SERIKALI YAJENGA KITUO CHA KISASA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 9 April 2020

SERIKALI YAJENGA KITUO CHA KISASA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya kukabiliana na COVID-19 baada ya kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani leo tarehe 8 Aprili, 2020.

Meneja wa mradi wa ujezi wa Hospitali ya kisasa ya magonjwa ya mlipuko, Kanali Solomoni Chausi akitoa taarifa mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya kukabiliana na COVID-19 walipofanya ziara ya kutembelea mradi huo.

Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula wakitembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, ambapo jengo moja lenye vitanda 40 litatumika kuwahudumia wagonjwa watakaobainika kuwa na virusi vya Corona.

SERIKALI inajenga kituo cha kisasa cha magonjwa ya mlipuko kitakacho gharimu shilingi bilioni 7 huku kikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja. Kituo hicho kinajengwa eneo la Kisoka, kilometa moja kutoka Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.

Meneja Mradi wa Ujenzi wa kituo hicho, akizungumza katika ziara ya Kamati ya kitaifa ya Makatibu Wakuu 14 ya kukabiliana na virusi vya Corona nchini ilipotembelea Hosteli za Magufuli na baadhi ya hospitali, Kanali Solomoni Shausi amesema inajengwa na Suma JKT na baadhi ya majengo yanatarajia kukamilika Aprili 30, mwaka huu.

Kamati hiyo ya kitaifa ya Makatibu Wakuu 14 ya kukabiliana na virusi vya Corona nchini imetembelea Hosteli za Magufuli ambako wasafiri kutoka nchi za nje wamepelekwa karantini kwa siku 14, huku wasafiri 72  wakiruhusiwa kurejea nyumbani baada ya vipimo kuonyesha hawana maambukizi ya Covid-19.

Wasafiri 226 kutoka nchi mbalimbali za nje walipelekwa karantini katika hosteli hizo na kwamba wasafiri wasafiri 72 wameruhusiwa kurejea nyumbani  na hivyo wamebaki wasafiri 154.

Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume wakati akitoa taarifa kwa Kamati hiyo ya kukabiliana na virusi vya Corona ambayo imetembelea Hosteli za Magufuli, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na kituo cha Kisoka ambacho kipo kilometa moja kutoka Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.

Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu wa Makatibu wakuu, Dkt. Zainab Chaula ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema Kamati hiyo imetembelea maeneo hayo ili kupata taarifa za Maendeleona mafanikio ya huduma za afya za kukabiliana na maambukizi ya  Covid-19 ambazo zinatolewa na wataalamu wa afya.

Dkt. Chaula amesema katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, jengo la kulaza wagonjwa wa Covid-19  limekamilika na kwamba wataalamu wako tayari kupokea wagonjwa wakati wowote kuanzia sasa.

“Kituo Hiki au jengo hili ambalo lina vitanda 40, hivi sasa hakijapokea wagonjwa lakini wakipatikana tutawaleta hapa kwa ajili ya kuwahudumia. Pia nawashukuru Makatibu wakuu wenzangu kwa kushiriki kutembelea  vituo hivi ambavyo vimeandaliwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya Covid-19,” amesema Dkt. Chaula.

No comments:

Post a Comment