· -Jumla
ya watoa huduma za Posta 119 wasajiliwa
Na Mwandishi
Wetu, Dodoma
MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania imetoa jumla ya leseni 119 kwa watoa huduma za Posta
nchini na kuwapongeza kwa kutoa huduma kwa kuzingatia masharti ya leseni zao.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt.
Jabiri Bakari wakati akiwasilisha salamu za TCRA katika uzinduzi rasmi wa Duka
la Posta mtandaoni (Posta Online Shop), uliofanyika jijini Dodoma.
Dkt.
Jabiri amebainisha kuwa TCRA wakati wote iko tayari kushirikiana na wadau wa
sekta ya posta ili kuhakikisha huduma za posta zinakuwa za kisasa zinazokidhi
mahitaji na matakwa ya wananchi katika zama za ukuaji wa Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano.
Alisisitiza
kuwa matumizi ya teknolojia hasa ya Habari na Mawasiliano ni fursa ya kukuza
biashara.
“Ni wajibu wetu kama wadau wa sekta ya Posta kuhakikisha
kwamba tunashirikiana katika mambo muhimu ambayo yanaendelea; tumependekeza
kuwa na wakati wa kushirikiana na wateja wetu katika sekta ya Posta kwa warsha
ya nusu siku” alisisitiza Dkt. Jabiri.
Alibainisha
kuwa, watoa huduma za posta waliosajiliwa wamekuwa wakitoa huduma ndani ya
nchi, Afrika Mashariki, Kimataifa na ndani ya miji katika kuhakikisha wananchi
wanapata huduma za posta na usafirishaji wa vipeto na vifurushi zenye uhakika
wakati wote.
Katika
maadhimisho hayo Shirika la Posta nchini limezindua wiki ya Posta na Duka la
Posta mtandaoni linalomwezesha mtumiaji kuagiza na kuuza bidhaa ndani na nje ya
nchi kwa utaratibu maalum uliowekwa na shirika hilo.
Akizungumzia
huduma hiyo Kaimu PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo
alibainisha kuwa, mtumiaji wa huduma za duka la posta mtandaoni sasa
hatalazimika kusumbuka kupata bidhaa anazohitaji, kwani atachagua bidhaa
aipendayo kwa njia ya mtandao na Shirika la Posta litamfikishia bidhaa hiyo
popote alipo duniani.
“Mjasiriamali
yeyote mwenye kitambulisho cha Mjasiriamali na Mfanyabiashara yeyote aliesajiliwa
anaweza kujisajili na kuweka bidhaa zake kwenye duka letu mtandaoni”
alibainisha Mbodo.
Mbodo
alibainisha kuwa duka mtandao hilo linatumia lugha zaidi ya Ishirini ikiwemo
Kiswahili hivyo kumwezesha mnunuzi, mjasiriamali na mfanyabiashara kuuza na
kununua bidhaa zake popote duniani pasina kikwazo cha lugha.
Kwa
upande wake Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA Mhandisi
Kundo Andrew Mathew alisisitiza kuwa ujio wa huduma za duka la Posta Mtandaoni
utawasaidia wakulima, wajasiriamali na wafanyabiashara kufanya shughuli zao
kisasa hatimae kuongeza tija.
“Duka
la Mtandaoni tunalozindua leo ni matokeo ya ukuaji wa teknolojia; biashara
mtandaoni ndiyo mwelekeo wa biashara duniani na inawezesha jamii kuhudumiwa kwa
urahisi; kwa sasa wananchi hawataifuata Posta bali Posta itawafuata popote
walipo” Alisisitiza Naibu Waziri Kundo.
Mpaka
sasa duka hilo la mtandaoni limesajili wafanyabiashara wapatao 300 na usajili
ungali ukiendelea.
Haya
yanajiri kuelekea kilele cha Siku ya Posta Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 9
na mwaka huu Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Posta Duniani inaungana na
mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment