Muonekano wa barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu KM 83 ambayo ujenzi wake unaendelea wilayani Rungwe mkoani Mbeya. |
Muonekano wa Kituo cha huduma ya pamoja mpakani (OSBP), cha Kasumulu katika mpaka wa Tanzania na Malawi ambacho ujenzi wake unaendelea wilayani Kyela mkoani Mbeya. |
Muonekano wa Kituo cha huduma ya pamoja mpakani (OSBP), cha Kasumulu katika mpaka wa Tanzania na Malawi ambacho ujenzi wake unaendelea wilayani Kyela mkoani Mbeya. |
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya ametoa muda wa miezi miwili kwa Mkandarasi M/S China Geo Engineering Corporation, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), na Wakala wa Majengo (TBA), mkoa wa Mbeya kuhakikisha ujenzi wa Kituo cha huduma ya pamoja mpakani (OSBP), cha Kasumulu katika mpaka wa Tanzania na Malawi kinakamilika ifikapo Septemba mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo Eng. Kasekenya ameelezea kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi huo na kumtaka Mkandarasi, Msimamizi, TANROADS na TBA kukutana haraka kutafuta ufumbuzi ili kituo hicho kikamilike kwa wakati na hadhi ya kimataifa ili wananchi na wasafirishaji wanufaike kwa huduma za kisasa.
“Fahamuni mko nyuma ya muda, hivyo ongezeni wataalam, wafanyakazi, muda wa kufanya kazi ikiwezekana iwe usiku na mchana na vifaa vinavyostahili vyote viwepo site ili nikija Septemba mnikabidhi kituo kilichokamilika na wananchi na wasafirishaji waanze kunufaika na huduma za kisasa “, amesisitiza Eng. Kasekenya.
Amesema Serikali inaendelea kumlipa mkandarasi anayejenga kituo hicho kwa wakati hivyo ni wajibu wa mkandarasi na msimamizi wa mradi kuhakikisha kasi ya malipo inaendana na kasi ya kukamilisha kazi hiyo.
Ujenzi huo unaohusisha jengo la abiria, jengo la malori, ghala, jengo la mifugo, mageti mawili, jengo la mizani na ujenzi wa barabara unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 26 utakapokamilika na kuwezesha mpaka huo kuwa na kituo cha kisasa na cha kimataifa kama ilivyo kwenye mipaka ya Rusumo mkoani Kagera, Namanga mkoani Arusha, Holili mkoani Kilimanjaro na Horohoro mkoani Tanga ambapo uwepo wa vituo hivyo unatoa huduma bora kwa wasafiri na wasafirishaji katika mipaka hiyo na hivyo kuchochea usalama, fursa za ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu KM 83 sehemu ya Mbaka-Kibanja (km 20.7), ambayo ujenzi wake unaendelea na kuwataka wananchi walio katika maeneo ya hifadhi ya barabara kupisha maeneo hayo ili mkandarasi afanyekazi kwa haraka.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wilaya za Rungwe na Kyela kwa kuwawezesha wananchi kuuza mazao yao kwa bei nzuri na kuongeza uzalishaji.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Josephine Manase wamemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa wataendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa wakandarasi ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa tija na ufanisi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI
No comments:
Post a Comment