UJUMBE WA MHE. WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI, PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB) KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI (WORLD METEOROLOGICAL DAY - WMD)”, TAREHE 23 MACHI, 2023 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 23 March 2023

UJUMBE WA MHE. WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI, PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB) KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI (WORLD METEOROLOGICAL DAY - WMD)”, TAREHE 23 MACHI, 2023


Mmoja wa wataalam wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) akitoa elimu ya hali ya hewa kwenye moja ya Shule za Msingi jijini Dar es Salaam akiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2023.

Mmoja wa wataalam wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) akitoa zawadi kwa mwanafunzi aliyejibu vizuri maswali ya elimu ya hali ya hewa kwenye moja ya Shule za Msingi jijini Dar es Salaam akiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2023.

UJUMBE WA MHE. WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI, PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB) KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI (WORLD METEOROLOGICAL DAY - WMD)”, TAREHE 23 MACHI, 2023.

Ndugu Wanahabari,

“Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania……….” 

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutufikisha sote katika Siku hii ya Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2023.

Ndugu Wanahabari na wananchi wa ujumla, Leo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaungana na Jumuiya ya Hali ya Hewa Duniani kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2023. Jumuiya ya Hali ya Hewa Duniani inatumia siku hii kuadhimisha siku ambayo mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi, 1950 ikiwa ni miaka 73 tangu kuanzishwa kwa WMO. Pamoja na kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani, tunaadhimisha miaka 150 ya Shirika la kwanza la Kimataifa la Hali ya Hewa (International Meteorological Organization-IMO) ambalo ni mtangulizi wa WMO lililoanzishwa mwaka 1873.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu 2023 ni: “Mustakabali wa Hali ya Hewa, Tabianchi na Maji kwa Vizazi Vyote” (“The Future of Weather, Climate and Water Across Generations”). 

Maadhimisho hayo yanaangazia pia mustakabali wa huduma hizi kwa vizazi vyote, upimaji na ubadilishanaji wa data na utaalamu kwa lengo la kukuza ushiriki wa wanasayansi, watoa maamuzi na vijana katika uzalishaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa na rasilimali maji. Tanzania ni miongoni mwa Nchi 193 Wanachama wa WMO na inaungana na Jumuia ya Kimataifa kuadhimisha miaka 73 ya WMO na maadhimisho ya miaka 150 ya Shirika la kwanza la Kimataifa la Hali ya Hewa (IMO).

Ndugu Wanahabari, Kama tunavyofahamu uchumi wa Tanzania unategemea sana sekta zinazotegemea na zinazoathiriwa na hali ya hewa na upatikanaji wa rasilimali maji ambazo ni muhimu katika kupanga na kufanya maamuzi. Miongoni mwa sekta hizo  kwa uchache ni kilimo, mifugo, uvuvi, nishati na maji. Pia, mfumo na mzunguko wa maji (hydrological cycle) huchangia kutengeneza mvua ambayo tunategemea katika upatikanaji wa rasilimali maji.

Kwa kuzingatia hilo, utoaji wa huduma bora za hali ya hewa na maji umekuwa kipaumbele cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika awamu zote. Huduma hizi zina umuhimu mkubwa na huongeza tija katika maendeleo ya sekta zote za kijamii na kiuchumi. Utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania ulianza kabla ya uhuru ambapo upimaji wa hali ya hewa ulianza mwishoni mwa miaka ya 1800. Mfano kituo cha kwanza cha hali ya hewa kilianzishwa mwaka 1892 katika mji wa Bagamoyo. Kuanzia mwaka 1929, huduma za hali ya hewa zilitolewa na iliyokuwa Taasisi ya Hali ya Hewa chini ya Serikali ya Kikoloni ya Uingereza katika nchi za Afrika Mashariki “The British East Africa Meteorological Services (BEAMS)”. Makao Makuu ya taasisi hiyo yalikuwa Tabora. 

Ndugu Wanahabari, Athari za mabadiliko ya hali ya hewa zimeendelea kutatiza sana uzalishaji na maendeleo katika sekta za kijamii na kiuchumi, hali inayosababisha sekta hizi kutokuwa na maendeleo endelevu na ya uhakika. Katika kukabiliana na changamoto hizo kunahitajika jitihada na hatua za makusudi na endelevu ikiwa ni pamoja na kujenga taasisi madhubuti kwa ajili ya kuboresha na kutoa huduma za hali ya hewa nchini.

Kama sehemu ya kushughulikia changamoto hizo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 ambayo ilihuisha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA). Pamoja na jukumu la utoaji wa huduma za hali ya hewa, Mamlaka iliongezewa jukumu la kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini. Lengo likiwa kuongeza uwezo wa kitaasisi ili kusaidia uboreshaji wa huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na huduma hizi kwa sekta ya maji na hatimaye kusaidia mahitaji ya jamii pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Hii ni pamoja na kuongeza kiasi cha data za hali ya hewa tunazobadilishana na nchi nyingine kupitia mifumo maalum ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Ndugu Wanahabari, Katika kuhakikisha tunakuwa na taarifa za uhakika za hali ya hewa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika huduma za hali ya hewa nchini. Miongoni mwa maeneo ya uwekezaji mkubwa ni: ununuzi wa miundombinu ya kisasa ya uchunguzi wa hali ya hewa ikiwa ni pamoja na RADA za hali ya hewa; uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa kwa ajili ya usimamizi wa data za hali ya hewa, uchakataji na uhakiki wa data, utabiri wa hali ya hewa na usambazaji wa taarifa hizi kwa wadau ikiwa ni pamoja na vijana kupitia mitandao ya kijamii. Eneo jingine ni kujenga uwezo wa rasilimali watu kwa uanzishwaji wa Shahada ya Kwanza ya Hali ya Hewa na Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo Endelevu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na upanuzi wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo Mkoani Kigoma. Uwekezaji huu umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza usahihi na ubora wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa jamii.

Ndugu Wanahabari, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushughulikia mapungufu na mahitaji yanayohusu utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa nchini kwa nia ya kuboresha huduma za tahadhari zinazoendana na kasi na kukabiliana na maendeleo ya kimataifa ya sayansi na teknolojia, pia katika kuunga mkono mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuhakikisha kuwa tahadhari za hali ya hewa zinawafikia watu wote duniani kote. Mpango huu unalenga kuhakikisha kwamba kila mtu alindwe kwa kupata taarifa za tahadhari ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka 2022.

Ndugu Wanahabari, Katika kuadhimisha miaka 73 ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na miaka 150 ya Shirika la awali la Kimataifa la Hali ya Hewa Duniani (IMO), natoa wito kwa wadau wote kutumia vyema taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa ajili ya kupanga shughuli za kijamii na kiuchumi na kufanya maamuzi pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2023 na maadhimisho ya miaka 150 ya Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (IMO). Aidha, nimalize kwa nukuu ya kauli ya Mhe: Samia Suluhu Hassani Rais wetu kuwa Kazi iendee. Kwa haya machache niliyo yazungumza.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.

No comments:

Post a Comment