Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde (kulia) akitekeleza majukumu yake. |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Wende Ng’ahara wamalize tofauti zao na wasipojirekebisha atamshauri Rais Dkt. John Magufuli kufanya maamuzi mengine.
Amesema kitendo cha viongozi hao kutoelewana kinaonesha mfano mbaya kwa watumishi walio chini yao, hivyo amewataka wajirekebishe mara moja kwani wameaminiwa na Serikali kuliongoza eneo hilo na si kuwachanganya wananchi.
Waziri Mkuu ametoa kalipio hilo Februari 20, 2019 wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mpira wa shule ya msingi Nyakanazi, kijiji cha Nyakanazi, Biharamuko mkoani Kagera.
Amesema kutokuelewana kwa viongozi hao ambao wakati mwingine wanatuhumiana kufanyiana vitendo vya kishirikina kumesababisha kuzorota kwa shughuli za maendeleo katika wilaya.
“Mliletwa hapa kuiwakilisha Serikali na kusimamia maendeleo ya wananchi nyie mnagombana.” Awali, Waziri Waziri Mkuu akiwa njiani kuelekea mkoani Kagera alitembelea kambi ya Nyanza Roads inayojenga barabara ya Nyakanazi-Kabingo, inayounganisha mikoa ya Kigoma na Kagera na kusema kuwa hajaridhishwa na kasi ya mkandarasi huyo.
Barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami inaurefu wa kilomita 50 na ilianza kujengwa 2014 ilitarajiwa kukamilika 2016, ambapo kwa sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 60.
“Sijaridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hii, mkandarasi na mhandisi mshauri wote wanaonekana hawapo makini katika kufanya kazi hii. Hii ni aibu kwa wakandarasi wa ndani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kutokupewa kazi kumbe hawako makini.”
No comments:
Post a Comment