BENKI YA NMB YAPIGA JEKI UIMARISHAJI SEKTA YA UTALII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 24 August 2022

BENKI YA NMB YAPIGA JEKI UIMARISHAJI SEKTA YA UTALII

Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay (kushoto), akikambidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Pindi Chana (wa pili kushoto), kwa ajili ya ufadhili wa mafunzo kwa wadau wa mnyororo wa thamani kwenye sekta ya utalii. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utalii Tanzania (NCT), Dk. Shogo Mlozi na wa pili kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala.

BENKI ya NMB ilikabidhi hundi yenye thamani ya 20m/- kwa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kusaidia kukuza uwezo wa sekta ya utalii hapa nchini .

Msaada huo wa benki hiyo unaunga mkono mkakati wa NCT unaolenga kuongeza ufanisi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii kwa lengo la kuboresha huduma wa sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay alisema benki hiyo imejipanga kuendelea kusaidia maendeleo ya Sekta ya Utalii na imejidhatiti katika kutoa suluhisho la huduma za kifedha kwa kuwa na mifumo bora zaidi ya ubadilishaji wa fedha na pia kuimarisha biashara ya kadi ambayo itawezesha watalii kutohangaika wanapofanya manunuzi na malipo mbalimbali.

Aidha, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Pindi Chana wakati wa hafla hiyo aliishukuru benki hiyo na kubainisha kuwa Serikali inalenga watalii Milioni tano ifikapo mwaka 2025 hivyo msaada huo umekuja wakati muafaka huku Sekta hiyo inatoa fursa nyingi katika sekta ya benki na fedha.

Lakini pia, Afisa Mtendaji Mkuu wa NCT Dk. Shogo Mlozi alibainisha kuwa mpango wa mafunzo ya kimkakati unalenga washiriki zaidi ya 5000 wakiwemo maofisa 700 wa uhamiaji na wengine walioko kwenye mnyororo wa thamani wa Sekta ya Utalii kutoka Mikoa inayojumuisha Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na Mara.


No comments:

Post a Comment