Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akisoma Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/2020, Bungeni jijini Dodoma, Juni 13.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZOYA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI
KWA MWAKA 2019/20
13 Juni, 2019 Dodoma
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP
I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZO
YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI KWA
MWAKA 2019/20
I. UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na
kukubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka
2019/20. Hii ni bajeti ya nne ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 137 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na
kifungu cha 26 cha Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015.
2.
Mheshimiwa Spika, hotuba hii inaambatana na vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha
Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya
Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali;
Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya
Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha
wa mwaka 2019 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2019
ambavyo ni sehemu ya bajeti hii.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumuinulia Mungu moyo wangu wote kwa shukrani,
kwa kuwa amenijalia mema mengi katika maisha yangu na katika utumishi wangu kwa
Taifa. Ninamshukuru kwa kuendelea kuijalia nchi yetu amani na umoja na
kutupatia safu ya juu ya uongozi wa Taifa hili unaomtanguliza Mungu katika
kuwatumikia Watanzania wote na kujielekeza kutatua kero za wanyonge.
4.
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo kwa Mwenyezi Mungu, naomba nimpongeze kwa
dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa CCM Taifa,
kwa uongozi wake shupavu na wa mfano katika bara la Afrika hususan katika
kufanya maamuzi magumu yenye maslahi mapana kwa Taifa. Katika kipindi cha
uongozi wake: amesimamia kwa ujasiri uvunaji adili wa rasilimali za Taifa;
ameongoza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi bila kigugumizi; amedhibiti
biashara haramu ya madawa ya kulevya; ameimarisha nidhamu na uwajibikaji katika
utumishi wa umma; na ameendelea kusikiliza na kushughulikia malalamiko na kero
za makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo wajasiriamali wadogo (wamachinga
na mama/baba lishe), wafanyabiashara wadogo wa madini, wakulima na wafugaji, na
wafanyabiashara wa kati na wakubwa kutoka katika wilaya zote nchini. Vile vile,
ameendelea kudumisha amani na usalama katika nchi. Aidha, amethubutu kutekeleza
miradi mikubwa ya kielelezo ili kujenga Tanzania mpya. Nitaeleza hapo baadaye
mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mabadiliko chanya
ya kiuchumi na kijamii nchini. Kwa sasa itoshe tu niseme kuwa yalihitajika
maamuzi magumu kutoka kwa kiongozi jasiri kuelekeza utekelezaji wa mageuzi
makubwa na miradi ya kielelezo ambayo yameleta maendeleo makubwa na ya kuvutia
katika miaka hii mitatu na nusu tu! Watanzania tunayo kila sababu ya kujivunia
kumpata kiongozi shupavu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenye
uthubutu na uzalendo wa hali ya juu.
5.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na pongezi hizo,
ninapenda kumshukuru kipekee Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini katika
dhamana hii kubwa ya Waziri wa Fedha na Mipango na hivyo kuniwezesha kuandaa na
kusoma hotuba ya bajeti kuu ya Serikali hivi sasa kwa mara ya nne mfululizo.
Kwa unyenyekevu, ninasema asante sana Mheshimiwa Rais kwa heshima hii kubwa uliyonipatia
mimi na wananchi wenzangu wa wilaya ya Buhigwe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
Ninayasema haya nikitambua kwamba wapo Watanzania wengi wenye sifa za kuwa
Waziri wa Fedha na Mipango. Mimi ni nani basi hata nikateuliwa na kukabidhiwa
majukumu haya makubwa? Kama alivyonijibu yeye mwenyewe siku aliponiteua, kazi
hii nimepewa kwa neema tu kutoka kwa Mungu. Hivyo, napenda niwaahidi tena
Watanzania kuwa nitaendelea kuifanya kazi hii ya Mungu kwa uadilifu.
6.
Mheshimiwa
Spika, naamini Watanzania
watakubaliana nami kuwa nguzo ya uongozi thabiti ni wasaidizi imara na
wanaojituma. Hivyo, kwa namna ya pekee, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mama
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa
busara na bidii katika kazi zake za kumsaidia Rais kuongoza Taifa letu.
Nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza
Zanzibar kwa hekima, hali ambayo imewaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo
yanayoonekana katika kipindi cha uongozi wake. Kadhalika, napenda kumpongeza
kwa dhati Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na mbunge wa jimbo la Ruangwa, kwa uongozi hodari ndani ya Serikali na
hapa Bungeni pamoja na kumsaidia Rais kufuatilia kwa karibu utekelezaji
wa ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Vile vile kwa namna ya pekee sana nimpongeze Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu
Mkuu wa CCM kwa utendaji wake uliotukuka na kusimamia misingi ya Chama Cha
Mapinduzi ya kupigania usawa wa binadamu na haki za wanyonge.
7.
Mheshimiwa
Spika, niwapongeze pia wakuu
wa mihimili mingine ya dola kwa usimamizi na uongozi shupavu, hususan wewe
Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa kuongoza vema mhimili wa Bunge.
Hakuna shaka hata kidogo na kila mtu sasa anajua kwamba Bunge hili ni chombo
chenye nguvu sana chini ya Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Naibu Spika Mheshimiwa
Dkt. Tulia Ackson (Mb). Aidha, ninampongeza sana Mheshimiwa Profesa Ibrahim
Hamisi Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa uongozi makini wa mhimili wa Mahakama.
8.
Mheshimiwa
Spika, nichukue fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni
Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma, kwa kutekeleza kazi
zake kwa weledi mkubwa.
9.
Mheshimiwa
Spika, napenda niwapongeze na
kuwashukuru kwa dhati wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama, makamanda na
askari wote (wanaovaa na wasiovaa sare za majeshi) kwa utumishi wao makini na
uzalendo wa hali ya juu. Kipekee naomba niwatambue Mkuu wa Majeshi, Jenerali
Venance Salvatory Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Nyakoro Sirro;
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Faustine Martin Kasike; Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt.
Modestus Francis Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman Msuya; Kamishna Jenerali wa
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Rogers William Siang’a; na
Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye. Hakika,
Watanzania tunatembea kifua mbele na kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii
na kiuchumi bila wasiwasi kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko
macho na imara kuliko chuma! Tunawaomba muendelee kutimiza wajibu wenu wa
kulinda mipaka na amani ya nchi yetu kwa wivu na moyo wa kizalendo na hivyo
kuzidi kuimarisha mazingira ya kuwasha moto wa maendeleo na ustawi wa Taifa
letu na wananchi wake.
10.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee
ninamshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Profesa Adelardus Lubango
Kilangi kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 na
Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2019. Napenda pia nitumie fursa hii kumpongeza
kwa dhati mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mheshimiwa George
Boniface Simbachawene, Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, na Makamu wake Mheshimiwa
Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kwa umakini wao
katika kuongoza shughuli za Kamati hii muhimu sana. Chini ya uongozi wao,
Kamati ya Bajeti imetupatia maoni mengi na ushauri wa kujenga ambao umeisadia
sana Serikali katika kuboresha mapendekezo ya bajeti hii.
11.
Mheshimiwa
Spika, kwa kipindi chote
ambacho nimekuwa kwenye nafasi hii, napenda nishuhudie kwa Bunge hili na Taifa
kwa ujumla kwamba, Kamati hii ya Bajeti imetoa mchango mkubwa sana katika
kuboresha sera za uchumi na bajeti kuliko Watanzania wengi wanavyofahamu.
Kusema kweli wanastahili kutambulika kipekee. Kama kuna nishani au tuzo ya
Spika kwa Kamati ya Bunge inayojitanabaisha kwa utumishi uliotukuka, basi kama
itakupendeza Mheshimiwa Spika, napendekeza iwe Kamati ya kwanza kutunukiwa
heshima hiyo. Aidha, ninawapongeza Wenyeviti, Makamu wenyeviti na wajumbe wa Kamati
zote za Kudumu za Bunge kwa michango yao waliyoitoa kupitia vikao vya kamati za
kisekta katika kuboresha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali
na Serikali kwa ujumla kwa mwaka 2019/20. Maboresho hayo yalilenga kuwapatia
Watanzania maendeleo hususan uboreshaji wa huduma za kijamii na miundombinu.
12.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ya mwaka
2019/20 imeandaliwa kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano
ya kuwainua wananchi wanyonge kiuchumi na kuboresha mazingira ya kufanya
biashara na kuwekeza hapa nchini. Dhima kuu kama ilivyokubaliwa na nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bado itaendelea kuwa “kujenga
uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”.
Bajeti hii inaendelea kufungamanisha juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda na
uendelezaji wa sekta ya kilimo inayoajiri wananchi wengi na hasa waishio
vijijini huku msisitizo ukiwa katika kuhamasisha tija na uzalishaji, kujenga
miundombinu ya kiuchumi, kutafuta masoko, kupunguza kero kwa wakulima,
wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wawekezaji na kuimarisha huduma za jamii.
13.
Mheshimiwa
Spika, leo asubuhi
niliwasilisha Hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20 ambapo nilieleza kwa kina
mwenendo wa viashiria mbalimbali vya uchumi katika mwaka 2018. Aidha, katika
hotuba hiyo, nilifafanua juu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
mwaka 2018/19 na kuainisha maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2019/20. Hivyo,
katika hotuba hii, nitajielekeza kutoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya
mwaka 2018/19 na ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka
2015, kuwasilisha maboresho ya mfumo na viwango vya kodi na tozo mbalimbali,
pamoja na mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20,
ambayo yanatoa picha ya namna gani Serikali inakusudia kuendelea kukuza uchumi,
kuboresha kilimo, miundombinu, huduma na kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza
ajira na kuboresha ustawi wa Watanzania.
II.
TATHMINI
YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19
Mwenendo wa Mapato
14.
Mheshimiwa
Spika, Katika bajeti ya mwaka
2018/19, Serikali ilitarajia kupata jumla ya shilingi trilioni 32.48 kutoka
katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Mchanganuo wa mapato yaliyopatikana hadi
Aprili 2019 ikilinganishwa na lengo la kipindi hicho ni kama ifuatavyo:
i.
Mapato ya kodi yalifikia
shilingi trilioni 12.9, sawa na asilimia 87.4 ya lengo;
ii.
Mapato yasiyo ya kodi
yalifikia shilingi trilioni 2.04, sawa na asilimia 122 ya lengo. Mapato yasiyo
ya kodi yalivuka lengo kutokana na kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika
ukusanyaji wa maduhuli kwenye taasisi za Serikali kupitia Mfumo wa
Kielektroniki wa Serikali wa Ukusanyaji
wa Mapato (Government electronic Payment Gateway –GePG);
iii.
Mapato ya Halmashauri
yalifikia shilingi bilioni 529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo;
iv.
Misaada na Mikopo nafuu
kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia shilingi trilioni 1.70 sawa na
asilimia 86 ya lengo;
v.
Mikopo ya ndani
ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi
trilioni 3.3, sawa na asilimia 57.4 ya lengo; na
vi.
Mikopo ya masharti ya
kibiashara ya nje ilifikia shilingi bilioni 692.3.
15.
Mheshimiwa
Spika, kutofikiwa kwa malengo
ya mapato ya kodi kulitokana na sababu mbalimbali, zikiwemo; ugumu wa kutoza
kodi sekta isiyo rasmi; kuendelea kuwepo kwa upotevu wa mapato kunakosababishwa
na tatizo la magendo hususan kupitia bandari bubu kwenye mwambao mrefu wa Bahari
ya Hindi; na mwamko mdogo wa wananchi kudai risiti za kielektroniki wanapofanya
manunuzi au baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutotoa risiti
wanapofanya mauzo.
16.
Mheshimiwa
Spika, kutopatikana kwa mikopo
ya ndani kama ilivyotarajiwa kumetokana na kupungua kwa washiriki katika soko
la fedha la ndani hususan mifuko ya hifadhi ya jamii iliyokuwa kwenye zoezi la
kuunganishwa. Kwa upande wa mikopo ya nje ya kibiashara, upungufu uliojitokeza
ulitokana na hali ya masoko ya fedha kimataifa kubana zaidi (tighter global
financial conditions) hususan kuimarika kwa dola ya Marekani, na riba kubwa za
mikopo. Hali hii pia ilipelekea majadiliano na taasisi za fedha za Kimataifa
kuchukua muda mrefu ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata mikopo hiyo kwa gharama
zinazohimilika.
17.
Mheshimiwa
Spika, mwenendo wa upokeaji wa
misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ulikabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya Washirika wa Maendeleo kutotimiza ahadi
zao kama walivyoahidi kwenye bajeti kinyume na misingi ya makubaliano kama
ilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania
(Development Coperation Framework – DCF).
