GEKUL ATOA RAI HALMASHAURI KULINDA MAENEO YA MICHEZO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 4 December 2022

GEKUL ATOA RAI HALMASHAURI KULINDA MAENEO YA MICHEZO



Na Shamimu Nyaki

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul ametoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinalinda na kutunza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo

Mhe. Gekul ametoa rai hiyo  Desemba 03, 2022 wakati akizindua Ligi ya Jimbo la Segerea chini ya Mhe. Bonnah Kamoli katika viwanja vya shule ya Msingi Tabata, Dar es Salaam, ambapo amesema Sera ya Maendeleo ya Michezo nchini, inazitaka Halmashauri na wadau kushirikiana katika kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo.

"Nakupongeza Mhe. Bonnah kwa kuanzisha ligi hii ambayo kwa kiasi kikubwa itaibua vipaji na kuongeza kipato kwa vijana wetu, Serikali inasisitiza michezo ifanyike katika ngazi zote, kwakua sio tuu inaunganisha Jamii lakini michezo ni afya, upendo, Umoja na ushirikiano bila kusahau inasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza," amesisitiza Mhe.Gekul.

Ametumia nafasi hiyo, kuwahimiza wadau wengi zaidi kuanzisha ligi za michezo mbalimbali na kuwaalika Vyama vya Michezo husika ili vione vipaji vilivyopo pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mchezo husika.

Aidha, amezitaka Halmashauri zote nchini  kupitia Wenyeviti wa Michezo ngazi ya Mkoa na Halmashauri ambao ni Makatibu Tawala, kutenga fedha katika Kila Bajeti kwa ajili ya michezo na zitumike katika michezo, ambapo pia amezitaka kulinda na kutunza maeneo ya michezo.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Segerea Mhe. Bonnah Kamoli, amesema lengo la kuanzisha ligi hiyo ni kuhakikisha vijana wanaonesha uwezo wao kwakua ni sehemu ya kufanya hivyo ambapo ameahidi zawadi kwa Washindi ambao watapatikana.

"ligi hii itakua ni ya takriban siku 40 na itahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa Miguu, Netiboli, rede na mingine ambayo itakua na jumla ya Timu 61 kutoka Jimbo la Segerea," amesema Mhe.Bonnah.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abbasi Mtemvu amewataka madiwani wa Mkoa huo kuanzisha ligi katika Kata zao, ili ligi hiyo ianzie ngazi ya mtaa mpaka Jimbo ambayo itasaidia kupata wachezaji wengi Wazuri ambao watasaidika Taifa.

No comments:

Post a Comment