WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Wakala wa Barabara (TANROADS), nchini kuhakikisha wanafanya utafiti katika eneo la Shamwengo karibu na kituo cha mafuta Inyala, mkoani Mbeya ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara eneo hilo.
Waziri Mbarawa amaeyasema hayo jijini Dodoma, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombionu baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa Wakala huo na Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) zilizowasilishwa leo, Bungeni jijini humo.
“Ni kweli hapa changamoto zimekuwa kubwa katika eneo hilo na Serikali haifumbii macho ajali zinazoendelea kutokkea kwenye eneo hilo, sasa TANROADS fanyeni tafiti ili kupata majibu ya haraka ili kutatua changamoto hii”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza Wakala huo kuhakikisha wanaweka alama za barabara kwenye miundombinu hiyo ili kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara pindi inapoharibika.
Aidha, Profesa Mbarawa amesema kuwa Serikali kupitia Wakala huo bado inaendelea na ukarabati na matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini hususan yenye miinuko na kona kali lengo ni kusaidia kupunguza ajali zinazoweza kujitokeza katika maeneo hayo.
Kuhusu utekelezaji wa miundombinu hiyo nchini jumla ya miradi 17, ilipata kibali cha ujenzi kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2020/21 ambapo hadi kufikia 22 Agosti, 2022 miradi 13 yenye mikataba ya thamani ya takribani Shilingi Bilioni 641 ilikuwa imesainiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Suleiman Kakoso ameitaka Wizara kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ujenzi wa barabara katika maeneo ya kimkakati ili kuhakikisha miundombinu inasambaa nchini kote na wananchi wote kupata maendeleo kwa usawa.
“Hakikisheni mnazingatia Sera ya Ujenzi wa miundombinu kuweka kipaumbele katika kuunganisha mikoa kwa mikoa, wilaya kwa wilaya, nchi kwa nchi na maeneo yenye uzalishaji”, amefafanua Mhe. Kakoso.
Ameitaka Wizara hiyo kuhakikisha inasimamia Sheria ya Barabara katika kulinda miundombinu hiyo ambayo kwa namna moja ama nyingine inaathiriwa na shughuli za kibinadamu na hivyo kupelekea kuharibika mapema kwa miundombinu hiyo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imepokea, kujadili na kushauri taarifa ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuhusu masuala mbalimbali ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
No comments:
Post a Comment