Mwenendo wa Matumizi
18.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ya mwaka 2018/19
iliyoidhinishwa na Bunge ilikuwa shilingi trilioni 32.48 ambapo shilingi
trilioni 20.47 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.01 ni matumizi ya
maendeleo. Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Aprili 2019, Serikali imetoa
jumla ya shilingi trilioni 22.19 zikijumuisha shilingi bilioni 529.25 kutoka
kwenye makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi
trilioni 16.75 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha
shilingi trilioni 6.28 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma, shilingi
trilioni 2.49 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi trilioni 7.98 kwa
ajili ya kugharamia deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
19.
Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia mwezi
Aprili 2019 Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 5.44 kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 4.89 ni fedha za
ndani na shilingi bilioni 547.38 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki
hakijumuishi baadhi ya fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa
moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi (D-Funds) ambazo hazikupita kwenye
mfumo wa malipo wa Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu za
kiuhasibu zitakapokamilika mwishoni mwa mwaka wa fedha.
20.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Mamlaka za
Serikali za Mtaa hadi kufikia Aprili 2019 jumla ya shilingi bilioni 529.25
ambazo zinatokana na makusanyo yao ya ndani zimetumika. Kati ya kiasi hicho,
shilingi bilioni 211.7 zimetumika kugharamia miradi ya maendeleo na shilingi
bilioni 317.55 zimetumika kugharamia matumizi ya kawaida.
21.
Mheshimiwa
Spika, miongoni mwa maeneo ya
kimkakati ambayo yamepatiwa fedha katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili
2019 ni pamoja na:
i.
Kulipa mishahara ya
watumishi kila mwezi kwa wakati ambapo hadi Aprili 2019 jumla ya shilingi
trilioni 6.3 zimelipwa;
ii.
Kuendelea kulipa madeni
ya Serikali kwa mujibu wa mikataba ambapo jumla ya shilingi trilioni 5.7
zilitumika, ikijumuisha shilingi trilioni 2.8 kwa ajili ya kulipa mtaji wa deni
la ndani kwa utaratibu wa “rollover”.
iii.
Kugharamia uendeshaji wa
ofisi ambapo jumla ya shilingi trilioni 2.2 zimelipwa;
iv.
Mradi wa kufua umeme
utokanao na nguvu za maji katika Mto Rufiji ambapo kiasi cha shilingi
bilioni 723.6 kimetolewa;
v.
Kugharamia elimu msingi
bila ada na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ambapo zimetolewa shilingi bilioni
616.9;
vi.
Awamu ya Tatu ya Mradi
wa Kupeleka Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jumla ya
shilingi bilioni 269.3 zimetolewa;
vii.
Ununuzi na uendeshaji wa
ndege mpya ambapo zimetolewa shilingi bilioni 238.8;na
viii.
Kuendeleza ujenzi wa
meli mpya katika maziwa makuu, zimetolewa shilingi bilioni 27.6.
Ulipaji wa Malimbikizo
ya Madai
22.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea
kuhakiki na kulipa madeni ya wazabuni, makandarasi na watumishi ambapo hadi Mei
2019 kiasi cha shilingi bilioni 598.4 kimelipwa kati ya bajeti iliyotengwa ya
shilingi bilioni 600.0 kwa mwaka 2018/19. Kati ya kiasi kilicholipwa shilingi bilioni
300.5 ni kwa ajili ya wakandarasi, shilingi bilioni 232.9 ni kwa ajili ya watoa
huduma, na shilingi bilioni 65.0 ni kwa ajili ya watumishi. Aidha, Serikali
imelipa malimbikizo ya kimshahara ya watumishi 790 waliostaafu kabla
hawajalipwa, ambapo hadi Aprili, 2019 jumla shilingi bilioni 3.10 zililipwa.
23.
Mheshimiwa
Spika, Serikali itaendelea
kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa na kuchukua hatua
mbalimbali kwa lengo la kupunguza ulimbikizaji wa madai ikiwa ni pamoja na
kuhimiza uzingatiaji wa Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015; Sheria ya
Ununuzi wa Umma SURA 410; Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na miongozo na
maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali.
24.
Mheshimiwa
Spika, napenda nisisitize kuwa
japokuwa rasilimali fedha zinazopatikana hazitoshi kugharamia mahitaji yote ya
kawaida na miradi ya maendeleo, hakuna shaka kwamba kupitia jitihada
tunazofanya hivi sasa, tunapanda mbegu leo ambazo zimeanza na zitaendelea kuzaa
matokeo mazuri ya Tanzania ya uchumi wa kati.
Mafanikio ya Serikali ya
Awamu ya Tano katika Kutekeleza Ilani ya CCM 2015
25.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Awamu ya
Tano inatekeleza kwa dhati ahadi zake kama zilivyobainishwa katika Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2016/17-2020/21 na vipaumbele vilivyobainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge la 11 mnamo tarehe 20/11/2015.
26.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa bajeti hii ni
ya nne, niruhusu tujikumbushe kwa uchache maeneo ambayo Mheshimiwa Rais
aliyawekea mkazo mkubwa mwanzoni mwa utawala wake. Maeneo hayo ni pamoja na:
kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati;
kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya Serikali; kuendeleza na
kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja, viwanja vya ndege,
reli mpya, bandari na umeme; ujenzi wa viwanda; kuongeza kasi ya kuzalisha
ajira na kupunguza umaskini; kuhakikisha kwamba madini na maliasili zetu
zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu; kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na
uvuvi; kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za maji, afya na elimu (ikiwa ni
pamoja na kuweka mkazo katika viwango vya ubora wa elimu na stadi za kazi);
mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; kuboresha mazingira ya uwekezaji;
Kuendeleza utalii; kushughulikia migogoro ya ardhi; kurejesha nidhamu katika
utumishi wa umma; na kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi.
.
27.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha
miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mafanikio
mengi yamepatikana katika maeneo niliyoyataja hapo juu, ikiashiria kwamba Ilani
ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 inatekelezwa ipasavyo.
28.
Mheshimiwa
Spika, miongoni mwa mafanikio
ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kipindi cha miaka mitatu na
nusu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na:
i.
Ujenzi wa reli ya kati
kwa kiwango cha standard gauge, ambapo hadi Aprili 2019 ujenzi wa
kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 48.9 na
kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422), ujenzi umefikia asilimia 7.12.
Mradi huu utakapokamilika utaboresha usafiri nchini na kuwezesha usafirishaji
wa mizigo (mazao, mifugo, madini, mazao ya misitu) na abiria kwenda na kutoka
nchi jirani zisizo na bahari (Uganda, Rwanda, Burundi, DRC) na kuiwezesha
Tanzania kuwa kitovu cha biashara na huduma (trade and logistics hub) katika
nchi za maziwa makuu. Aidha, mradi huu utapunguza uharibifu wa barabara
unaotokana na usafirishaji wa mizigo mizito kwa malori, utapunguza msongamano
wa shehena ya mizigo katika bandari ya Dar es Salaam na kutoa fursa za ajira;
ii.
Ufufuaji wa Shirika la
Ndege la Tanzania (ATCL) ambapo hadi Aprili 2019 jumla ya ndege sita mpya
zimenunuliwa na kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga nchini (Dar es Salaam,
Mwanza, Bukoba, Kigoma, Tabora, Dodoma, Iringa, Mbeya, Songea, Mtwara, Arusha,
Mpanda) na kimataifa (Hahaya – Comoro, Lusaka, Harare, Entebbe, Bujumbura).
Aidha, ndege nyingine mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Bombadier Q400
zinatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka 2019. Hivi karibuni, ATCL
inatarajiwa kuanza safari kwenda Mumbai (India), Johannesburg (Afrika Kusini)
na Guangzhou (China). Kuimarishwa kwa usafiri wa anga kutasaidia sana kukuza
biashara na sekta ya utalii nchini;
iii.
Ujenzi wa jengo la tatu
la abiria (Terminal III) na miundombinu yake katika kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa
mwaka umekamilika;
iv.
Ujenzi wa barabara kuu
na za mikoa kwa kiwango cha lami, ikiwemo daraja la juu la Mfugale katika
makutano ya TAZARA; ujenzi wa barabara ya juu yenye ngazi tatu (ubungo
interchange) katika makutano ya Ubungo; barabara ya njia nane kutoka Kimara Dar
es Salaam hadi Kibaha (km 19); daraja la Magufuli katika mto Kilombero; na
kuanza ujenzi wa daraja jipya la Selander jijini Dar es Salaam ikijumuisha
barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2;
v.
Ujenzi wa meli mpya za
kubeba mizigo na abiria kwenye Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa;
vi.
Kukamilika kwa upanuzi
wa gati namba moja, kuanza ujenzi wa gati namba mbili, na kuendelea na ujenzi
wa sakafu ngumu katika gati la kupakua na kupakia magari katika bandari ya Dar
es Salaam. Upanuzi huu utawezesha meli kubwa kuingia na kutoka bandarini kwa
ajili ya kushusha na kupakia mizigo;
vii.
Ujenzi wa mradi wa
kihistoria wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika Mto Rufiji wenye
uwezo wa kuzalisha MW 2,115 ambapo ujenzi wa miundombinu wezeshi imekamilika na
mkandarasi wa kutekeleza ujenzi huo ameshapatikana. Mradi huu utaiwezesha nchi
yetu kuwa na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ambao ni wa lazima katika
jitihada na dhamira yetu kama Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda. Mradi huu pia
utafungua fursa za utalii, uvuvi na kilimo cha umwagiliaji; na
viii.
Kuendelea na utekelezaji
wa Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini (REA) ambapo hadi Mei 2019, jumla
ya vijiji 7,127 vimeunganishiwa umeme.
29.
Mheshimiwa
Spika, yapo pia mafaniko
makubwa yaliyopatikana katika kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za jamii
kwa kipindi cha Awamu ya Tano ambayo ni pamoja na;
i. Kuendelea na utekelezaji wa ahadi ya kugharamia
elimu msingi (kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne) bila ada na
kuongezeka kwa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
ii. Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vyuo vikuu
ikiwemo kukamilika na kuzinduliwa kwa maktaba ya kimataifa yenye uwezo wa
kuhudumia wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
iii. Kuboreshwa kwa huduma za afya katika hospitali
za rufaa, mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini. Aidha, upatikanaji
wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na huduma za kibingwa umeimarika. Vile vile,
idadi ya wagonjwa waliokuwa wanapelekwa kutibiwa nje imepungua na hivyo kuokoa
fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya matibabu nje ya nchi; na
iv. Kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za maji safi
mijini na vijijini ambapo katika Jiji la Dar es Salaam umefikia asilimia
85, katika mikoa mingine asilimia 80, miji midogo asilimia 64 na vijijini
asilimia 64.8.
30.
Mheshimiwa
Spika, mafanikio mengine
yaliyopatikana katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ni:
i.
Kutengamaa kwa viashiria
vya uchumi jumla ikiwemo ukuaji wa Pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 6.9
katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2016 – 2018), kukua kwa sekta ya
kilimo kwa wastani wa asilimia 5.3, mfumuko wa bei wa tarakimu moja ya kiwango
cha wastani wa asilimia 4.7 katika kipindi hicho, utulivu wa thamani ya
shilingi, na kupungua kwa kiwango cha umaskini kutoka asilimia 28.2 hadi
asilimia 26.4.
ii.
Serikali kuhamia makao
makuu ya nchi, Dodoma na kuendeleza eneo la Mji wa Serikali kwa kujenga majengo
23 ya ofisi za wizara zote na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
miundombinu yake (umeme, maji, barabara).
iii.
Kudhibiti utoroshaji na
uuzaji wa madini nje ili kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake ikiwa ni
pamoja na kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kutunga Sheria
ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017, ujenzi wa
uzio kuzunguka eneo la migodi ya Tanzanite Mirerani na kuanzisha masoko ya
madini;
iv.
Kuanza utekelezaji wa
Mkakati wa Kuharakisha Maendeleo ya viwanda Nchini (Fast Tracking
Industrialization Strategy). Aidha, sekta binafsi pamoja na mifuko ya hifadhi
ya jamii zimewekeza kwenye miradi ya viwanda ambapo mifuko hiyo inaendeleza
miradi 7 kati ya miradi 25;
v.
Mifumo ya kielektroniki
ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato imeimarishwa;
vi.
Usimamizi wa fedha za
Serikali umeimarishwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina;
vii.
