TAASISI YA IIA TANZANIA KUANDAA MKUTANO WA SHIRIKISHO LA WAKAGUZI AFRIKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 5 June 2022

TAASISI YA IIA TANZANIA KUANDAA MKUTANO WA SHIRIKISHO LA WAKAGUZI AFRIKA

Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), Bi. Zelia Njeza akizungumza na waandishi wa habari kwenye Coral Beach Hotel jijini Dar es Salaam juzi, kuelezea mafanikio ya taasisi hiyo.

Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), Bi. Zelia Njeza akifafanua jambo kwa waandishi wa habari Coral Beach Hotel jijini Dar es Salaam juzi, alipozungumza kuelezea mafanikio ya taasisi hiyo.



Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya IIA, Bw. George Binde akifafanua jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) katika mkutano huo.

TAASISI ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania nchini (IIA) imeshinda tuzo ya kuandaa mkutano mkubwa wa Shirikisho la Wakaguzi wa ndani Afrika, ambao unatarajia kuwakutanisha wakaguzi takribani 500 kwa pamoja kujadili masuala mbalimbali ya shughuli zao na changamoto zingine.

Akizungumza na vyombo vya habari juzi, Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya IIA, Bi. Zelia Njeza alisema ushindi wa kuandaa mkutano huo utakao fanyika nchini Mei, 2024 jijini Arusha waliupata nchini Zambia wiki iliyopita, ambapo IIA ilitangazwa rasmi kuandaa mkutano huo mkubwa wa wakaguzi.

"Wiki iliyopita tukiwa nchini Zambia tulitangazwa rasmi kuandaa Mkutano wa 10 wa AFIIA - 'African Federation of Institutes of Internal Auditors' tunatarajia kupata washiriki mbalimbali kutoka nje ya nchi ambapo ni zaidi ya 500.

"...Sisi kwetu haya ni mafanikio makubwa kwani tutakuwa tumeileta Afrika na Dunia kiujumla kuja Tanzania kwa pamoja na kujionea nchi yetu inafanya kitu gani kwenye masuala ya utalii japokuwa lengo kuu kuja kwao ni masuala ya ukaguzi wa ndani," alisema Bi. Njeza.

Alisema tukio hilo la kukutanisha wananchi kutoka mataifa mbalimbali litakuwa ni fursa za kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Mhe. Rais wa Tanzania, Samia Hassan Suluhu kuitangaza nchi nje ili kuvutia watalii kuitembelea Tanzania kwa shughuli za utalii.

Akizungumzia mafanikio ya IIA, aliongeza kuwa Mwezi Mei ulikuwa ni Mwezi maalum kwa Wakaguzi wa Ndani Ulimwenguni kwa ajili ya kutathmini shughuli zao pamoja na kuzungumza na wadau wa taasisi kutoa elimu kwa umma na pia kung'amua changamoto na namna ya kuzikabili.

 Aidha alisema katika kusheherekea mafanikio ya IIA, taasisi hiyo kwa kuutumia Mwezi Mei imefanikiwa kuwafikia wadau anuai wa ukaguzi wa ndani na jamii kiujumla kutoa elimu juu ya umuhimu wa shughuli zao.

Amesema kuwa Mafanikio hayo waliyoyapata ni jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tananzia kuridhia  taratibu za ukaguzi wa ndani za kimataifa zitumike nchini.

"Kwahiyo kwa kutumia taratibu za ndani tuliweza kushirikiana na Serikali kwamba taratibu za kimataifa ambazo tunaziita IPPF ziweze kutumika nchini na kuongoza ukaguzi wetu wa ndani." alisema Zelia. 

Licha ya mafanikio waliopatikana lakini pia amesema kuwa Tanzania ni Katibu na Makao Makuu ya shirikisho la wakaguzi wa ndani katika Bara la Afrika.

"Ukiangalia kwenye ramani unakuta sisi ndio Makao Makuu ya Wakaguzi wa ndani, ambapo inatoa fursa mbalimbali kwa wataalamu wetu wakaguzi wa ndani kwenye masuala mazima ya elimu na kwenye mahusiano mazuri ya Afrika na Dunia nzima." Amesema Zelia.

Amesema wameshatengeneza uwanda mpana wa mashirikiano kati ya Tanzania, Afrika na duniani kwajili ya kutatua changamoto mbalimbali ili kuleta mafanikio makubwa  kwa nchi na kwa taasisi ambazo wakaguzi wa ndani wanafanyia kazi. 


Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA), Bi. Njeza katika mkutano na vyombo vya habari Coral Beach Hotel jijini Dar es Salaam juzi.

Akizungumzia kuhusiana na uadilifu amesema taasisi hiyo ipo mstari wa mbele kusimamia misingi bora kwa kila mwanachama wa taasisi anatakiwa kuishi kwa kufuata maadili bora ambayo hutolewa na taasisi. Na pale inapotokea mwanachama anaenda tofauti na maadili kuna taratibu ambazo zinachukuliwa ikibidi kufutwa uanachama. 

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya IIA, Bw. George Binde amesema mikakati ya taasisi hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa Umma na kwa wadau mbalimbali ikiwemo kuitangaza taasisi na umuhimu wake kwa jamii. 

"Wiki tatu zilizopita wakaguzi wa ndani waliandaa mkutano wa kwanza ambao ulishirikisha viongozi na wakurugenzi wa taasisi mbalimba za umma na kuzungumza namna ya kushirikiana kuhakikisha tunakuwa na mchango mkubwa katika taasisi za umma pamoja na kuzungumza changamoto wanazozipitia. Alisema Bw. Binde.

No comments:

Post a Comment