WILAYA YA NYASA YAADHIMISHA SIKU YA KAHAWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 16 September 2021

WILAYA YA NYASA YAADHIMISHA SIKU YA KAHAWA

MKUU wa wilaya ya Mbinga Mh. Aziza Ally Mangosongo, akisikiliza maelekezo ya kilimo cha kahawa kutoka kwa wanakikundi cha pisi walio shiriki kulima shamba darasa katika kijiji cha kingerikiti wilayani Nyasa, kwenye maadhimisho ya siku ya kahawa yaliyofanyika  kijijini hapo, yenye lengo la kutoa Elimu ya uzalishaji Kahawa (Picha na NETHO Sichali na LILIAN NGWAVI( UoI) Nyasa DC).

HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyasa kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania, Tarehe 14.08.2021 imeadhimisha siku ya Wakulima wa kahawa maadhimisho yenye lengo la kutoa Elimu kwa wakulima wa kahawa, na kuhamasisha wakulima kulima zao hilo kitaalamu.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika shamba darasa la Kahawa la Kikundi cha Pisi, Katika Kijiji cha Kingerikiti Kata ya Kingerikiti Wilayani Nyasa, na Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa  Kanali Laban Thomas aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe Aziza Ally Mangosongo  .

Akifungua Maadhimisho ya siku ya Kahawa, Mkuu wa Wilaya ya  Nyasa amewataka wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao na kupanda mbegu aina ya Compact, ambayo ni mpya inavumilia ukame na inatoa mavuno bora na kuongeza kipato kwa wakulima,  na  Halmashauri kwa ujumla.

Ameongeza kuwa, kahawa ni zao la biashara la  kimkakati la Serikali ambalo linatakiwa uzalishaji wake uhamasishwe na wakulima wote waweze kuhamasika na kulima kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la kahawa, kuanzia upandaji hadi uvunaji wake ili uweze kuongeza tija, na uzalishaji wa kahawa bora.

Ametoa wito kwa wawekezaji, kuja kuwekeza kilimo cha kahawa katika Wilaya ya Nyasa kwa kuwa kuna eneo kubwa la uwekezaji wa kilimo cha kahawa katika Tarafa ya mpepo, ambapo kuna Hekta 2169, ambazo hazijawahi kulimwa hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuwekeza Wilayani hapa.

Awali akitoa taarifa fupi ya lengo la siku ya Kilimo cha kahawa, Kaimu Meneja wa Bodi ya Kahawa Mkoa wa Ruvuma Bw Rashid Rashid amesema Lengo la siku hiyo ni wakulima wapate elimu, jinsi ya uzalishaji bora wa zao la kahawa ambapo wakulima waliofundishwa kwa vitendo toka kuandaa shamba, kupanda, kutunza mpaka kuvuna wanatoa elimu kwa wakulima wenzao ambao hawajawahi kushiriki.

Aidha ameongeza kuwa wataalamu wa Zao la kahawa wamepata ufumbuzi wa zao la kahawa kwa kupanda mbegu mpya aina ya compact ambayo inavumilia ukame, inatoa mavuno bora,na haipatwi na magonjwa ya mara kwa mara.

Ameyataja mafanikio yaliyopatikana katika kilimo cha kahawa Wilaya ya Nyasa ni pamoja na kuongezeka kwa wakulima wa kahawa,upandaji wa mbegu bora aina ya Compact ambayo imeongeza uzalishaji  wa zao la kahawa, na hivi sasa Chama cha Msingi Kingerikiti Amcos kimeanza kukaanga na kuuza kahawa yake,hivyo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana.

Kwa upande wao wakulima wa zao hilo wamesema zao la kahawa inawasaidia kupambana na umaskin,i kwa kuwa huwapa mavuno bora na fedha ambazo zinatatua changamoto zinazowakabili na kupata nyumba bora na kusomesha watoto wao.

Wilaya ya Nyasa ni mzalishaji mkubwa wa zao la kahawa na zao hili huchangia kwa asilimi 80 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hivyo huhamasisha wananchi wa Tarafa ya Mpepo kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya upandaji ulimaji,uchakataji, na  mpaka kufikisha zao hilo sokoni na kwa sasa wakulima wamehamasika na kuongeza kilimo cha zao la kahawa.


No comments:

Post a Comment