Kuimarishwa kwa taasisi
za umma na zile ambazo Serikali ina hisa. Serikali imeendelea kufuatilia na
kusimamia kwa karibu zaidi utendaji katika mashirika ya umma ili kuhakikisha
kuwa michango na gawio stahiki inatolewa kwa Serikali. Katika kuimarisha
mashirika ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa, Serikali imepata
mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na mashirika mengi ambayo yalikuwa hayatoi
gawio na michango stahiki kwa Serikali kuanza kufanya hivyo. Mwaka 2015/16
kulikuwa na mashirika 13 tu yaliyotoa gawio kwa Serikali kiasi cha shilingi
bilioni 119.2 na sasa yameongezeka kufikia mashirika 28 ambayo hadi Mei 2019
yalikuwa yametoa gawio la jumla ya shilingi bilioni 497.5.
viii.
Serikali imefanya
majadiliano yenye maslahi kwa Taifa na baadhi ya makampuni ikiwemo kampuni ya
“Airtel Tanzania” ambayo yameleta mafanikio yafuatayo: Umiliki wa hisa za
Serikali kuongezeka kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 bila kuzilipia,
Mwenyekiti wa Bodi na Afisa Mkuu wa Ufundi (Chief Technical Officer) kuteuliwa
na Serikali, Kampuni kuilipa Serikali shilingi bilioni moja kila mwezi kwa
kipindi cha miaka mitano ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3 kimeshalipwa kwa
kipindi cha mwezi Aprili, Mei na Juni 2019, Kupatikana kwa kiasi cha dola za
Marekani milioni moja kutoka kwa Mwenyekiti wa “Bharti Airtel” kama sehemu ya
uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility) ambazo zimeelekezwa
kujenga hospitali mpya ya kisasa Dodoma, Kufutwa kwa madeni na madai ya “Bharti
Airtel” kwa Airtel (T) kiasi cha shilingi bilioni 937 (Dola milioni 407.38), na
Serikali kupata gawio maalum kutoka mapato ghafi ya Airtel Tanzania kwa mwaka
2019; na
ix.
Mafanikio katika
mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambapo ripoti ya uwazi ya kimataifa
(Transparency International) ya mwaka 2018 imeonesha Tanzania imeshika nafasi
ya 16 kwa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ikilinganishwa na nafasi
ya 27 mwaka 2015.
31.
Mheshimiwa
Spika, kwa matokeo haya
niliyoeleza, ni wazi kabisa kuwa Taifa letu linakwenda mbele chini ya Serikali
hii ya tano ya CCM na liko katika mwelekeo sahihi (moving forward in the right
direction). Serikali ya CCM chini ya Jemadari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inawashukuru
sana wananchi wote wa Tanzania waliotimiza wajibu wao wa msingi kwa kulipa kodi
ipasavyo na hivyo kuwezesha Taifa kupata mafanikio hayo makubwa sana katika
kipindi kifupi. Wananchi wamejitoa na kuonesha uzalendo wa hali ya juu kwa
kushiriki kwenye ujenzi wa Tanzania mpya. Mafanikio haya pia ni matunda mazuri
ya kutunza nidhamu katika usimamizi wa uchumi, udhibiti wa mianya ya upotevu wa
mapato na matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma. Bajeti hii ninayowasilisha
mbele ya Bunge lako Tukufu itaendelea kutekeleza malengo ya Serikali kama
yalivyoanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Mpango wa Pili
wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17-2020/21.
III.
SERA
ZA BAJETI KWA MWAKA 2019/20
Shabaha za Uchumi Jumla
32.
Mheshimiwa
Spika, Shabaha za uchumi jumla
katika kipindi cha mwaka 2019/20 ni kama ifuatavyo:-
i.
Pato la Taifa kukua kwa
asilimia 7.1 mwaka 2019 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.0 mwaka 2018;
ii.
Mfumuko wa bei kuendelea
kubaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3.0 hadi 4.5 katika
kipindi cha muda wa kati;
iii.
Mapato ya ndani kufikia
asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 14.3
mwaka 2018/19;
iv.
Mapato ya kodi kufikia
asilimia 13.1 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.1
mwaka 2018/19;
v.
Matumizi ya Serikali
kufikia asilimia 22.7 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya
asilimia 21.6 mwaka 2018/19; na
vi.
Nakisi ya bajeti
inakadiriwa kufikia asilimia 2.3 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka
matarajio ya asilimia 2.0 mwaka 2018/19.
Sera na Mikakati ya
Kuongeza Mapato
33.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2019/20,
Serikali imekusudia kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa
lengo la kuiwezesha kugharamia shughuli za Serikali ikiwemo miradi mikubwa ya
miundombinu na huduma za jamii. Katika kufanikisha azma hii, Serikali
itatekeleza sera zifuatazo:
i.
Kuboresha mazingira ya
kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogo na za kati ili
kupanua wigo wa kodi na mapato mengine ya Serikali;
ii.
Kurekebisha viwango vya
kodi kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya
ushindani kutoka nje;
iii.
Kuboresha mazingira ya
ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya TEHAMA katika
usimamizi wa kodi;
iv.
Kuimarisha usimamizi wa
sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa
mapato, pamoja na kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu kwa mlipakodi;
v.
Kuimarisha makusanyo
yasiyo ya kodi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA;
vi.
Kuendelea kuwianisha na
kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na wakala, taasisi na Mamlaka za
Serikali za Mitaa; na
vii.
Kuiongezea Mamlaka ya
Mapato ya Tanzania uwezo hususan watumishi, vitendea kazi bora na mafunzo ili
kutambua na kudhibiti mbinu za ukwepaji kodi.
34.
Mheshimiwa
Spika, ili kufikia malengo ya
makadirio ya mapato ya ndani, Serikali imeandaa mikakati mahsusi ya kiutawala
itakayotekelezwa katika kipindi cha muda wa kati. Mikakati hiyo inajumuisha:
i.
Kuongeza ufanisi katika
usimamizi na ukusanyaji wa kodi za ndani kwa kutekeleza Mfumo Jumuishi wa
Usimamizi wa Mapato ya Ndani (Integrated Domestic Revenue Admistrative
System-IDRAS);
ii.
Kupanua wigo wa kodi
kupitia utambuzi na usajili wa walipakodi wapya pamoja na kuendelea na zoezi la
urasimishaji wa sekta isiyo rasmi;
iii.
Kuwekeza kwenye maeneo
ambayo Serikali inaweza kupata mapato zaidi hususan katika uvuvi wa bahari kuu
kwa kujenga bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli za uvuvi;
iv.
Kuimarisha uwezo wa
ufuatiliaji na udhibiti wa uhamishaji wa faida unaofanywa na kampuni za
kimataifa;
v.
Kuimarisha usimamizi wa
misamaha ya kodi kwa kuhakikisha inaelekezwa kwenye miradi inayokusudiwa;
vi.
Kuhakikisha kuwa
maduhuli yote yanapitia katika Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji
wa Mapato (GePG) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato; na
vii.
Kuimarisha mifumo ya
ufuatiliaji katika taasisi za Serikali ili kuhakikisha kuwa michango stahiki ya
taasisi za umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali inawasilishwa kwa wakati.
35.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa misaada
na mikopo nafuu kutoka nje, Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano na
ushirikiano na Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali itaendeleza mazungumzo
na Washirika wa Maendeleo ili kila upande uzingatie misingi na kanuni za
ushirikiano wa maendeleo pamoja na kuendeleza majadiliano ya kimkakati
(Strategic Dialogue) na kumaliza tofauti za kisera au kimtazamo pindi
inapojitokeza, pasipo kuathiri utoaji wa fedha za utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali.
36.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu mikopo ya
kibiashara ya ndani na nje, Serikali itaimarisha uhamasishaji wa wadau katika
soko la ndani kwa lengo la kuimarisha ushiriki wao katika minada ya dhamana za
Serikali. Aidha, jitihada zinafanyika ili kuvutia wawekezaji mbalimbali kutoka
nje ya nchi wenye nia ya kuikopesha Serikali ili kuwezesha utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa uchumi wa Taifa letu.
Sera za Matumizi
37.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2019/20,
Serikali itaendelea kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na
kufanya ufuatiliaji na tathmini ya matumizi hususan katika miradi ya maendeleo.
Lengo kuu ni kuwa na matumizi bora ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
na kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya fedha. Aidha, Serikali itaendelea
kuhakiki, kulipa na kuzuia kuongezeka kwa malimbikizo ya madai kwa Serikali.
Pia, Serikali itaendelea kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yenye
kuchochea ukuaji wa uchumi.
Maeneo ya vipaumbele kwa
mwaka 2019/20
38.
Mheshimiwa
Spika, katika Hotuba
niliyoiwasilisha asubuhi kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 na
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20, niliainisha vipaumbele kwa mwaka
2019/20 ambavyo vitatekelezwa kwa kuzingatia umuhimu wa pekee wa kulinda
mazingira nchini (environmental sustainability). Bajeti hii inalenga kutekeleza
vipaumbele hivyo kama ifuatavyo:
i.
Viwanda
na kilimo: Katika kuendeleza azma
ya kujenga uchumi wa viwanda, katika mwaka 2019/20 Serikali itajikita kuvutia
uwekezaji zaidi kwenye viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini
kama vile mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuzalisha bidhaa
kwa ajili ya soko la ndani na ziada kwa ajili ya kuuza nje, pamoja na kuongeza
fursa za ajira. Vile vile kama wote tunavyofahamu, sekta ya kilimo (mazao,
uvuvi, mifugo na misitu) ni muhimu sana kwa uendelezaji wa viwanda Tanzania kwa
kuwa sehemu kubwa ya malighafi za viwanda zinatokana na kilimo. Katika
kuimarisha sekta hii, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) hususan kuhakikisha upatikanaji wa
mbegu bora, pembejeo, huduma za ugani, masoko, miundombinu wezeshi na tafiti,
ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha zaidi kwenye maeneo wezeshi kwa kilimo na
kutoa nafuu za kikodi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha bodi za mazao,
kuboresha na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya mazao ili
kuviwezesha kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kuwekeza
kwenye shughuli mbalimbali za kilimo na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo
vya kuongeza thamani ya mazao.
ii.
Ukuaji
wa uchumi na maendeleo ya watu: Licha ya kutilia mkazo kuongeza ukuaji wa sekta kuu za uchumi
zinazotegemewa na kuajiri Watanzania wengi, bajeti ya 2019/20 itaelekezwa
kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu na ujuzi, chakula na lishe
bora na huduma za maji safi na salama. Aidha, kupitia bajeti hii, msukumo
utawekwa katika kuongeza ubora wa nguvukazi ili iendane na mahitaji ya soko la
ajira.
iii.
Uboreshaji
wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji: Bajeti hii imeweka msisitizo mkubwa katika
kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan reli, bandari, nishati,
barabara, madaraja, na viwanja vya ndege. Aidha, Serikali itaendelea kupitia na
kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi, sambamba na
kuimarisha ulinzi na usalama ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na
nje. Napenda niwahakikishie wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia mwaka
ujao wa fedha, Serikali itaanza kutekeleza kwa nguvu zaidi mpangokazi wa
kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint for the Regulatory Reforms to
improve the Business Environment) ili mazingira ya biashara nchini yawe
rafiki zaidi na yenye gharama nafuu.
iv.
Ufuatiliaji
na tathmini Bajeti hii pia
inakusudia kuimarisha zaidi ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo katika ngazi zote. Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi wa
ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa bajeti lakini wakati huo huo kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa kodi
unafanyika bila kuathiri biashara. Napenda kuwasisitiza tena watumishi wa TRA
kwamba hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe kodi au
malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA.
IV.
MABORESHO
YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
39.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada
zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na
usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yamezingatia dhamira ya
Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika
(stable and predictable). Vilevile yanalenga pamoja na mambo mengine, kuchochea
kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo, viwanda, kukuza ajira,
na kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa
Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka
2017/18 kwa kuanza kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na
Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta baadhi ya tozo na ada,
kupunguza na kuondoa muingiliano katika kutoza tozo hizo. Marekebisho
yanayopendekezwa yanahusu Sheria zifuatazo:-
a.
Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b.
Sheria ya Kodi ya
Mapato, SURA 332;
c.
Sheria ya Ushuru wa
Bidhaa, SURA 147;
d.
Sheria ya Usimamizi wa
Kodi, SURA 438;
e.
Sheria ya Usalama
Barabarani, SURA 168;
f.
Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
g.
Sheria ya Bajeti, SURA
439;
h.
Marekebisho madogo
madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali;
i.
Kuanza utekelezaji wa
Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha
Ada na Tozo mbalimbali;na
j.
Hatua za Kisera na
Kiutawala katika Kuboresha ukusanyaji wa mapato.
a.
Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
40.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama
ifuatavyo:-
i.
Kusamehe Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenye makasha yenye majokofu (HS Code 8418.69.90)
yanayotumika kwenye Kilimo cha Kisasa cha mboga mboga (horticulture) kwa
wakulima watakaoingiza makasha hayo kutoka nje ya nchi kwa matumizi ya kilimo.
Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika uzalishaji na
kuhamasisha kilimo cha kisasa cha
mboga mboga nchini;
ii.
Kufanya marekebisho
kwenye Kifungu cha 68(3)(d) ili kisihusishe uuzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje
ya nchi. Lengo la hatua hii ni kuwawezesha wauzaji wa mazao ghafi ya
kilimo nje ya nchi kuendelea kufanya biashara hiyo kwa kadri ya kibali
kitakavyotolewa na Serikali;
iii.
Kusamehe Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenye vifaa vya kukaushia nafaka (Grain Drying Equipment
HS Code 8419.31.00). Msamaha huu unatarajiwa kutoa unafuu kwenye gharama za
kukausha nafaka kwa ajili ya kuzihifadhi. Aidha hatua hii itachochea ukuaji wa
kilimo cha mazao ya nafaka;
iv.
Kupunguza kiwango cha
Kodi ya Ongezeko la Thamani kutoka asilimia kumi na nane (18) hadi asilimia
sifuri (0) kwenye huduma ya umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania
Zanzibar ili kuwapunguzia gharama za maisha wananchi wa Tanzania Zanzibar.
Serikali iliridhia na kuelekeza kuwa umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda
Tanzania Visiwani utozwe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia
sifuri;
v.
Kutoa msamaha wa Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwa vilainishi vya ndege vinavyoingizwa nchini na
waendeshaji wa ndani, Shirika la ndege la Taifa, au mashirika ya ndege
yanayotambulika katika Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga (Bilateral Air
Services Agreements) kwa Kufanya marekebisho ya Sehemu ya Pili ya Jedwali la
Misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani katika kipengele cha 11.
Hatua hii itawezesha nchi yetu kusaini Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga
ambayo ilishindikana kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha
huo;
vi.
Kusamehe Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenye tiketi za ndege, vipeperushi, kalenda, shajara,
karatasi zenye nembo na sare za wafanyakazi zilizowekwa nembo ya Shirika husika
la ndege, kwa kufanya marekebisho ya Sehemu ya Pili ya Jedwali la Misamaha la
Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kuongeza kipengele kipya kinachotoa
msamaha pale vinapoingizwa nchini na mashirika ya ndege yanayotambulika katika
Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga. Hatua hii itawezesha nchi yetu kusaini
Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo ilishindikana kusainiwa hapo
awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo; na
vii.
Kufuta msamaha wa Kodi
ya Ongezeko la Thamani uliokuwa unatolewa kwenye taulo za Kike (HS Code
9619.00.10) kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei
nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha wafanyabiashara. Aidha, wakati
Serikali ilipoweka msamaha huu ilitarajia kwamba wazalishaji wa taulo za kike
wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi.
Hatua zote za Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,646.7
b. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
41.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
i.
Kupunguza kiwango cha
Kodi ya Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax) kwenye Sheria ya Kodi
ya Mapato kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili (2)
kuanzia mwaka 2019/20 hadi mwaka 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya
kuzalisha taulo za kike. Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano
(Performance Agreement) na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila
upande. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa
hiyo muhimu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali. Vile vile hatua hii
itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo kutoka
nje na kuhamasisha uzalishaji wake ndani ya nchi;
ii.
Kusamehe Kodi ya Zuio
inayotozwa kwenye gharama zinazoambatana na mikopo (mfano ada za bima, gharama
ya usimamizi, na uandaaji wa mkopo, na ada nyingine zinazoendana na gharama za
mkopo) kwa mikopo inayotolewa na Benki, Taasisi za Fedha za nje na wahisani
mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali. Lengo la hatua hii
ni kuiwezesha Serikali kupata mikopo kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi.
Aidha, msamaha huu utaiwezesha Serikali kutekeleza miradi yake kwa wakati;
iii.
Kutoa msamaha wa
kutengeneza hesabu ambazo zinatakiwa kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
kwa ajili ya ukokotoaji wa Kodi ya Mapato kutoka kiwango cha sasa cha shilingi
milioni ishirini (20,000,000/=) hadi shilingi milioni mia moja (100,000,000/=).
Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa mlipa kodi ya kutafuta mtaalam
(Certified Public Acountant) kwa ajili ya kutengeneza hesabu. Aidha, hatua hii
inalenga pia kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza mapato ya Serikali; na
iv.
Kusamehe kodi kwenye
mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne (4,000,000/=) kwa wenye
vitambulisho vya wajasiriamali na kupunguza kiwango cha chini cha kodi kutoka
shilingi laki moja na nusu (150,000/=) kwa mwaka hadi shilingi laki moja
(100,000/=) kwa mwaka kama ilivyofafanuliwa kwenye Jedwali Na. 1 na Na. 2.
Lengo la hatua hii ni kupunguza mzigo wa kodi kwa walipakodi wadogo pamoja na
kuoanisha viwango vya kodi na kiwango cha chini kinachotakiwa kwa
mfanyabiashara kutumia mashine ya kodi ya kielektroniki (EFD) ambacho kwa sasa
ni shilingi milioni kumi na nne (14,000,000/=). Aidha, hatua hii inalenga pia
katika kusisitiza matumizi ya mashine za kielektroniki (Electronic Fiscal
Device- EFD) ili kuwezesha ukokotoaji wa kodi ulio sahihi na kuongeza ulipaji
kodi wa hiari.
Jedwali Na.1: Viwango vya sasa vinavyotozwa kodi kwa
Wafanyabiashara wasiotengeneza Vitabu vya Hesabu
Mauzo (Shilingi)
|
Kodi
ya kulipa kwa Mfanyabiashara asiye na Kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu
cha 35 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Kodi ya kulipa kwa
Mfanyabiashara mwenye kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha
Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Mauzo yasiyozidi
Shilingi 4,000,000
|
Hamna
|
Hamna
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 4,000,000 lakini hayazidi shilingi 7,500,000
|
Shilingi 150,000
|
Asilimia 3 ya kiasi
cha mauzo kinachozidi shilingi 4,000,000
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 7,500,000 lakini hayazidi shilingi 11,500,000
|
Shilingi 318,000
|
Shilingi 135,000
jumlisha asilimia 3.8 ya kiasi cha mauzo kinachozidi Shilingi 7,500,000
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 11,500,000 lakini hayazidi shilingi 16,000,000
|
Shilingi 546,000
|
Shilingi 285,000
jumlisha asilimia 4.5 ya kiasi cha mauzo kinachozidi Shilingi
11,500,000
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 16,000,000 lakini hayazidi shilingi 20,000,000
|
Shilingi 862,500
|
Shilingi 487,000
jumlisha asilimia 5.3 ya kiasi cha mauzo kinachozidi shilingi 16,000,000
|
Jedwali Na. 2: Viwango Vipya vinavyopendekezwa kutozwa kodi kwa Wafanyabiashara
wasiotengeneza Vitabu vya Hesabu
Mauzo (Shilingi)
|
Kodi ya kulipa kwa
Mfanyabiashara asiye na Kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha
Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Kodi ya kulipa kwa
Mfanyabiashara mwenye kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha
Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Mauzo yasiyozidi
Shilingi 4,000,000
|
Hamna
|
Hamna
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 4,000,000 lakini hayazidi shilingi 7,000,000
|
Shilingi
100,000
|
Asilimia 3 kiasi cha
mauzo kinachozidi shilingi 4,000,000.
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 7,000,000 lakini hayazidi shilingi 11,000,000
|
Shilingi
250,000
|
Shilingi 90,000
jumlisha asilimia 3 kiasi cha mauzo kinachozidi Shilingi 7,000,000.
|
Mauzo yanayozidi
shilingi 11,000,000 lakini hayazidi shilingi 14,000,000
|
Shilingi 450,000
|
Shilingi 230,000
jumlisha asilimia 3 ya kiasi cha mauzo kinachozidi Shilingi
11,000,000
|
Mauzo
yanayozidi shilingi 14,000,000 lakini hayazidi shilingi 100,000,000
|
Shilingi 450,000
jumlisha asilimia 3.5 ya kiasi cha mauzo kinachozidi shilingi 14,000,000
|
Hatua hizi za Kodi ya
Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 35,192.5
c.
Sheria
ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
42.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Sheria ya
Ushuru wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru
wa Bidhaa (specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza
kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya
uchumi jumla. Kwa msingi huo wa sheria, napendekeza kutokufanya mabadiliko
ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli.
Aidha, hatua hii inazingatia kiwango kidogo cha mfumuko wa bei nchini na azma
ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda, na hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye
Sekta ya Viwanda, kuvilinda na hatimaye kukuza ajira na mchango wa sekta hiyo
kwenye Pato la Taifa. Hata hivyo, napendekeza kurekebisha Sheria ya Ushuru wa
Bidhaa kwa bidhaa chache tu kama ifuatavyo:-
i.
Kupunguza Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa
kutokana na usindikaji wa matunda (kama ndizi, mabibo, rozela/choya, nyanya,
nk) yanayozalishwa hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi
asilimia 75 kutoka shilingi 200 kwa lita hadi shilingi 61 kwa
lita ikiwa ni punguzo la shilingi 139 kwa lita. Lengo la hatua hii ni
kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari na pia kuvutia uwekezaji kwenye viwanda
vidogo vidogo vya aina hii. Aidha, bei ya mvinyo huu kwa lita inafanana na bei
ya vinywaji baridi;
ii.
Kutoza Ushuru wa Bidhaa
wa asilimia 10 kwenye nywele za bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na
asilimia 25 kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi
zinazotambuliwa kwa HS Code 67.03; 67.04 na 05.01. Lengo la hatua hii ni
kuongeza mapato ya Serikali;
iii.
Kusamehe Ushuru wa
Bidhaa kwenye vilainishi vya ndege (lubricants) vinavyoingizwa nchini na
Shirika la ndege la Taifa au mashirika ya ndege yanayotambulika katika mikataba
ya Kimataifa ya huduma za anga. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha nchi yetu
kusaini mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo ilishindikana kusainiwa
hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo; na
iv.
Kutoza Ushuru wa Bidhaa
wa asilimia 10 kwenye bidhaa za mabomba na vifaa vya plastiki
vinavyotumika kwenye ujenzi wa miradi ya ujenzi wa miundo mbinu ya maji kwa
kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo na
kutosheleza mahitaji hapa nchini. Hatua hii inahusisha bidhaa za mabomba na
plastiki zinazotambuliwa katika HS Code 39.17. Lengo la kuanzisha Ushuru wa
Bidhaa kwenye bidhaa hizo ni kulinda viwanda na kuongeza fursa za kazi, ajira
na mapato ya Serikali.
Hatua za Ushuru wa
Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,955.50.
d. Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438
43.
Mheshimiwa
Spika; napendekeza kuongeza
muda wa ziada wa miezi sita (6) hadi Disemba 2019 kwa walipa Kodi waliokubaliwa
kulipa kodi wanazodaiwa kwa utaratibu maalum wa kusamehe malimbikizo ya nyuma
ya riba na adhabu (Tax Amnesty on Interest and Penalties) kwa asilimia 100 kwa
kufanya marekebisho ya Kifungu cha 70 (2) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya
mwaka 2015 . Hatua hii inapendekezwa kutokana na muitikio mzuri wa walipakodi
wakati msamaha huo ulipotolewa mwezi Julai 2018 ambapo dhamira ya Serikali
ilikuwa ni kutoa ahueni kwa walipakodi waliokuwa na malimbikizo makubwa
yanayoathiri biashara zao.
Hatua hiyo ya
marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi inatarajiwa kuongeza mapato
ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 367,000.
e.
Sheria
ya Usalama Barabarani, SURA 168
44.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kama ifuatavyo:-
i.
Kuongeza muda wa Leseni
za udereva kutoka miaka mitatu (3) ya sasa hadi miaka mitano (5);
ii.
Kuongeza tozo ya Leseni
ya udereva kutoka shilingi elfu arobaini (40,000) kwenda shilingi elfu sabini
(70,000); na
iii.
Kuongeza ada ya kadi ya
usajili wa magari kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi elfu
hamsini (50,000/=); pikipiki za matairi matatu kutoka shilingi elfu kumi
(10,000/=) hadi shilingi elfu thelathini (30,000/=) na pikipiki kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi
shilingi elfu ishirini (20,000/=).
