaha ya mzinga ambao ili iweze kufanya kazi
vizuri wanahitajika watu sita ambao kila mmoja ana jukumu lake la kufanya ili
mzinga huo ufanye kazi kwa ufanisi, hii ni timu na akikosekana mmoja mzinga
hautaweza kufanya kazi sawasawa, nasisi tuige ushirikiano kama huu kila mmoja
atekeleze jukumu lake ili tufikie lengo moja,” amefafanua Brigedia Jenerali
Mwangela

No comments:
Post a Comment