Zaytun Swai Ataka Kujua Mkakati wa Serikali Kuvutia Wawekezaji wa Biashara ya Kaboni katika Mkoa wa Arusha.
Serikali imetoa wito kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kuendelea kuchangamkia fursa za uwekezaji katika biashara ya kaboni ili kuinua uchumi na kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kuitunza.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Zaytun Swai aliyetaka kujua kuna mkakati gani kuvutia wawekezaji wa biashara ya kaboni katika Mkoa wa Arusha.
Akijibu swali hilo Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali itaendelea kutafuta masoko ambapo tayari wawekezaji wamejitokeza kuwekeza katika halmashauri za wilaya za Karatu na Monduli mkoani Arusha, kampuni zilizojitokeza kuwekeza mkoani humo ni pamoja na The Nature Conservancy (TNC), Albrin (Sandrose), Soils for the Future Tanzania (SftTZ) na Carbon.
Aidha, Mhe. Khamis amesisitiza na kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali itaendelea kusimamia sheria, kanuni miongozo na taratibu, katika uendeshaji wa biashara hii ili wananchi wavutiwe na wanufaike na uwepo wa biashara hiyo.
Akiendelea kujibu swali hilo, amesema, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuvutia wawekezaji wa biashara hiyo katika Mkoa wa Arusha.
Mhe. Khamis alitaja mikakati hiyo kuwa, kuanzishwa kisheria Kwa NCMC sanjari na Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni (2022), ambazo zimefanyiwa marekebisho mwaka 2023.
Halikadhalika, Kutoa elimu kwa umma kuhusu biashara ya kaboni, elimu imeendelea kutolewa pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika biashara hiyo.
Kwa upande mwngine, Naibu Waziri Khamis amesema kutokana na uwepo wa misitu mikubwa upande wa Zanzibar, visiwa hivyo vinakwenda kunufaika na matunda ya biashara ya kaboni.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Mazingira ya Zanzibar (ZEMA), wawikilishi, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na Mawaziri, wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi wa visiwa hivyo kuhusu umuhimu wa kutunza miti ili kunuifa na biashara ya kaboni.

No comments:
Post a Comment