%20Tanzania,%20Emil%20Hagamu%20akizungumza.jpg)
Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania, Emil Hagamu akizungumza.
Na Frida Manga
SHIRIKA la Kutetea Uhai Nchini Tanzania (Pro-Life) limeanzisha programu maalum ya miezi mitatu yenye lengo la kuhimiza kulindwa na kuheshimisha uhai wa binadamu, kufuatia wasiwasi unaoibuliwa na Mswada wa Ujinsia na Afya ya Uzazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotarajiwa kujadiliwa na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika hilo Emil Hagamu mswada huo unatishia misingi ya uhai, ndoa, familia na malezi ya watoto kwa kupendekeza matumizi ya vidhibiti mimba kwa watu wote bila kuzingatia umri, hali ya ndoa wala maadili ya jamii. Aidha, unapendekeza kuruhusu utoaji wa mimba katika vituo vinavyodaiwa kuwa salama, pamoja na kuwapa watoto uhuru wa kufundishwa masuala ya ngono bila vikwazo, ukipuuza nafasi ya mila, desturi na maadili ya Kiafrika katika malezi.
Pro-Life Tanzania imesema mapendekezo hayo yanakinzana na Katiba ya nchi, inayotambua na kulinda haki ya kila binadamu kuheshimiwa na kuthaminiwa uhai wake. Shirika hilo limeiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kusimama kidete kukemea sera na sheria zinazodhoofisha thamani ya uhai wa binadamu, hususan vitendo vya utoaji mimba.
Kupitia programu hiyo, shirika linatumia misingi ya utamaduni na dini kuhimiza heshima ya uhai kadri ya uumbaji wa Mungu, pamoja na kurejesha maadili, miiko na heshima ya mtu katika jamii ya waafrika hasa katika muktadha wa ndoa, familia na malezi ya watoto.
Hagamu amesema Programu hiyo imeanza kutekelezwa katika mikoa ya Songea, Mbeya na Arusha, na inalenga kuwafikia wananchi wote, hususan wanafunzi, viongozi wa dini na viongozi wa jamii, kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa uhai na kuheshimisha thamani ya maisha ya binadamu.

No comments:
Post a Comment