Lengo la mapendekezo
haya ni kupunguza gharama za kuchapisha leseni kwa kipindi cha miaka mitatu
kwani leseni hizo zinaweza kudumu zaidi ya miaka mitano. Aidha, marekebisho
haya pia yanalenga katika kuoanisha gharama za uchapishaji wa leseni na kipindi
cha leseni husika.
Hatua hizi kwa pamoja
zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 18,147.0
f.
Sheria
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004
45.
Mheshimiwa
Spika, kikao cha Mawaziri wa
Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget
consultations of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 3 Mei, 2019 mjini
Arusha, kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa Pamoja wa
Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.
Mapendekezo hayo yanalenga katika kuendeleza viwanda, kukuza ajira na kuboresha
maisha ya wananchi katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
46.
Mheshimiwa
Spika, Mapendekezo ya Mawaziri
wa Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha
yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika
mwaka 2018/19.
i.
Mapendekezo ya hatua
mpya za viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo:-
a.
Kupunguza Ushuru wa
Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwenye malighafi ya
kutengeneza taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotengenezwa hapa nchini kwa
mwaka mmoja. Aidha, Watakaonufaika na punguzo hili ni viwanda vinavyozalisha
bidhaa hiyo hapa Tanzania na utaratibu utakaotumika katika kuagiza malighafi
hizo ni ule wa kuwapa unafuu wa Ushuru wa Forodha “Duty Remission”.
Aidha, Serikali itaendelea kutoza ushuru wa Forodha wa asilimia 25 kwa taulo za
watoto (Baby Diapers) za kutoka nje ya nchi. Hatua hii inatarajiwa kutoa unafuu
wa gharama za uzalishaji, ajira na mapato ya Serikali. Aidha ni matarajio ya
Serikali kuwa viwanda vinavyonufaika na msamaha huu wa Ushuru wa Forodha
vitazalisha bidhaa hizi muhimu kwa afya ya watoto na kuziuza kwa bei nafuu ili
watanzania wengi waweze kuzinunua. Malighafi zitakazohusika katika msamaha huu
ni zile zinazotumbulika katika HS Code 3506.91.00; PE Film HS Code 3926.90.90;
Super Aborbent Polymer HS Code 3906.90.00; Wet Strength Paper HS Code
4803.00.00; Non Wovens HS Code 5603.11.00; Polyethylene Laminated Non Wovens HS
Code 5903.90.00; Spandex HS Code 5402.44.00; na Dust Free Paper Hs Code
4803.00.00;
b. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha
asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifaa
vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito.
Hatua hii itawanufaisha wanaofanya shughuli hizo na utaratibu wa “Duty
Remission” ndio utatumika katika kuagiza vifaa hivyo. Lengo la hatua hii ni
kutoa unafuu wa gharama na kuhamasisha ukataji na usafishaji wa madini hayo
hapa nchini na hivyo kuongeza thamani yake kabla ya kuuzwa. Aidha, hatua hii
itaongeza mapato ya Serikali na ajira. Vifaa vitakavyohusika ni vile
vinavyotambulika katika HS Codes 3606.90.00; 6804.10.00; 6813.20.00;
7018.90.00; 7020.00.99; 8202.20.00; 8202.99.00; 8203.20.00; 8205.10.00;
8423.89.90; 8513.10.90; na 9002.19.00;
c. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye makaratasi (HS Code 4805.11.00 na
4805.19.00) yanayotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya mboga
mboga kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Utaratibu wa “Duty Remission”
utatumika ambapo viwanda vinavyotengeneza vifungashio hivyo tu ndivyo
vitakavyonufaika. Lengo la kuondoa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi hizo ni
kupunguza gharama ya utengenezaji wa vifungashio ili kulinda viwanda vya ndani
dhidi ya ushindani wa nje, kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa
vifungashio vya aina hii na hatimaye kuhamasisha uuzaji nje wa mboga mboga kwa
ajili ya kupata fedha za kigeni;
d. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya mbegu
vinavyotumiwa na wazalishaji wa mbegu hapa nchini. vifungashio vitakavyohusika
ni vile vinavyotambulika katika HS codes 3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00;
7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00; 6304.91.90; 7607.19.90. Lengo la hatua hii
ni kuongeza ubora wa mbegu na pia kuzipa unafuu wa gharama Taasisi
zinazozalisha mbegu hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission”
utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;
e. Kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwa utaratibu wa “Duty Remmission”
kwenye malighafi (Alluminium Alloys) zenye HS Code 7606.92.00 zinazotumika
katika kutengeneza sufuria (Alluminium pots). Hatua hii inalenga katika
kupunguza gharama za uzalishaji, kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu
hapa nchini, kulinda viwanda vya ndani ili viweze kuongeza uzalishaji wa
kutosheleza mahitaji na kuongeza ajira;
f. Ili kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa kahawa
hapa nchini pamoja na kuongeza mapato ya Serikali napendekeza kuongeza Ushuru
wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka
mmoja kwenye kahawa inayoagizwa nje ya nchi (HS Code 09.01);
g. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10
au dola za kimarekani 125 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton)
kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala
ya asilimia 10 pekee. Bidhaa hizo ni “Flat -rolled products of iron
or Non-alloy steel na Flat –rolled products of other alloy steel.” Bidhaa
hizi hutambulika katika HS Codes 7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00;
7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00; 7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00;
7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la kuweka viwango hivyo vya Ushuru wa Forodha ni
kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo na kulinda viwanda
vya hapa nchini na ajira;
h. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au
dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye
bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala ya
asilimia 25 pekee. Ushuru huo unahusu bidhaa zinazotambulika katika HS
Code 7212.30.00; 7212.40.00 na 7212.50,00. Hatua hii ina lengo la kulinda
viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo
zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda
ajira na mapato ya Serikali;
i. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au
dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa
mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za mabati
zinazotambulika katika HS Code 7212.60.00 badala ya kutoza ushuru wa asilimia 10
pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu
wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and
under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;
j. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton)
kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa
badala ya ushuru wa asilimia 25 pekee. Hatua hii inahusu bidhaa
zinazotambulika katika HS codes 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00;
7210.70.00 na 7210.90.00. Lengo la hatua hiyo ni kuwalinda wazalishaji wa
bidhaa hizo hapa nchini kutokana na ushindani wa nje;
k. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
au dola za kimarekani 250 badala ya kiwango cha asilimia 25 au
dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye
bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye nondo
kwa mwaka mmoja. (Reinforment bars and hallow profile). Hatua hii inahusu
bidhaa zinazotambulika katika Hs codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7213.99.00;
7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00; 7214.90.00; 7214.99.00; 7215.10.00;
7215.50.00; 7215.90.00; 7225.90.00; 7225.92.00; 7225.99.00; 7306.30.00;
7306.50.00; 7306.61.00; 7306.69.00; na 7306.90.00. Lengo la hatua hii ni
kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini na kuongeza ajira;
l. Kwa kuwa mbogamboga zinalimwa kwa wingi hapa
nchini, napendekeza kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi
asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mboga mboga (horticultural
products) zinazotambulika kwenye HS codes 0603.11.00; 0603.12.00; 0603.13.00;
0603.14.00; 0603.19.00; 0604.20.00; 0604.90.00; 0701.90.00; 0702.00.00;
0703.10.00; 0703.20.00; 0706.10.00; 0710.10.00; 0710.21.00; 0710.22.00;
0710.30.00; 0714.10.00; 0714.20.00; 0804.30.00; 0804.40.00; 0804.50.00;
0805.10.00; 0805.40.00; 0805.50.00; 0806.10.00; 0807.11.00; 0807.20.00;
0808.10.00; 0808.20.00. Aidha, hatua hii itaongeza mapato ya serikali; na
m. Kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha
asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za
fito za plastiki zijulikanazo kama PVC Profiles HS Code 3916.10.00;
3916.20.00; 3916.90.00 ambazo hutumika kwa ajili ya kutengenezea fremu za
milango, madirisha n.k. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali.
ii.
Mapendekezo ya kuendelea
na utekelezaji wa viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2018/19 ni kama
ifuatavyo;-
a.
Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye
karatasi zinazotambulika kwenye HS codes 4804.11.00; 4804.21.00; 4804.29.00;
4804.31.00 na 4804.41.00. Karatasi hizi ni zile zinazozalishwa na kiwanda cha
Mufindi;
b. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 35
hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye ngano inayotambulika kwa HS Code
1001.99.00 na HS Code 1001.99.90. Hatua hii imezingatia kwamba uzalishaji wa
ngano katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hautoshelezi mahitaji, na
bidhaa hii ni muhimu katika kutengeneza vyakula mbalimbali. Lengo la Serikali
ni kuwezesha Viwanda na walaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa ngano waweze
kupata vyakula husika kwa bei nafuu na tulivu. Aidha utaratibu wa “Duty
Remission” utaendelea kutumika katika kuagiza ngano hiyo ambapo Viwanda
vinavyotumia ngano ya aina hii katika uzalishaji ndivyo vinavyohusika katika
kutumia kiwango hicho nafuu cha Ushuru wa Forodha. Kutokana na mahitaji makubwa
ya ngano katika Jumuia ya Afrika Mashariki na SADC, wakati umefika sasa kwa
wananchi kuchangamkia fursa ya Kulima ngano katika maeneo mbalimbali nchini
yanayofaa kwa kilimo cha ngano ikiwemo eneo la shamba la Basuto;
c. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki
zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Electronic Fiscal Device)
zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00;
d. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa
ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates” (ABL) HS Code
3920.10.90 ambayo hutumika kama malighafi ya kutengeneza dawa ya meno kwenye
viwanda vya ndani;
e. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwa utaratibu wa “Duty Remission”
kwenye bidhaa ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama RBD Palm Stearin (HS Code
1511.90.40);
f. Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa
asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti
(safety matches) vnavyotambuliwa kwenye HS code 3605.00.00 kutegemea kiwango
kipi ni kikubwa;
g. Kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa
asilimia 25 au dola za kimarekani 350 kwa kila tani moja ya
ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma za
misumari zinazotambulika katika HS code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins,
corrugated nails, staples other than those of heading 83.05);
h. Kutoza ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye soseji (sausages) na bidhaa
za aina hiyo (HS code 1601.00.00);
i. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye chingamu (chewing gum)
zinazotambulika katika HS code 1704.10.00;
j. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye peremende (HS code
1704.90.00);
k.
Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye chokoleti
(chocolates) HS code 18.06 kwa mwaka mmoja;
l. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwenye biskuti (HS code 1905) kwa mwaka mmoja;
m. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa
(tomato sauces) zinazotambulika katika HS code 2103.20.00;
n.
Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye maji
(mineral water) yanayotambulika katika HS code 2201.10.00;
o. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwenye nyama (meat and edible meat offal in
chapter 2) kwa mwaka mmoja;
p.
Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 25 kwenye mafuta Ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya,
mizeituni, nazi, karanga, mahindi n.k) kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga
katika kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya kula
hapa nchini. Nchi yetu ina fursa kubwa ya kukuza uzalishaji wa bidhaa hiyo.
Hivyo, kuna umuhimu wa kuchochea na kuhamashisha uzalishaji wa mbegu za mafuta
na uchakataji wa mafuta ghafi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa hapa nchini.
Lengo la hatua hii ni kuongeza ajira mashambani, viwandani na pia kulinda fedha
za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi. Mafuta ghafi hayo
yanatambulika kwenye HS code 1507.10.00; 1508.10.00; 1511.10.00; 1512.11.00;
1513.11.00; 1514.11.00; 1514.91.00; 1515.11.00; 1515.21.00; 1515.30.00;
q. Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula
yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho (semi-refined, refined/double refined
oil) mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, karanga, nazi, mahindi n.k.
Ongezeko la Ushuru wa Forodha linatarajiwa kuhamasisha uchakataji wa mbegu za
mafuta hapa nchini na kuongeza ajira viwandani na mashambani. Aidha ongezeko la
Ushuru wa Forodha linahusu mafuta yote ya kula yaliyochakatwa yanayoingizwa
nchini na yanayotambulika kwenye HS codes 1507.90.00; 1508.90.00; 1509.90.00;
1510.00.00; 1511.90.10; 1511.90.30; 1511.90.90; 1512.19.00; 1512.29.00;
1513.19.00; 1513.29.00; 1514.19.00; 1514.99.00; 1515.19.00; 1515.20.00;
1515.50.00; 1515.90.00;
r.
Kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye “Gypsum Powder” HS
code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja;
s.
