Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya.
SERIKALI imesema itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam kwa kuzijenga kwa kiwango cha lami kama ilivyopangwa.
Akijibu swali Bungeni leo lililoulizwa na Mbunge wa Kigamboni Dakta, Faustine Ndugulile aliyetaka kujua ni lini Serikali itazijenga barabara za Kibada – Mwasonga – Tundwi hadi Songani na ile ya Ngomvi – Kimbiji hadi Pembamnazi kwa kiwango cha lami, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Kibada – Mwasonga – Tundwi - Songani - Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 zimetangazwa tangu Januari 6 mwaka huu na zinatarajiwa kufunguliwa Februari, 17, 2023.
Kuhusu barabara ya Chimala-Itamba-Makete yenye urefu wa KM 58 Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuijenga barabara hiyo kwa lami na hivyo kuchochea utalii katika hifadhi ya Kitulo mkoani Njombe.
Aidha, barabara ya Ngomvi – Kimbiji hadi Pembamnazi yenye urefu wa (KM 27) upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika na sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuanza ujenzi huo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kuhakikisha inakuwepo miundombinu rafiki kwa walemavu ili kuwawezesha kutumia usafiri huo kwa urahisi.
Amesema kifungu cha 6(e) cha sheria ya LATRA Sura ya 413, kimeeleza kuwa moja ya majukumu ya LATRA ni kuhakikisha uwepo wa huduma ya usafiri wa umma unaoweza kutumiwa na watu wote wakiwemo wenye vipato vya chini ,waishio vijijini, wenye mahitaji maalum ambao inajumuisha watu wenye ulemavu.
Ameitaka LATRA kushirikiana na TBS katika kuweka na kusimamia utekelezaji wa viwango vya vyombo vya usafiri wa umma ili viwe na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu wakati wote.
Mhe. Mwakibete alikuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum mkoa wa Iringa Dakta, Ritta Kabati alietaka kujua ni lini Serikali italeta sheria ya wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI
No comments:
Post a Comment