TMA YAWATOA HOFU WANANCHI JUU YA MWONEKANO WA RANGI ANGANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 17 April 2020

TMA YAWATOA HOFU WANANCHI JUU YA MWONEKANO WA RANGI ANGANI


Muonekano wa anga ulivyokuwa.

KUHUSU MWONEKANO WA ANGA KUWA NA RANGI NYEKUNDU AU CHUNGWA KATIKA BAADHI YA MAENEO NCHINI.

KUMEKUWA na hali ya taharuki na maswali kutoka kwa umma terehe 16 Aprili, 2020 jioni kuhusu mwonekano wa anga kuwa na rangi nyekundu au chungwa katika baadhi ya maeneo nchini. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa ufafanuzi kuhusu hali hiyo ya anga kama ifuatavyo;

Mwonekano huo wa rangi ya anga ni hali ya kawaida ambayo hutokea wakati jua linapozama au kuchomoza katika mazingira yenye kuwa na hali ya hewa kama vile mawingu, matone madogo madogo ya maji na barafu katika anga mara mvua inapokatika na jua linapokuwa katika upande tofauti na eneo mvua inaponyesha.

Hali ambayo husababisha kutawanywa kwa miale ya mwanga wa jua. Hivyo kutokana na ukubwa wa matone ya maji katika wingu na chembechembe za vumbi katika anga, sehemu ya miale ya jua inayotawanywa zaidi katika mazingira hayo ni mawimbi ya miale ya jua inayohusiana na rangi nyekundu au chungwa hivyo kufanya anga kuonekana katika rangi hizo (Mawimbi madogo sana huwakilisha rangi ya blue na makubwa rangi nyekundu au rangi ya chungwa).

Hali hii haina tofauti sana na namna Upinde Mvua unavyojitokeza angani, isipokuwa upinde mvua unakuwa na rangi zote saba za spectrum ya mwanga. Mabadiliko hayo ya hali ya anga hayana madhara yeyote. Katika hali iliyozoeleka mara nyingi, anga huonekana kuwa rangi ya bluu kutokana na kutawanywa kwa mawimbi ya miale ya jua kunakofanywa na gesi ya Nitrojeni na Oksijeni ambazo ndizo hufanya sehemu kubwa ya gesi katika hewa.

Hali hiyo inatokana na molekuli za gesi hizo kuwa ni ndogo sana hivyo hutawanya sehemu ya mawimbi madogo zaidi ya miale ya jua iliyo katika rangi ya blue katika spectrum ya mwanga. Rangi hiyo huonekana katika macho ya binadamu kwa kipindi hicho.

Imetolewa na; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

No comments:

Post a Comment