Kupunguza ushuru wa
forodha kutoka asilimia 100 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja
kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje
ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji
hapa nchini. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha
sukari, ajira na mapato ya Serikali;
t.
Kutoza kwa mwaka mmoja
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 kwenye mitumba inayoingia kutoka nje (badala
ya asilimia 35 au dola za marekani 0.40 kwa kilo moja kutegemea
kiwango kipi kikubwa);
u.
Kusamehe Ushuru wa
Forodha kwenye malighafi, vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza
nguo na viatu vya ngozi. Aidha, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki wameridhia orodha iliyooanishwa (harmonized list) ya malighafi na
vipuri ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kuziwezesha nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki ziweze kufanya biashara kwa bidhaa za nguo na viatu vya ngozi
vitakavyozalishwa ndani ya Jumuiya; na
v.
Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki zimekubaliana kutoza Ushuru wa Mauzo nje (Export Levy) wa
asilimia 10 kwenye ngozi iliyosindikwa kwa kiwango cha kati (wet blue).
Lengo la hatua hii ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi, kuongeza thamani, na
kuongeza ajira katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
47.
Mheshimiwa
Spika, Mawaziri wa Fedha wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye
Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management
Act, 2004) kama ifuatavyo:-
i.
Kufanya marekebisho
katika kipengele cha 1 (a) Sehemu B ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CMA, 2004) ili kuingiza vilainishi kwa ajili
matengenezo ya ndege (Lubricants for Aircraft), sare (uniforms), kalenda, shajara
na peni kwenye orodha inayopata msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye huduma za
ndege. Lengo la kutoa msamaha huo ni kuiwezesha nchi yetu kusaini mikataba ya
Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo haikuweza kusainiwa hapo awali kutokana na
kutokuwepo kwa msamaha huo.
Hatua hizi za Ushuru wa
Forodha kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi
cha shilingi milioni 31,074.0
g. Sheria ya Bajeti, SURA 339
48.
Mheshimiwa
Spika, ili kuwezesha
utekelezaji wa Miradi Mikubwa yenye manufaa kwa Taifa kama vile Ujenzi wa
Miundombinu, Ununuzi wa Ndege, Mabehewa au Vichwa vya Treni, Miradi ya Umeme
n.k, inapendekezwa kurekebisha Kanuni ya 23 ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za
mwaka 2015, ili kumpa Mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuongeza muda wa
matumizi ya fedha za mwaka wa fedha uliomalizika hususan zinazohusu Miradi ya
Maendeleo. Hivi sasa Kanuni hii imeweka ukomo wa miezi mitatu (3) wa kutumia
fedha za mwaka wa fedha uliomalizika, ambapo baada ya muda huu wa miezi mitatu
(3) kuisha, fedha hizo hupaswa kurejeshwa Mfuko Mkuu wa Serikali.
Utaratibu huu wa sasa wa kurejesha fedha za miradi, Mfuko Mkuu wa
Serikali baada ya kumalizika kwa muda wa miezi mitatu (3) unaathiri utekelezaji
wa Miradi ya Maendeleo kutokana na kutokuwepo kwa fedha za kulipia Hati za Madai
hadi hapo mgao mpya wa fedha utakapotolewa kwenye bajeti ya mwaka mpya wa
fedha.
h. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya
Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali.
49.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya
marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za
kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha
utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya
Fedha ya mwaka 2019 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
i.
Kuanza
utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa biashara (Blueprint)
kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali.
50.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia matokeo ya
mkutano wa Mh. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na wafanyabiashara kutoka
wilaya zote nchini uliofanyika ikulu, Dar es salaam, tarehe 7 Juni, 2019,
Serikali inapendekeza kufuta au kupunguza ada na tozo hamsini na nne (54)
zinazotozwa na Wizara, Idara na taasisi zinazojitegemea ili Kuondoa kero na
urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Hatua hizi ni sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo
wa udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the
Business Environment). Aidha, hatua hii imelenga kuondoa muingiliano
wa majukumu ya kiutendaji baina ya Wizara, Taasisi na Mamlaka za Udhibiti.
Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2019
na Matangazo ya Serikali (Government Notices). Marekebisho hayo yatajumuisha:-
I.
Mamlaka
ya Dawa (TFDA)
a.
Kufuta tozo za
Kushikilia usajili wa dawa za chanjo (Vaccines and Biologicals) inayotozwa kwa
kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150); dawa za mitishamba (Herbal
medicines) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150); vifaa
tiba (medical devices) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia moja
(100); vitendanishi (diagnostics) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani
mia mbili hamsini (250); chakula kinachotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani
mia moja (100); vipukusi (antiseptics and diagnostics) vinavyotozwa kwa kiasi
cha shilingi laki moja (100,000/=); na tozo za bidhaa zinazotengenezwa ndani ya
nchi (retention fees for domestic products);
b.
Kufuta tozo za Kudurufu
cheti cha usajili wa vitendanishi inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani
mia moja (100);
c. Kufuta tozo za ukaguzi wa maduka mapya ya kuuzia
vyakula inayotozwa kwa kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000);
d.
Kufuta tozo za usajili
wa maduka ya reja reja ya dawa za mifugo kati ya shilingi elfu hamsini
(50,000/=) hadi shilingi laki moja (100,000/=);
e. kufuta tozo ya ukaguzi wa viwanda vya samaki
nchini iliyokuwa inatozwa kwa kiwango cha kati ya shilingi laki mbili
(200,000/=) hadi shilingi laki mbili na elfu hamsini (250,000/=);
f.
Kufuta tozo ya ukaguzi
wa maduka mapya ya samaki ya shilingi elfu hamsini (50,000/=); na
g.
Kufuta tozo ya leseni ya
mwaka ya biashara ya samaki kati ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) hadi
shilingi laki tatu (300,000/=).
Lengo la hatua hizi ni
kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa
sheria kwa hiari na kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za TFDA (customer
base).
Hatua hii inatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,500.0
II.
Shirika
la Viwango Tanzania
Napendekeza kufanya
marekebisho ya Sheria ya Shirika la Viwango Tanzania kwa:-
a.
Kufuta tozo ya shilingi
elfu hamsini (50,000/=) ya maombi ya alama ya ubora (TBS mark);
b. Kufuta tozo ya nembo ya ubora (TBS mark
guarantee) ya asilimia kumi na tano (15) ya tozo ya gharama za mwanzo za
ukaguzi wa ubora (transport costs and overhead fees);
c. Kufuta
tozo ya dhamana ya cheti cha kutumia nembo ya ubora (TBS mark licence). Tozo
hii hutozwa kwa kiwango cha asilimia hamsini (50) ya gharama za usafirishaji na
upimaji wa Sampuli kutoka sokoni na viwandani;
d. Kufuta tozo ya shilingi elfu hamsini (50,000/=)
ya ununuzi wa fomu ya maombi ya bidhaa zinazotoka nje kwa bidhaa zote;
e.
Kufuta tozo ya gharama
za ugenzi (calibration of equipment based on industrial metrology). Tozo hii
hutozwa kulingana na umbali wa sehemu (Kwa mfano Dar es salaam - chini ya umbali
wa kilometa 5 kutoka TBS ni shilling elfu kumi (10,000/=); umbali wa kati
ya kilometa 5 hadi 7 kutoka TBS ni shilingi elfu hamsini (50,000/=); na umbali
wa zaidi ya kilometa 7 kutoka TBS ni shilingi laki moja (100,000/=); na
f.
Kufuta tozo ya asilimia
0.2 ya gharama ya mzigo na usafirishaji ya udhibiti wa vipodozi, vifaa tiba
ikiwa ni pamoja na kondomu, mabomba ya sindano (syringes), glavu (gloves),
pamba (cotton wool) na bendeji (bandage).
Lengo la hatua hii ni
kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara na wazalishaji, kupunguza gharama katika
uendeshaji wa vifaa vya viwandani na kupunguza tozo za kero.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,687.4
Aidha, napendekeza
kufanya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
kwenye eneo la usimamizi wa viwango ambao unajumuisha ubora na usalama wa
chakula na vipondozi ili Shirika la Viwango Tanzania (TBS) liendelee kusimamia
eneo la chakula na vipodozi kwa ujumla kama ilivyo kuwa tangu mwaka 1975. Hivyo
basi, Shirika la Viwango litachukua jukumu la kuunganisha utaratibu wa usajili
wa majengo (premises registration), Usajili wa bidhaa (product registration),
udhibiti wa bidhaa (certification) na udhibiti wa bidhaa kutoka nje (import
inspection) kwa ujumla. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) itaendelea kusimamia
madawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi ili kuongeza ufanisi katika eneo hili.
III.
Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
Napendekeza kufanya
marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Majumbani na
Viwandani, Sura 182 kwa kufuta tozo zifuatazo:-
a.
Kufuta tozo ya huduma ya
kusitisha kibali cha awali na kutoa kibali kipya inayotozwa kwa kiwango cha
Dola za Kimarekani hamsini (50);
b.
Kufuta tozo ya huduma ya
kubadilisha taarifa za kibali inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani
hamsini (50);
c.
Kufuta tozo ya usajili
wa kampuni ya Wakala wa Forodha (Clearing Agent) inayotozwa kwa kiwango cha
Dola za Kimarekani mia tano (500) kila kipindi cha usajili;
d.
Kufuta tozo ya huduma ya
kubadilisha taarifa za usajili inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani
mia moja (100) kila kipindi cha usajili;
e.
Kufuta tozo ya huduma ya
ukaguzi wa dharura inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia tatu (300)
kwa kila ukaguzi;
f. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
(maintenance fee) kwa viwanda vya magodoro inayotozwa kwa kiwango cha
Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kila mwaka;
g.
Kufuta ada ya kulinda
cheti cha usajili kwa viwanda vya rangi inayotozwa kwa kiwango cha Dola
za Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;
h. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
kwa viwanda vya nguo inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu
moja (1,000) kwa mwaka;
i. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
kwa viwanda vya ngozi inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu
moja (1,000) kwa mwaka;
j. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
kwa viwanda vya plastiki inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani
elfu moja (1,000) kwa mwaka;
k. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
kwa viwanda vinginevyo vikubwa inayotozwa kwa kiwango cha Dola za
Kimarekani elfu moja (1,000) kwa mwaka;
l. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
kwa viwanda vidogo vidogo inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani
mia mbili hamsini (250) kwa mwaka;
m. Kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili
kwa wasambazaji wakubwa inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani
elfu moja (1,000) kwa mwaka; na
n.
Kufuta ada ya kulinda
cheti cha usajili kwa wasambazaji wa kati inayotozwa kwa kiwango cha Dola za
Kimarekani mia tano (500) kwa mwaka.
Aidha, napendekeza pia
kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na udhibiti wa Kemikali za
Majumbani na Viwandani Sura 182, ili kurekebisha viwango vya tozo kama
ifuatavyo:-
a.
Kutoza tozo ya shilingi
elfu arobaini (40,000/=) ya usajili wa kemikali kwa kila kemikali kwa kipindi
cha usajili badala ya Dola za Kimarekani ishirini (20);
b.
Kutoza tozo ya shilingi
laki mbili (200,000/=) kwa wafanyabiashara wakubwa na shilingi elfu hamsini
(50,000/=) kwa wajasiriamali wadogo kwa kila cheti cha usajili (Certificate
holder registration);
c.
Kutoza tozo ya shilingi
laki mbili (200,000/=) badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100) kwa wafanya
biashara wakubwa na shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa wafanyabiashara wadogo
kwa Usajili wa eneo la kuhifadhia kemikali (Premises registration);
d.
Kutoza tozo ya shilingi
laki tatu (300,000/=) kwa siku kwa kila mtu ya kuchambua kemikali chakavu
badala ya Dola za Kimarekani mia tatu (300);
e.
Kutoza tozo ya shilingi
laki mbili (200,000/=) ya kuainisha na kuidhinisha njia ya kuteketeza kemikali
badala ya Dola za Kimarekani mia tano (500);
f.
Kutoza tozo ya shilingi
laki tatu (300,000/=) kwa kila siku kwa kila mtu ya kusimamia kupakia,
kusafirisha, kushusha na kuteketeza kemikali chakavu badala ya Dola za
Kimarekani mia tatu (300);
g.
Kutoza tozo ya shilingi
laki tatu (300,000/=) ya ukaguzi wa maghala na sehemu za kuhifadhia kemikali
badala ya Dola za Kimarekani mia mbili (200);
h. Kutoza tozo ya shilingi laki moja na elfu
hamsini (150,000/=) kwa kila siku kwa kila mtu kwa tathmini ya njia za
Usafirishaji na ukaguzi wa dharura (Transportation Routes assessment and
emergency inspection) badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100);
i.
