HESLB NA TASAF KUWAWEZESHA WANAFUNZI WA KAYA MASKINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 15 September 2021

HESLB NA TASAF KUWAWEZESHA WANAFUNZI WA KAYA MASKINI

Hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya Bodi ya Mikopo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii.

Hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya Bodi ya Mikopo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo ameitaka Bodi ya Mikopo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kuendeleza mashirikiano yaliyopo ili kuhakikisha watanzania wahitaji wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu wanawezeshwa.

Akizungumza katika Hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Sebastian Inoshi, wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya taasisi hizo leo Jijini Dodoma, Dkt. Akwilapo alisema upo umuhimu mkubwa kwa taasisi za Serikali kushirikiana katika kuwafikia wananchi na kutoa huduma.

Dkt. Akwilapo aliongeza kuwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania wahitaji wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu wanapata mikopo ya elimu ya juu na kutimiza ndoto zao, hivyo upo umuhimu mkubwa wa TASAF na Bodi ya Mikopo kuhakikisha makubaliano haya yanatekelezwa kama inavyotarajiwa.

“Katika hili naomba niwape takwimu, mwaka 2019/2020, Serikali ilitoa TZS 450 Bilioni zilizowanufaisha jumla ya wanafunzi 132,392, Bajeti hii imeongezeka hadi kufikia TZS 570 Bilioni mwaka huu wa fedha wa 2021/2022 ambazo zitawanufaisha jumla ya wanafunzi 160,000” alisema Dkt. Akwilapo.

Aidha Dkt. Akwilapo aliitaka Bodi ya Mikopo na TASAF ziongeze kasi ya kuunganishwa kwa mifumo ya TEHAMA ili kuwezesha utambuzi wa haraka na uhakika wa wanafunzi wanaotoka katika kaya masikini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaopata udahili katika taasisi za elimu ya juu nchini na ambao wapo katika mpango wa TASAF wanapata mikopo ya elimu ya juu na kutimiza ndoto zao.

 “Makubaliano haya yatasaidia kuongeza ufanisi katika kubadilishana taarifa, hivyo na HESLB imejipanga kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu, Wanafunzi wahitaji wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa kuomba mkopo kwa usahihi” alisema Badru.

Naye Mkurugenz Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Ladislaus Mwamanga alisema taasisi hiyo itahakikisha inasimamia kwa umakini mkubwa malengo ya mashirikiano hayo ili kuhakikisha wanafunzi wahitaji wanaotoka katika kaya maskini wanapata mikopo YA elimu ya juu kutoka HESLB.

Mashirikiano haya yanaiwezesha HESLB kama taasisi ya mikopo ya wanafunzi kupanga mikopo kwa wanafunzi wahitaji kutoka katika Mpango wetu, tumejipanga kuhakikisha kuwa mifumo yetu kuwatambua kwa haraka wanafunzi wote ambao wanakidhi vigezo vya HESLB katika kupangiwa mikopo ya elimu ya juu” alisema Mwamanga.  

No comments:

Post a Comment