Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa kwanza) na Mkuu wa Mkoa
wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka, wakitoka kukagua kingo za daraja la mto
Halali lililopo katika barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 wilaya ya
Wanging'ombe, mkoani humo.
SERIKALI imesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 kwa kiwango cha lami kumepunguza ajali zilizokuwa zikitokea na kutarahisisha shughuli za kibiashara na usafirishaji wa mazao katika kanda ya nyanda za juu kusini.
Amezungumza
hayo mkoani Njombe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack
Kamwelwe, wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa na
mkandarasi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group.
Waziri
Kamwelwe amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo pamoja na
madaraja yake ambao kwa sasa umefikia asilimia 97.
"Nimeridhika
na ujenzi wa barabara hii kwa kuwa hapo awali ilikuwa inaelezwa kuwa na ajali
nyingi lakini sasa zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upana wa barabara
hii kufikia mita tatu na nusu kila upande na mabega ya mita moja na nusu"
amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara nyingi
hapa nchini kwa ubora na viwango vya juu ikiwa na lengo la kurahisisha
usafirishaji, kuleta maendeleo kwa wananchi na kupunguza ajali.
"Hakuna
Serikali inayopenda kupoteza wananchi wake katika ajali za barabarani hivyo
ujenzi wa barabara utaenda sambamba na usalama wa wananchi wetu kwa kuwekewa
alama, taa na michoro barabarani", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.
Kuhusu
mzani wa makambako, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa mwarobaini wa foleni katika
eneo hilo umepatiwa tiba kwa kuwa sasa magari yanapimwa pande zote mbili ili kuondoa
msongamano.
Aidha,
amewataka wananchi kutoharibu miundombinu ya barabara ikiwemo alama za
barabarani, taa pamoja na vyuma vinavyowekwa chini ya madaraja kwani vitu hivyo
vina umuhimu wake na huongeza umakini kwa madereva wawapo barabarani.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka, pamoja na
kuishukuru Serikali kwa ujenzi wa miradi ya barabara za wilayani amemuomba
Waziri Kamwelwe kujenga kipande cha barabara kwa kiwango cha lami kinachoelekea
katika eneo la mgodi wa madini ya chuma tarafa ya Mndindi wilayani Ludewa.
Amemuelezea
pia umuhimu wa kujenga barabara ya Kibena-Lupembe ambayo bado haijaanza
kujengwa na inatengewa fedha kila mwaka kwani ndio eneo lenye uzalishaji mkubwa
wa mazao na barabara hiyo inaunganisha mkoa wa Njombe na mkoa wa Morogoro.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusuph Mazana,
amesema kuwa mpaka sasa kazi zilizobaki katika barabara hiyo ni uwekaji wa
alama za barabarani, michoro ya barabarani, kingo na taa za barabarani na kazi
ya mifereji ya maji.
Mhandisi
Mazana amemueleza Waziri Kamwelwe kuwa katika eneo la Makambako barabara mpya
imehamia upande wa kulia mita 2.5 na kuathiri baadhi ya maeneo ya wananchi
wapatao kaya 22 na hivyo tathimini ya mali zilizoathirika zinaendelea
kuandaliwa kwa ajili ya malipo ya fidia.
Ujenzi
wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 ni sehemu ya mradi wa
barabara ya Mafinga-Igawa KM 138.7 ambao umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia
mkopo wa Benki ya Dunia chini ya mradi wa Southern Africa Trade and Transport
Facilitation Project (SATTFP) na utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni
103.

No comments:
Post a Comment