Kutoza tozo ya shilingi
laki moja na elfu hamsini (150,000/=) kwa siku kwa kila mtu kwa kusindikiza
kemikali hatarishi badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100); na
j. Usafirishaji wa kemikali hatarishi na kemikali
zingine ndani na nje ya nchi utatozwa tozo kama zilivyoainishwa kwenye Jedwali
Na. 3 hapa chini:-
Jedwali
Na 3.
Kiasi cha kemikali
kinachosafirishwa kwa MT
|
Ada ya sasa
(USD)
|
Ada inayopendekezwa
(USD)
|
Kati ya 0.1 - 10
|
1-2
kila MT
|
10
|
10.1 - 200
|
1 kila MT
|
|
201 - 1000
|
400
|
|
1001 - 5000
|
600
|
|
5001 - 10,000
|
800
|
|
10,001- 20,000
|
1,200
|
|
20,001- 40,000
|
1,500
|
|
40,001+
|
2,000
|
Aidha, ili kutimiza
matakwa ya sheria ya kutumia fedha za kitanzania, tozo zote zilizokuwa
zinatozwa kwa dola za kimarekani zitatozwa kwa fedha za Kitanzania isipokuwa
kwa shehena za kemikali zinazoenda nje ya nchi (On-transit). Lengo la hatua
hizi ni kupunguza wingi na ukubwa wa tozo ili kuweka mazingira bora ya biashara
nchini. Aidha, mizigo ya kemikali inayopitishwa katika bandari ya Dar es salaam
itaongezeka na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 450.0
IV.
Wizara
ya Mifugo na Uvuvi- Sekta ya Mifugo
Napendekeza kufuta tozo
mbalimbali kwenye Sekta ya mifugo kama ifuatavyo:-
a.
Kufuta tozo ya shilingi
5,000 ya vibali vya vyombo vya kusafirisha maziwa chini ya lita 51;
b. Kufuta tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa
vituo vya kukusanyia maziwa lita 201 kwa siku;
c. Kufuta tozo ya shilingi 5,000 ya usajili wa
wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 kwa siku;
d.
Kufuta tozo ya shilingi
500,000 ya usajili wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa;
e.
Kufuta tozo ya shilingi
15,000 ya usajili wa wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama;
f. Kufuta tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa
wafugaji wa kati wa mifugo ya nyama;
g.
Kufuta tozo ya shilingi
75,000 ya usajili wa wafugaji wakubwa wa mifugo ya nyama;
h. Kufuta tozo ya shilingi 20,000 ya usajili wa
wasimamizi wa minada ya awali;
i.
Kufuta tozo ya shilingi
30,000 ya usajili wa wasimamizi wa minada ya upili na mipakani;
j.
Kufuta tozo ya shilingi
50,000 ya usajili wa minada ya upili na mipakani;
k.
Kufuta tozo ya shilingi
30,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa minada ya awali;
l.
Kufuta tozo ya shilingi
60,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa minada ya upili na mipakani;
m. Kufuta tozo ya shilingi 100,000 ya usajili wa
wafanyabiashara wa nyama na bidhaa zake nje ya nchi;
n.
Kufuta tozo ya shilingi
1,000 ya kibali cha kusafirisha kuku nchini (vifaranga 100 kwa siku moja); na
o. Kufuta tozo ya shilingi 200 ya kibali cha
kusafirisha kuku mkubwa nchini.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha takribani shilingi milioni 16,689.8
V.
Wizara
ya Maliasili na Utalii
Napendekeza kufuta ada
ya Leseni ya kufanya biashara ya Utalii inayohusisha uwindaji wa kitaalamu (professional
hunting) iliyokuwa inatozwa kwa dola za kimarekani mia mbili (USD 200) kwa raia
wa Tanzania na dola za kimarekani elfu moja (USD 1000) kwa raia wa kigeni.
Lengo la hatua hii ni kupunguza tozo zinazotozwa katika sekta ya utalii, na
kuvutia watalii. Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi
cha takribani Dola za Kimarekani elfu themanini (USD 80,000).
VI.
Wizara
ya Maji
Napendekeza kufuta ada
ya matumizi ya maji kwa watumiaji wenye visima nyumbani ambayo ilikuwa inatozwa
kuanzia shilingi laki moja (100,000/=) na kuendelea kulingana na matumizi ya
maji. Lengo la kufuta tozo hiyo ni kupunguza gharama kwa wananchi wanaochimba
visima vya maji kwa matumizi binafsi nyumbani na kuwezesha upatikanaji wa maji
hayo kwa gharama nafuu. Hata hivyo, ili kudhibiti uchimbaji holela wa visima,
itabidi visima hivyo viendelee kusajiliwa na Bodi za Maji za Mabonde.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,961
Aidha, Serikali
itaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa Mpango wa
kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (BLUEPRINT). Lengo ni
kuendelea kuweka mazingira bora ya kuvutia uwekezaji, katika kipindi cha muda
wa kati na muda mrefu. Hatua hii inatoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha
biashara mpya zitakazo ongeza ajira na kukuza uchumi. Kwa kuzingatia kuwa,
Serikali imewekeza katika kuboresha mazingira ya udhibiti wa mazingira ya
biashara, kupitia mpango wa BLUEPRINT, hivyo basi, ni matarajio na wito wa
Serikali kwamba wawekezaji wa ndani na nje, watachangamkia fursa hii kwa
kuanzisha na kuendeleza uwekezaji mpya ili kukuza faida za biashara na kuweza
kulipa kodi stahiki kwa hiari na kuongeza mapato ya Serikali.
j.
Hatua
za Kisera na Kiutawala katika Kuboresha ukusanyaji wa mapato
51.
Mheshimiwa
Spika, napendekeza kuweka
utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini ambapo wananchi wa kawaida
wataruhusiwa kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia Wakala wa
Forodha (Clearing and Forwarding Agents). Hata hivyo, utaratibu huu
hautahusisha mizigo inayopitishwa hapa nchini kwenda nje ya nchi (Transit
Cargo). Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania itaandaa utaratibu wenye kueleweka kwa
urahisi ili kuwawezesha Wananchi kugomboa mizigo yao kwa gharama nafuu zaidi na
bila kuchelewa.
52.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inapendekeza
kuchukua hatua mbalimbali za Kisera na Utawala kwa lengo la kuimarisha na
kurahisisha ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
i.
Ili kuondoa malalamiko
ya wafanyabiashara dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Serikali kupitia Wizara
ya Fedha na Mipango, imeamua kuanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko na
taarifa za kodi (Office of Tax Ombudsman) ambacho kitaratibiwa na Wizara ya
Fedha na Mipango. Aidha, kitengo hiki kitahusisha kupokea na kupitia malalamiko
ya taarifa za Kodi zitakazotolewa na walipakodi au watu wenye nia njema. Baadhi
ya majukumu ya Kitengo hiki ni kama yafuatayo:-
a.
Kupokea malalamiko ya
rushwa dhidi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;
b.
Kupokea malalamiko ya
ukadiriaji wa Kodi na uthamanishaji wa bidhaa usio wa haki wala uhalisia dhidi
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;
c.
Kupokea malalamiko ya
matumizi ya nguvu katika ukusanyaji kodi dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;
d. Kupokea malalamiko ya ufungaji wa biashara bila
kufuata sheria na taratibu dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania; na
e. Kupokea malalamiko pamoja na kero nyingine
zinazofanana na hayo dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
ii.
Ili kuongeza ukusanyaji
wa mapato ya kodi za ndani, serikali inakamilisha manunuzi ya mfumo unganishi
wa kielektroniki (Intergrated Domestic Revenue Adminstration System- IDRAS)
katika kukusanya kodi na mapato yasiyo ya kodi ili kuleta uwazi na ufanisi
katika ukusanyaji wa mapato. Pia mfumo huu utarahisisha ulipaji wa kodi na
kupunguza rushwa miongoni mwa watumishi wasio waaminifu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania;
iii.
Kuendelea kusimamia
matumizi ya mfumo wa kukusanyia kodi wa kielektroniki (Electronic Fiscal
Device Management System) ambao umefanyiwa maboresho makubwa na kuanza kazi
tangu tarehe 1 June, 2019, ili kudhibiti na kubaini udanganyifu unaofanywa
katika matumizi ya mfumo huo. Aidha, hatua hii itadhibiti uvujaji wa mapato
katika urejeshaji wa kodi ( Tax refund), utoaji wa risiti bandia, n.k;
iv.
Kutokana na wimbi la
vijana wengi kujihusisha na michezo ya kubahatisha na kusahau majukumu ya
ujenzi wa taifa, Serikali ikishirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha
imebuni na kutengeneza mfumo maalum ambao utatumika kudhibiti uchezaji wa
michezo hii (Responsible Gaming). Pia, Mfumo huu utatumika kudhibiti
udanganyifu ambao unafanywa na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha ili
Serikali ipate mapato yake halali;
v.
Kutokana na malalamiko
ya walipa kodi kuhusu ukadiriaji wa kodi na uthaminishaji wa bidhaa usio na
haki wala uhalisia, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanzisha
dawati la kushughulikia mapingamizi ya makadirio ya kodi ambapo pingamizi za
uthamanishaji na utambuzi litashughulikiwa ndani ya masaa ishirini na nne (24);
na
vi.
Kutoa unafuu wa kutolipa
kodi kwa kipindi cha miezi sita (6) kuanzia wakati mfanyabiashara au mwekezaji
anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). Hatua hii inatofautiana na
hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN anaanza kufanyiwa tathmini
(tax assessment) ya mapato yake ya biashara na kutakiwa kulipa kodi. Hatua hii
itawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wapya kupata muda wa kujiandaa na mahitaji
yanayotakiwa katika shughuli wanazofanya na kuondoa usumbufu au dhana ya woga
wakati wa kuanzisha biashara. Mfano kuna mahitaji ya Leseni ya biashara na
vibali vingine muhimu.
k.
Tarehe
ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.
53.
Mheshimiwa
Spika, hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2019, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
V.
SURA
YA BAJETI KWA MWAKA 2019/20
54.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia shabaha,
malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2019/20, Sura ya Bajeti inaonesha
kuwa jumla ya shilingi trilioni 33.11 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika
katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri)
yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 23.05, sawa na asilimia 69.6 ya bajeti
yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla
ya shilingi trilioni 19.10 sawa na asilimia 12.9 ya Pato la Taifa. Mapato
yasiyo ya kodi kwa mwaka 2019/20 yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 3.18 na
mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Shilingi bilioni 765.5.
55.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatarajia
kukopa shilingi trilioni 4.96 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho,
shilingi trilioni 3.46 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za
Serikali zinazoiva na kiasi cha Shilingi bilioni 1.50 sawa na asilimia 1.0 ya
Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Kwa
lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, Serikali
inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.32 kutoka soko la nje kwa masharti ya
kibiashara.
56.
Mheshimiwa
Spika, Washirika wa Maendeleo
wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 2.78 ambayo ni asilimia 8 ya bajeti.
Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo shilingi trilioni 2.31;
Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 199.5; na Misaada na Mikopo nafuu
ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) shilingi bilioni 272.8.
57.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2019/20,
Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 33.11 kwa matumizi ya
kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 20.86 zimetengwa
kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.0 ya bajeti, ikijumuisha
Shilingi trilioni 9.72 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na shilingi
trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara. Aidha, shilingi trilioni 3.58 ni kwa
ajili ya Matumizi Mengineyo (Other Charges-OC) ikijumuisha shilingi bilioni
460.5 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya Halmashauri.
Aidha, kwa mwaka 2019/20, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
58.
Mheshimiwa
Spika, matumizi ya maendeleo
yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 12.25, sawa na asilimia 37.0 ya bajeti
yote, ambapo kiasi cha Shilingi trilioni 9.74 ni fedha za ndani na shilingi
trilioni 2.51 ni fedha za nje. Kati ya fedha za maendeleo zilizotengwa,
shilingi trilioni 2.48 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard
Gauge; shilingi trilioni 1.44 ni kwa ajili ya mradi wa kufua umeme Mto
Rufiji; shilingi bilioni 788.8 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na REA;
shilingi bilioni 450 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na
shilingi bilioni 288.5 kwa ajili ya elimu msingi bila ada. Aidha, Serikali
imetenga jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni
yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na
umeme.
59.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti
kwa mwaka 2019/20 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa
Bajeti ya Mwaka 2019/20
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
VI.
