TANZANIA itatumia rasilimali ya madini ya kimkati kukuza uchumi wa viwanda na kutoa mchango wake kwa Dunia katika kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs).
Hayo yameelezwa na Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji alipohihitimisha ziara yake ya kikazi nchini China alikohudhuria Mkutano wa Kimataifa ulioangazia namna ya kuharakisha malengo endelevu ya Dunia 2030 (SDGs).
Mheshimiwa Prof. Mkumbo alieleza kuwa Mkutano huo ulibaini kuwepo kwa changamoto zinazoyakabili mataifa mengi duniani, Umasikini na Mabadiliko ya tabianchi yakiwa kitovu cha mjadala katika vikao mbalimbali vya mkutano huo.
“tumeona katika mijadala kwamba, ili kuondoa umasikini tunahitaji uwekezaji katika ujenzi wa Miundombinu na teknolojia ya mawasiliano” ameeleza Prof. Mkumbo.
Mheshimiwa Waziri, amefafanua kwamba Tanzania inanafasi ya kutoa mchango wake wa kutatua changamoto hizo kwa dunia hasa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"kuelekea 2030 Dunia itabadilisha nishati, sisi Tanzania tuna madini yanayotumika kutengeneza Betri za magari, hivyo tumetumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha Betri, wakifanya hivyo, tutaisaidia Dunia kutumia nishati safi, wao watakuwa wanatusaidia kupunguza umasikini, kwani hakuna nchi imeendelea bila kujenga viwanda” alisema Prof. Mkumbo.
Naye balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Balozi, Khamis Mussa Omar ameweka wazi kuwa uhusiano wa China na Tanzania umeimarika sana katika sekta mbalimbali na sasa umetimiza miaka 60 na kuingia katika hatua mpya.
“Tangu tumeanzisha uhusiano na China miaka 60 iliyopita, tumekuwa na ushirikiano muhimu katika sekta za ujenzi wa miradi inayonufaisha jamii kama, kilimo, viwanda na miundombinu” Amesema Balozi Omar.
Mkutano huo umekuwa wenye manufaa makubwa kwa Tanzania kwa kuwa umeangazia changamoto ambazo dunia inapitia katika utekelezaji wa Mipango yake inayosimawiwa na mkakati wa maendeleo endelevu 2030 (SDGs).
Kawa mujibu wa Bw. Lawrence Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, ameweka wazi kuwa, mijadala iliyoendelea katika Mkutano huo imekuwa muhimu kwa Tanzania kuelekea katika uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Mambo yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni ya kuzingatia katika mipango yetu na uandishi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, bila kufanya hivyo, tutajikuta tupo katika mtanziko kama Dunia ilivyo leo kuhusu SDGs, Dira yetu isisahu kuwekeza kwenye elimu ya watu wetu ili watumia ujuzi na maarifa kuleta maendeleo, vile vile, tumeona mijadala umesisitiza kuwa watu wenye Afya ndiyo ufunguo wa uzalishaji, uwekezaji kwenye Afya za watu wetu ni muhimu” Alifafanua Bw. Mafuru.
Mkutano huo pia umekuwa miongoni mwa vielelezo vya Uhusiano Mkubwa baina ya Tanzania na China, kwa kuwa mbali na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Kukutana na Kufanya Mazungumzo na Makamy Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la China CDICA, alikuwa miongoni mwa viongozi walioalikwa kukutana na Naibu Waziri Mkuu Mkuu wa Nchi hiyo Bw. Liu Guozhong.
No comments:
Post a Comment