SERIKALI YAPANGA KUWATUMIA WANAFUNZI WA KOZI ZA AFYA VYUO VYA KATI NA VIKUU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 23 January 2023

SERIKALI YAPANGA KUWATUMIA WANAFUNZI WA KOZI ZA AFYA VYUO VYA KATI NA VIKUU


Na Faustine Gimu

KATIKA kuhakikisha elimu ya afya inafika shuleni kwa ufasaha, serikali imesema itaweka mkakati wa kuwatumia wanafunzi wanaosoma kozi za afya vyuo vya kati na vyuo vikuu kutoa elimu ya afya katika shule za Msingi, Sekondari na ngazi ya jamii.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya ELimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga katika Warsha ya siku mbili ya “Afya Day” Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Yohane [St. John’s] iliyoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Dkt. Haonga amesema ili kuhakikisha elimu ya Afya inafika kwa wakati shuleni ni muhimu sasa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu wanaosomea kozi za afya wakatumika kutoa elimu ya afya kama sehemu ya mafunzo ya vitendo kwao .

“Mwanafunzi wa chuo kikuu anayesoma ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada kwenye eneo la afya muda wa kufanya mazoezi ni muhimu, kinachotakiwa ni kuainisha vipaumbele  na kufanya mawasiliano na uongozi wa vyuo kwani kuna changamoto nyingi kwa vijana ikiwemo masuala ya lishe, afya uzazi, nitaelekeza wadau wa maendeleo kuongeza bajeti kuwezesha suala hili na liwe la utekelezaji Dodoma na nchi nzima kwa ujumla.“ amesema Dkt.Haonga.

Aidha, Dkt. Haonga amesema Waandishi wa Habari wana mchango mkubwa katika eneo la Elimu ya Afya kwa Umma ili kuondoa dhana ya upotoshaji kwa jamii.

 “Sisi tunawahitaji sana Waandishi wa habari kwenye eneo la Elimu ya Afya kwa Umma ili waweze kutusaidia kufafanua dhana potofu zinazoibuka kuhusu masuala ya Afya zinazoweza kusababisha wananchi wasizingatie kanuni bora za afya,” amesema Dkt. Haonga.

Afisa Mpango wa Afya shuleni, Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Magdalena Dinawi amesema  kwa taratibu za nchi kijana anaweza kupima Virusi vya UKIMWI kuanzia miaka 15 na kuendelea bila ridhaa ya wazazi wake.

Kwa upande wake mwenyekiti wa timu za uhamasishaji uchangiaji damu kanda ya kati Dkt. Leah Kitundya amesema mahitaji ya damu ni makubwa hivyo amehimiza wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia damu.

“Haijawahi tokea damu zikatosha, unapochangia leo damu zinamaliza muda wa matumizi [Expire]ndani ya siku 35, hivyo siku 35 huwa hazifiki damu zinaisha, makusanyo ni madogo mahitaji ni makubwa, kinachotakiwa damu zikusanywe zimsubiri mgonjwa elimu inahitajika sana,” amesema.

Ikumbukwe kuwa Warsha  ‘’Afya Day’’ Dodoma imefanikisha ukusanyaji wa chupa za damu 130  ambapo jumla ya wananchi 138 walijitokeza kuchangia damu na wengine walipata huduma zingine ikiwemo elimu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana, upimaji wa Kiwango cha Sukari mwilini, Shinikizo la Damu (BP) na maambukizi ya VVU ambapo imekwenda sambamba na kaulimbiu isemayo "Nachukua hatua Stahiki za Kinga dhidi ya Magonjwa, kufanya uchunguzi wa Afya wa awali mara kwa mara na kuwahi huduma za matibabu ili kuendeleza afya yangu"

No comments:

Post a Comment