HITIMISHO
60.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ni nyenzo ya
kufikia matarajio ya wananchi wetu. Hivyo, katika kuandaa bajeti hii, Serikali
iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo, Kamati ya Bunge ya Bajeti,
wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi, wananchi wa kawaida, na wataalam
wa kodi hususan wale walioshiriki vikao vya kazi vya kikosi kazi cha maboresho
ya kodi (Task Force and Think Tank) kujadili na kushauri juu ya
mapendekezo ya maboresho ya kodi na tozo mbalimbali. Baadhi ya wadau
walituletea maoni na ushauri kwa maandishi au barua pepe. Nakiri kuwa
walitupatia mrejesho ambao umesaidia kuboresha será na vipaumbele vya
nchi yetu kwa mwaka 2019/20 na siku zijazo. Napenda kwa niaba ya Serikali
kuwashukuru sana kwa michango hiyo mizuri ambayo tumejitahidi kuizingatia. Ni
matarajio ya Serikali kwamba wadau hao wataendelea kufanya hivyo katika
mchakato wa bajeti zitakazofuata.
61.
Mheshimiwa
Spika, bajeti ya 2019/20
inahusu kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua
fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa
jamii na hatimaye kuondokana na umaskini, ujinga na maradhi. Hususan,
bajeti hii imelenga:
i.
Kuimarisha na kujenga
miundombinu ya kisasa ili kuongeza uwezo wa Taifa katika uzalishaji viwandani
hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini na kutoa
huduma bora (afya, elimu na maji) kwa wananchi. Aidha, miundombinu hiyo itasaidia
kuongeza biashara nchini, kikanda na kimataifa;
ii.
Kujenga mazingira mazuri
ya kufanya biashara na uwekezaji kwa kushughulikia changamoto zilizobainishwa
katika mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint);
iii.
Kuimarisha kilimo
(uzalishaji wenye tija na masoko ya mazao, ufugaji, uvuvi, na misitu) kwa
kuzingatia umuhimu mkubwa wa sekta hii katika uchumi wa Taifa (chakula, ajira,
kipato cha mwananchi, mchango katika fedha za kigeni na muunganiko wa sekta hii
na maendeleo ya viwanda);
iv.
Kudumisha amani na
usalama katika Taifa; na Kujenga misingi ya Taifa kujitegemea kiuchumi
62.
Mheshimiwa
Spika, safari ya kuijenga
Tanzania mpya imeiva lakini haitakuwa rahisi hasa tukizingatia mabadiliko
yanayoendelea katika uchumi wa dunia, ushindani mkali wa kibiashara, mabadiliko
ya haraka ya teknolojia na demografÃa na changamoto zinazotokana na mabadiliko
ya tabianchi. Hata hivyo, bahati nzuri ni kuwa, katika historia ya nchi yetu,
Watanzania ni watu jasiri katika mapambano dhidi ya changamoto zinazojitokeza
na kila wakati zilipojitokeza tulizishinda kwa kutumia ubunifu na nguvu
ya umoja wa Watanzania.
63.
Mheshimiwa
Spika, hivi sasa tuko imara
zaidi chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Uchumi wetu unaendelea kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka 2018 ulikua kwa
asilimia 7.0 na kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kinazidi
kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18.
Naamini pasipo shaka yoyote kwamba kwa umoja wetu, uongozi makini, kufanya kazi
kwa bidii na kwa kutumia rasilimali za nchi yetu vizuri, tutaijenga Tanzania
mpya, ambayo itakuwa kitovu kikuu cha uchumi (Economic hub) katika ukanda wa
Afrika Mashariki katika muda usiozidi miongo miwili ijayo.
64.
Mheshimiwa
Spika, ninapoelekea mwisho wa
hotuba hii, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo
kwa misaada na mikopo nafuu wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na
programu mbalimbali za maendeleo nchini. Katika bajeti ya mwaka 2019/20, Washirika
wa Maendeleo kwa pamoja wanatarajia kuchangia jumla ya shilingi trilioni 2.78.
Naomba niwatambue kwa kuwataja mmoja mmoja: Nikianza na nchi za Canada, China,
Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Japan, Korea ya Kusini, Marekani,
Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, Uingereza, na
Uswisi. Aidha, zipo taasisi za kimataifa ambazo ni: Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), Benki ya Dunia, Arab Bank for Economic Development in Afrika
(BADEA), Global Fund, Kuwait Fund, Abu Dhabi Fund, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya
(EU), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), OPEC Fund, Global Environmental
Facility (GEF), Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mfuko wa kukinga
Hatari ya Kimazingira (GRMF), Climate Development Special Fund, African Legal
Support Facility (ALSF), Dignity, Global Agriculture and Food Security Program
(GAFSP),na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF, IFAD, UNDP, UNFPA,
Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), na United Nations Environment Programme
(UNEP). Napenda pia kutambua uhusiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF). Ni matarajio yetu kuwa misaada ya kiufundi na fedha
zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi
kilichoahidiwa. Nasi kwa upande wa Serikali tunaahidi kutumia misaada hiyo kama
ilivyokusudiwa.
65.
Mheshimiwa
Spika, napenda nitumie nafasi
hii kuwahimiza Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na taasisi
za kimataifa hapa nchini Tanzania waongeze nguvu kukuza biashara kati ya nchi
zao na nchi yetu na kuhamasisha wenye mitaji toka nchi zao kuja kuwekeza hapa
Tanzania. Tanzania ni salama kwa uwekezaji wenye faida kwao na kwetu. Aidha,
wafanye jitihada zaidi kuhamasisha watalii kuja kujionea vivutio vya utalii,
ambavyo ni fahari ya Tanzania.
66.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Awamu ya
Tano inatambua na kuthamini michango yao katika maendeleo ya Taifa letu ili
mradi isiambatane na masharti yanayohatarisha uhuru wa Tanzania (national
sovereignity), au kwenda kinyume na mila na desturi zetu. Hata pale ambapo
Serikali au mihimili mingine imefanya maamuzi ambayo hawakubaliani nayo, ni
vema na haki washirika wetu wa maendeleo watupe muda wa kuyatafakari na
kujadiliana nao kwa staha badala ya kuishinikiza Serikali ibadili uamuzi wake
ndipo watoe fedha, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.
67.
Mheshimiwa
Spika, kwa Watanzania wenzangu,
napenda kuwasisitiza tuendelee kushikamana katika kuijenga Tanzania mpya. Tuwe
wazalendo na tena tukae macho daima kulinda na kutetea maslahi ya Taifa letu.
Tuongeze bidii kufanya kazi. Enzi za kutegemea wajomba hazipo tena na habari
njema ni kuwa: “Tukiamua Tunaweza” na Serikali ya CCM inayoongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imethibitisha ukweli huo.
68.
Mheshimiwa
Spika, naomba kwa niaba ya
Serikali kupongeza mchango mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi wote ambao
wamelipa kodi kwa mujibu wa sheria. Aidha, napenda kutambua mchango adhimu wa
mashirika na taasisi ambazo Serikali ina hisa yaliyotoa gawio au asilimia 15 ya
mapato ghafi kuingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Katika mwaka ujao wa fedha,
Serikali inayataka mashirika yote ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa
kuhakikisha kuwa wanatoa gawio au mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi na
Msajili wa Hazina asimamie kikamilifu utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali.
69.
Mheshimiwa
Spika, kama mnavyofahamu, mwezi
Oktoba mwaka huu wa 2019 tutafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Serikali kwa
upande wake imejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya
kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo. Ninawasihi wananchi wote wenye
sifa wajitokeze kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. Aidha, katika
kuchagua viongozi wa ngazi hiyo, tafuteni Watanzania wenye sifa zifuatazo:
i.
Awe mchapakazi mwenye
kujitoa sadaka kuwatumikia watu, hasa wananchi wa kawaida;
ii.
Awe mwepesi kuona, kusikiliza
na kuguswa na shida za wananchi wake. Tena awe jasiri katika kupigania haki za
wanyonge na awe na uwezo na ubunifu katika kutatua kero za wananchi hao;
iii.
Awe mwadilifu,
anayechukia na kupiga vita rushwa na ufisadi kwa matendo;
iv.
Anayetambua fursa
zilizopo katika eneo lake, kubuni mikakati ya kuwaendeleza wananchi
anaowaongoza na kuwatia watu wake hamasa ya kuthubutu kutumia fursa hizo;
v.
Awe mtetezi hodari wa
kulinda mazingira na mpambanaji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi;
vi.
Mwenye kutoabudu nyadhifa;
anayetambua kuwa nafasi na vyeo tulivyopewa ni vya muda tu. Ni vya kupita!
Thamani halisi ya kiongozi ni kufanya kazi kwa bidii na kuacha kumbukumbu nzuri
kwa ustawi wa eneo analoliongoza na Taifa kwa ujumla;
vii.
Awe kama mchezaji mzuri
wa kiungo katika timu ya ushindi, anayetambua kwamba mkono mmoja hauwezi kupiga
makofi ya shangwe;
viii.
Awe mwenye kutambua
kwamba kazi za kiongozi zina maana sana kwa kuwa zinamwezesha kubadilisha
maisha ya maelfu ya Watanzania, hasa wanyonge, kuwa bora zaidi;
ix.
Awe na uwezo wa kuwaeleza
wananchi kinaganaga kuhusu Serikali yao inawapeleka wapi na wajibu wa kila
mmoja ili waendelee kuiunga mkono; na
x.
Awe anatoka ndani ya
chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni CCM!
Naomba nikiri kuwa, sifa
hizi nilizozitaja nimeziazima kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ridhaa yake!
70.
Mheshimiwa
Spika, nawaomba viongozi wote
wa dini pamoja na waumini wote kila mmoja kwa imani yake, tuendelee kumwombea
Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili Mwenyezi Mungu
aendelee kumjalia afya njema, hekima, busara na kumwongoza kwa kila jambo
alifanyalo kuliletea Taifa letu maendeleo.
71.
Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie
fursa hii kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambao
wamekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na maandalizi
na uratibu wa bajeti hii ya Watanzania. Kipekee ninawashukuru Mheshimiwa Dkt.
Ashatu K. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye ni Mbunge mahiri wa
Jimbo la Kondoa; Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bwana Doto M.
James, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Bi. Amina Kh. Shaaban, Dkt.
Khatibu M. Kazungu na Bwana Adolf H. Ndunguru pamoja na watumishi wa ngazi zote
wa Wizara ya Fedha na Mipango. Vile vile, ninamshukuru Profesa Florens D.
Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Naibu Gavana Dkt. Yamungu
Kayandabila, Dkt. Bernard Kibesse na Bwana Julian Raphael Banzi kwa kusimamia
vema sekta nyeti ya fedha. Kwa nafasi ya kipekee, napenda nimpongeze Dkt. Edwin
Mhede kwa kuteuliwa na Rais kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA). Ni matumaini yangu na ya Watanzania kuwa atakuwa chachu ya kujenga
taswira mpya ya TRA itakayoongeza mapato ya Serikali bila manyanyaso kwa
wafanya biashara.
72.
Mheshimiwa
Spika, ninawashukuru viongozi
na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa utekelezaji mzuri wa
majukumu yao. Nawashukuru Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Taasisi na Wakala za
Serikali zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wafanyakazi wake
wote kwa kazi nzuri wanazofanya na kuendelea kunipa ushirikiano wa dhati
katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi wa hali ya juu.
73.
Mheshimiwa
Spika, niwashukuru pia
wananchi wenzangu wa Wilaya ya Buhigwe na mkoa wetu wa Kigoma ambao walinilea na kunifundisha
kufanya kazi. Mwisho kabisa naishukuru familia yangu, hususan mke wangu mpenzi
na rafiki yangu Mbonimpaye, watoto, wajukuu, ndugu, jamaa na marafiki zetu wote
tuliopewa na Mungu. Asanteni kwa kuniombea msaada wa Mungu katika kazi hii,
usiku na mchana. Nami ninasema kwa kila mmoja wao:
“Bwana akubarikie na
kukulinda,
Bwana akuangazie nuru za
uso wake, na kukufadhili,
Bwana akuinulie uso
wake, na kukupa amani”
Hesabu 6: 24-26.
Nimalizie kwa kumshukuru
sana Mwenyezi Mungu kwa baraka zake na kuniwezesha kuwasilisha hotuba hii.
Aidha, apende kuendelea kunijalia uwezo na unyenyekevu wa kulitumikia Taifa
letu na wananchi wake kwa uadilifu. Asanteni sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania
wote kwa kunisikiliza.
MUNGU IBARIKI AFRIKA,
MUNGU IBARIKI TANZANIA
74.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment