SAO HILL YAGAWA MICHE YA MITI MILLIONI MOJA KWA LENGO LA KUTUNZA MAZINGIRA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 22 February 2022

SAO HILL YAGAWA MICHE YA MITI MILLIONI MOJA KWA LENGO LA KUTUNZA MAZINGIRA

Mhifadhi Mkuu wa shamba la Miti Sao Hill, Lucas Sabida akiongea mbele ya mkuu wa wilaya ya mufindi wakati wa zoezi la ugawaiji wa miche ya miti milioni moja.

Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Sao Hill, Lucas Sabida akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule wakigawa miche.

Baadhi ya wafanyakazi wa shamba la miti la Sao Hill wakiwa kwenye zoezi la kugawa miche ya miti kwa wananchi  na taasisi mbalimbali za serikali.

Hii ndio miche yenyewe ambayo Sao Hill wanagawakwa wananchi  na taasisi mbalimbali za serikali.


Na Fredy Mgunda, Iringa

WAKALA wa huduma za misitu Tanzania TFS kupitia shamba la miti la Sao Hill Mkoani Iringa limegawa miche milioni moja (1,000,000) kwa wananchi wa vijiji vinavyolizunguka shamba la Miti SaoHill na wadau taasisi mbalimbali za serikali mkoani Iringa na nje ya Iringa katika msimu wa mwaka wa 2021/2022 kwa lengo la kuimalisha ujirani mwema ambao umekuwa umedumu kwa miaka mingi.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa miti hiyo Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Sao HillLucas Sabida alisema kuwa zoezi la ugawaji miche ya miti kwa ajili ya ujirani mwema hufanyika kila mwaka kipindi cha masika kwa lengo la kuhakikisha wanapanda miti hiyo na inakuwa kwa wakati,hasa kipindi hiki kizuri cha mvua za msimu.


alisema kuwa hatua ya ugawaji wa miche ya miti husaidia kwa kiasi kikubwa kuwakumbusha wananchi juu ya uhifadhi wa misitu katika maeneo yao kwani wanapochukua miche hiyo huelekezwa namna na ya kuipanda na tunzaji wake.


Sabida aliwataka wananchi kuendelea kuhimizwa juu ya utunzaji wa miti wanayoipanda ili iwe na manufaa kwao na vizazi vijavyo.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021 wamezalisha na kugawa jumla ya miti milioni tano yenye thamani ya kiasi cha bilioni moja na milioni mia tano (1,500,000,000/=).

Sabida alisema kuwa mwaka huu wamegawa miche milioni moja yenye thamani ya shilingi milioni mia tatu (300,000,000/=) kwa wananchi wanaolizunguka shamba hilo pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa zoezi la ugawaji wa miche hiyo mkuu wa wilaya ya Mufindi Saad Mtambule alisema kuwa anaupongeza uongozi wa shamba la miti la Sao Hill kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kutunza miti na mazingira kwa ujumla.

Alisema kuwa uwepo wa shamba hilo katika wilaya ya Mufindi kunachangia kwa asilimia kubwa kukuza uchumi wa wananchi ambao kwa asilimia kubwa pia wanategemea uchumi wa misitu kuendesha maisha yao.

Mtambule alisema kuwa zaidi ya wananchi elfu sita wameajiriwa kwenye viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa za misitu hivyo uwepo wa shamba hilo kunachochea kukuza uchumi wa wananchi kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuacha mara moja tabia ya kuchoma moto bila kupata kibali kutoka kwa mamlaka husika na kuwahimiza kuendelea kupanda miti kwa wingi.

 Shamba la Miti SaoHill ni miongoni mwa mashamba 23 ya miti ya kupandwa ya serikali yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) lenye ukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwaajili ya upandaji miti kibiashara na hifadhi ya mazingira na vyanzo vya maji,makazi ya watumishi na uwekezaji.


No comments:

Post a Comment