RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA AFARIKI DUNIA, TAIFA KUOMBOLEZA SIKU SABA... - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 24 July 2020

RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA AFARIKI DUNIA, TAIFA KUOMBOLEZA SIKU SABA...

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamini William Mkapa.
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamini William Mkapa amefariki duni. Mkapa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akipata matibabu jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Chamwino, Dodoma inaeleza rais huyo na Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi, CCM amefariki dunia hospitalini jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

"Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamini William Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa niwaombe Watanzania tulipokee hilitumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea mzee wetu Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa, ambaye ametangulia mbele za haki..." alieleza katika taarifa yake Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Hata hivyo, tayari Rais Dk. Magufuli ametangaza siku saba za taifa kuomboleza msiba huo mzito kwa taifa. Rais amesema siku za maombelezo zinaanza leo Julai 24, 2020 na bendera itapepea nusu mlingoti. Amewataka Watanzania kuwa watulivu na wastahimilivu na wamoja katika kipindi hiki kigumu cha msiba mkubwa wa kiongozi huyo.

Marehemu, Benjamin Mkapa alizaliwa Novemba 12, 1938 Mjini Ndanda mkoani Mtwara. Alipata elimu yake ya Sekondari, Pugu Secondari kabla ya kupata masomo ya chuo katika vyuo vya; Chuo Kikuu cha Kenyatta, Chuo Kikuu cha Makerere, Chuo Kikuu cha Columbia na Chuo Kikuu cha Makerere.

Miongoni mwa nafasi alizoshikilia zamani ni pamoja na kuwa afisa wa utawala huko Dodoma na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Yeye pia aliongoza ujumbe wa Tanzania huko Marekani na alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje kutoka 1977 hadi 1980 na kutoka 1984 hadi 1990.

Benjamini Mkapa (wa kwanza kushoto) akiwa na marais wastaafu na Rais John Pombe Magufuli (wa pili kushoto) wakati akizinduwa kitabu chake.
Mwaka 1995, Mkapa alichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, huku msingi wake ukiwa kampeni maarufu ya kupambana na ufisadi na kuungwa mkono kwa nguvu na rais wa zamani na Baba wa Taifa, Julius Nyerere. Juhudi za Mkapa za kupambana na ufisadi ni pamoja na kuumba jukwaa la wazi lililoitwa Tume ya Rais juu ya Ufisadi (Tume ya Warioba) na kuongeza msaada kwa Afisi ya Kuzuia Ufisadi.

Akiwa madarakani, Mkapa alibinafsisha kampuni zilizomilikiwa na serikali akaweka sera za soko huria. Wapo waliomuunga mkono kuwa alifanya hivyo kuvutia uwekezaji wa kigeni ungesaidia kukuza uchumi. Sera zake zilipata msaada wa Benki ya Dunia na IMF na kupelekea baadhi ya madeni ya nje ya Tanzania kufutiliwa mbali.

Marehemu, Benjamin Mkapa ambaye ameacha mke na watoto wawili, ataendelea kukumbukwa zaidi kwa kitabu chake; My Life, My Purpose alichokitoa mwishoni mwa mwaka 2019 kuelezea maisha yake.

No comments:

Post a Comment